Saturday, June 15, 2019

Ali Kiba, Diamonds Platinumz kumuunga mkono Dkt. Kigwangalla kupanda Mlima Kilimanjaro


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamis Kigwangalla, ametangaza kuunda timu malumu ya watu mashuhuri ya kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni mwezi Septemba mwaka huu,  kwa malengo ya kuhamasisha utalii wa ndani na  kuchangia fedha katika mfuko wa mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kupitia njia hiyo.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati akikabidhi Bendera ya Taifa kwa wapanda mlima Kilimanjaro 32 na waendesha baiskeli 48, kuzunguka mlima mlima Kilimanjaro kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kupitia changamoto ya kupanda mlima Kilimanjaro ya Geita Gold Mine (GGM) dhidi ya Ukimwi.

“Mwezi Septemba mwaka huu nitapanda Mlima Kilimanjaro kuhamasisha Utalii wa ndani na kuchangia fedha kwa ajili ya changamoto hii ya mapambano dhidi ya Ukimwi yalioasisiwa na GGM Kili Challenge, sitapanda peke yangu  nitahamasisha na makundi mengine wakiwemo Wasanii wa mziki wa kizazi kipya ili tupande mlima Kilimanjaro, ” alifafanua Dkt. Kigwangalla.

“Mwaka jana nilipanga kupanda mlima, bahati mbaya nilipata ajali nikashindwa kutimiza azma hiyo, kwa sasa tayari nimeshaanza mazungumzo na wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya kama Alikiba, Diamond, Lady Jay  Dee, na Mrisho Mpoto, ili waniunge mkono…” alisema Dkt Kigwangalla.

Aidha Waziri huyo aliendelea kufafanua kuwa, tutapanda mlima Kilimanjaro kwa pamoja  kuhamasisha utalii wa ndani na kuhamasisha uchangiaji wa mfuko wa Tume ya taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ili kuunga mkono jitihada za GGM na tume hiyo  kwa kushiriki zoezi la uchangiaji .

Waziri Dkt Kigwangalla amewaalika na Mawaziri, Wanasiasa, Wabunge Wawekezaji na Wafanyabiashara waanze kujiandisha ili kupata timu ya kutosha.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment