Friday, June 7, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Kanali Muammar Gaddafi na Afrika Moja


Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake. 

Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969. Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani. 

Anaweza kuchukiwa kwa mengi, lakini ukweli lazima usemwe kwamba huyu ni kiongozi aliyesimama imara kupinga ukoloni wa aina yoyote na wala asiyeogopa kusema lolote dhidi ya wakoloni. Gaddafi aliwahi kuwaambia watu wake kuwa viungo vinavyotengeneza Coca Cola na Pepsi vinatoka Afrika, kwa hivyo Waafrika walipaswa kutengeneza soda hizo wenyewe. Aliupa msukumo mkubwa Umoja wa afrika kwa hali na mali. 

Akijiita Mfalme wa Wafalme wa Afrika, Gaddafi alitoa mabilioni ya fedha kuendeleza miundombinu ya utalii katika mataifa rafiki. Lakini katika medani ya kimataifa, jina lake liliingia doa kubwa baada ya kubainika kuwa alikuwa akitoa mafunzo kwa makundi ya kigaidi, likiwemo la RAF la Ujerumani na IRA la Ireland ya Kaskazini. Alishukiwa pia kuhusika na mashambulizi katika klabu ya burudani jijini Berlin. Aliwahi pia kuwa pia muungaji mkono wa waasi wa Chad na Ghana. Kubwa katika yote, ni mashambulizi dhidi ya ndege ya abiria ya Shirika la Pan Am katika anga ya Lockerbie, Scotland.

MAISHA YAKE YA UTOTONI
Unaweza kumuita Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi Alizaliwa karibu na kijiji kimoja kilichokuwa nje ya mji wa Sirte nchini Libya cha Qasr Abu Hadi katika eneo la jangwa magharibi mwa taifa hilo la Libya. 

Mama yake alifahamika kwa jina la Aisha ambaye alifariki mwaka 1978 na baba yake Mohammad Abdul Salam bin Hamed bin Mohammad ambaye alikuwa akifahamika kama Abu Meniar alifariki dunia mwaka 1985. Jamii aliyotoka Gaddafi ilikuwa ni jamii ya wasiosoma ambayo ilikuwa haitunzi rekodi zake hususani zile za kuzaliwa kutokana na mfumo wa kuhamahama. Wabedui walikuwa wafugaji wa mbuzi na ngamia ambao walikuwa hawakai sehemu moja. 

Hata waandishi wa historia wa Gaddafi David Blundy na Andrew Lycett  walinukuriwa katika maandishi yao kuwa Gaddafi alizaliwa kabla ya 1940. Wazazi wa Gaddafi walibahati kuwa na watoto wengine watatu wa kike. Aliongoza Libya tangu alipompindua Mfalme Idris I, katika mapinduzi yasiyo ya kumwaga damu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 27 mwaka 1969. Alikuwa maarufu kwa nguo alizopenda kuvaa, na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa, kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani. 

Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am na hapo Umoja wa Mataifa ukaondoa vikwazo dhidi ya Libya. Baada ya miezi kadhaa, serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za magharibi. 

Hapo ndipo mabadiliko halisi yalionekana kwa kuwa nchi hizo za magharibi zilibadili mtazamo wao na kuacha kumtenga Gaddafi na kushirikiana naye hata kama alikuwa hatabiriki. Kwa mujibu wa mtaalamu mmoja wa siasa za Libya Saas Djebbar wakati fulani alikaririwa akisema Gaddafi Ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, “Lakini ni mwanasiasa mashuhuri; hakuna shaka lolote kuhusu hilo. 

Ni mwanasiasa anayeweza kuhimili misukosuko ya kisiasa kwa hali ya juu sana,” alisema mtaalamu huyo wa siasa. Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri na, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956. Gaddafi alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi na aliwahi kupata mafunzo zaidi akiwa Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya, mji wa Benghazi, na kupanga mapinduzi ya  Septemba 1, 1969. 

Gaddafi alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi. Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa iliyojumuisha kanuni za kiislamu na mfumo uliyo tofauti na siasa za ujamaa au ubepari. Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'. Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine. Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa anakaa kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume. 

Hema hiyo pia ilikuwa ikitumiwa  kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi alikuwa akiendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende. Benjamin Barber, mtaalam wa kisiasa wa kujitegemea, kutoka Marekani aliwahi kukutana na Gaddafi mara kadhaa hivi enzi za uhai wake na kuzungumza naye kuhusu mustakabali wa Libya. Muammar Gaddafi na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair waliwahi kuandaa mkutano wa viongozi kutoka nchi mbalimbali  Mei 29, 2007 kwenye hema hiyo ya Kibedui. Kanali Gaddafi alijitahidi kwa muda mrefu kutoa ushawishi wake nyumbani na ng'ambo. 

Awali alituma jeshi lake nchini Chad ambapo wanajeshi walidhibiti ukanda wa Aozou, kaskazini mwa nchi hiyo, mwaka 1973. Katika miaka ya 80 aliandaa mafunzo kwa makundi ya waasi kutoka Afrika Magharibi yaliyojumuisha wale wa Tuareg ambao ni Waberiberi.

Jumuiya ya wanadiplomasia ilimua kuitenga kutokana na Kanali Gaddafi kuunga mkono makundi yenye silaha, ikiwemo Irish Republican Army na Palestina PLO .Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986. Ilisemekana kuwa Kanali Gaddafi alitikiswa na mashambulio ya mabomu hayo ambapo mtoto wake wa kike wa kufikia aliuawa. 

Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika. Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara la Afrika. Wakati wa mabadiliko katika karne ya 20, huku Libya ikiwa inapata tabu kutokana na vikwazo dhidi ya nchi hiyo, alianza kurekebisha hali nchini mwake. Mwaka wa 2003, mabadiliko yakaanza kuonekana na baada ya miaka mitano mkataba wa kulipa fidia kwa waathirika wa Lockerbire uliafikiwa na hii ikarejesha uhusiano kati ya Washington na Libya. 

Lakini katika hali halisi, wakosoaji wanasema Kanali Gaddafi alifanikiwa kuidhibiti nchi hiyo.Wanaompinga walikuwa wamekandamizwa kikatili na kwamba vyombo vya habari vilibaki katika udhibiti mkubwa wa serikali. Libya ilikuwa na sheria ambazo haziwaruhusi watu kukusanyika katika misingi ya kisiasa zinazopinga mapinduzi ya Kanali Gaddafi. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema serikali hiyo imewatia mbaroni mamia ya raia kwa kukiuka sheria hiyo na baadhi yao kuhukumiwa kifo.

MWISHO WA UTAWALA WA GADDAFI
Utawala wa Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya ulifikia kikomo Oktoba 20, 2011 baada ya kiongozi huyo kuuawa katika mapigano na waasi waliokuwa wakiungwa mkono na mataifa ya magharibi kwa takribani miezi minane ya kumwondoa madarakani. 

Gaddafi alipoteza maisha kutokana na majeraha aliyoyapata katika mapigano hayo, yaliyosababisha kujeruhiwa vibaya katika miguu yake, na kufariki dunia muda mfupi baadaye. Kwa mujibu wa taarifa za viongozi wa Serikali ya Mpito Libya (NTC), kiongozi huyo alifariki dunia baada ya kukamatwa katika mji wa Sirte alikozaliwa. Hata hivyo, habari za kuuawa kwake zilijaa na utata kutokana na kuelezwa mazingira tofauti. Mmoja wa walioshuhudia mauaji hayo, Abdel Majid Mlegta ambaye ni mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu wa NTC, katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), alisema kuwa kiongozi huyo alikufa baada ya kupigwa risasi kichwani. 

Abdel Majid aliiambia Reuters kwamba mbali na kupigwa kichwani, Kanali Gaddafi, alikamatwa baada ya kujeruhiwa miguu yote miwili, wakati akijaribu kukimbia na msafara ambao ulishambuliwa na ndege za NATO. Mauaji hayo ambayo yalikuja baada ya kukamatwa, ni miongoni mwa mapinduzi  makubwa zaidi katika ukanda wa nchi za Kiarabu ambayo yalizing'oa tawala za Misri na Tunisia  Pia katika mapigano hayo Kamanda wa Brigedia ya 11, Abdul Hakim Al Jalil, alisema kuwa Mkuu wa majeshi ya Kanali Gaddafi, Abu Bakr Younus Jabr naye aliuawa, na alishuhudia mwili wake.  

Pia, Ofisa mwingine wa NTC, alisema kuwa pia Moussa Ibrahim, msemaji wa Gaddafi, alikamatwa karibu na mji wa Sirte, alikouawa bosi wake. Taarifa nyingine za mauaji ya Gaddafi zilisema mmoja wa wapiganaji vijana, aliyejitambulisha kwa jina la Mohammed (20) ambaye alikutwa akiwa amevaa kofia yenye maandishi yaliyosomeka New York Yankees, alisema kuwa Kanali Gaddafi alikutwa akiwa amejificha kwenye shimo ardhini. 

Aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa kiongozi huyo wa zamani, baada ya kukamatwa aliwaeleza wapiganaji wasimpige risasi. Mpiganaji huyo wa waasi alisema kuwa baada ya kujeruhiwa alisafirishwa kwa gari la wagonjwa hadi katika mji wa Misrata.  Baada ya kupata taarifa hizo, milio ya meli na magali ilisikika katika mji huo huku milio ya risasi ikisikika hewani na watu wakishangilia.

Haijulikani hadi leo ni wapi alipozikwa kiongozi huyo baada ya kuuawa kwake.

KILICHOPO SASA BAADA YA GADDAFI KUUAWA
Baada ya rais wa Libya Muammar Gaddafi kuuawa Oktoba 20 mwaka 2011 mjini Syrte na wapiganaji waliojinasibu kupigania mabadiliko; makundi kadhaa yameoneonekana kukita mizizi yake nchini humo na kuendesha mapigano huku raia wakitaabika na kujuta. 

Raia waliohojiwa wanasema wakati wa utawala wa Gaddafi hali ilikuwa nzuri isiyokuwa na mfano licha ya matatizo madogo kuweza kujitokeza. Kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya, raia wa Libya wanaonekana wakiwa na kumbukumbu nzuri za utawala wa Gaddafi. Makundi yanayojinasibu kupigana vita vitakatifu yanaendesha mauaji kila kukicha na kushindwa kuafikiana katika michakato ya amani. 

Kwa sasa majeshi ya Field Marshal Khalifa Haftar ambaye alikuwa kamanda katika utawala wa Gaddafi anaonekana tishio zaidi nchini Libya. Utulivu hakuna katika ardhi hiyo. 

IMETAYARISHWA NA; Jabir Johnson (2019)

0 Comments:

Post a Comment