Mahakama ya Mwanzo ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro imetoa
talaka baada ya mdai ambaye ni mwanaume mkazi wa Himo kuieleza mahakama hiyo
kuwa mdaiwa ambaye ni mwanamke alimtelekeza kwa muda mrefu na kumwachia watoto
bila kujua wanaishi vipi wala kula nini.
Hayo yamejiri baada ya mdai aliyefahamika kwa jina la Solomon
George Mongi (60) kudai talaka dhidi ya Marry Benjamin Shayo. Hakimu Mkazi wa
mahakama hiyo Adnan Kingazi alisema mahakama baada ya kupokea ushahidi
ilijiuliza hoja za msingi kama ndoa ilikuwa ya halali kati ya mdai na mdaiwa;
kama kuna mgogoro kati ya wanandoa hao na jitihada za kuusuluhisha zimefanyika bila
mafanikio.
Pia ilielezwa mahakamani hapo kama mdai anazo sababu za
kisheria pamoja na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa ndoa yao imevunjika
moja kwa moka na kama anastahili talaka;
Aidha mahakama ilijiuliza kama kuna ushahidi wa mali
walizochuma pamoja wanandoa hao na kwamba nani mwenye wajibu wa kutunza na
kuishi na watoto waliozaliwa na wanandoa hao. Hakimu Mkazi Kingazi alisema baada
ya mahakama kuchambua kwa kina hoja hizo ilibaini kuwa mdai baada ya
kuthibitisha madai yake ya talaka kupitia Kifungu cha 101 cha Sheria ya Ndoa za
Mwaka 1971 kinachosema, “ Si ruhusa kwa mtu yeyote kufungua madai ya talaka
isipokuwa tu pale atakapokuwa ametanguliza kuupeleka mgogoro wao wa ndoa kwenye
Baraza la Usuluhishi wa Ndoa na Baraza hilo kutoa hati ya kuthibitisha kuwa
imeshindwa kuwasuluhisha wanandoa hao.”
Kingazi alisema kifungu cha 110 (1) cha Sheria ya Ndoa ya
Mwaka 1971 kimeridhia maombi ya mdai kuwa anastahili kupewa talaka. Mbali na maamuzi ambayo mdai alipata stahili
ya talaka yake mahakama hiyo iliamuru kufanywa kwa tathmini ya nyumba mbili za
wadaawa ili ziuzwe kisheria na hatimaye wadaawa hao wagawane kiasi
kitakachopatikana.
Aidha mahakama iliamuru taratibu za kusajili talaka na
kuondoa usajili wa ndoa ya wadaawa kwenye mamlaka husika zifanyike na Mdaiwa
amlipe mdai gharama za shauri hilo pamoja na usumbufu wote uliojitokeza tangu
alipomtelekeza na watoto mwaka 2007 amekaa mpweke kwa miaka 12 sasa.
Awali Mdai aliwasilisha shauri la Madai ya Talaka na mgawanyo wa mali katika mahakama hiyo kwamba
mdaiwa alikosa uaminifu kipindi chote cha ndoa. Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba
kipindi chote cha shauri hilo mdaiwa alipuuzia wito wa mahakama hivyo shauri
hilo likasikilizwa upande mmoja.
Ilidaiwa mahakamani hapo
Mdai alishawahi kumfumania mdaiwa akiwa na mwanaume maeneo ya stendi
kubwa ya Moshi wakiwa kwenye teksi na
kwamba kama asingekuwa uvumilivu angeweza kufa kwa pressure kwani mdaiwa
alifikia hatua ya kutaka kuuza nyumba yao iliyopo Pasua.
Ilidaiwa mahakamani hapo Mdai alipeleka shauri lake katika
Baraza la Usuluhishi la Kata ya Bomambuzi
Matindigani lakini mdaiwa alikataa kuitia wito wa baraza hilo.
Mdai ambaye ni fundi magari alifunga ndoa takatifu ya
Kikristo tarehe 4 Februari 1998 katika Kanisa la Kilutheri la Samanga
na kubahatika kupata watoto watatu ambao ni John (34), Benjamin (25) na
Praygod (19).
STORY BY: Jabir Johnson
0 Comments:
Post a Comment