Saturday, June 15, 2019

GGM yapongezwa Kampeni ya Kupanda Mlima Kilimanjaro



SERIKALI imeupongeza uongozi wa mgodi wa uchimbaji wa dhahabu wa  Geita (GGM) kwa kuanzisha kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro (GGM Kilimanjaro Challenge against HIV and AIDS) ambayo alisema  mbali na vita dhidi ya UKIMWI, pia imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa Taifa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Waziri wa Maliasili na Utalii Dr. Khamis Kigwangalla, wakati wa hafla ya kuwaaga wapanda mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli, kwa ajili ya kampeni hyo mwaka huu, iliyofanyika katika lango la kupandia mlima huo mrefu Barani Afrika la Machame.

“Ninaelewa kuwa mbali na lengo lake kuu la kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI, programu hii pia imetoa mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania hususan wale wanaokuja kupanda Mlima Kilimanjaro," alisema.

Aliongeza, "Baada ya kampeni hii Kili Challenge, washiriki wanaotoka nje ya nchi hurudi kwao na kuwaleleza wenzao kuhusu mlima Kilimanjaro na maajabu yake pamoja na ukarimu wetu Watanzania na hili hupelekea wengi wao kuamua kuja kuitembelea Tanzania, hivyo kuongeza idadi ya watalii hapa nchini”, alisema.

Dkt. Kigwangalla, aliendelea kusema kuwa anatarjia kupanda mlima Kilimanjaro mwezi mwaka huu, kwa lengo la kutunisha mfuko wa kitaifa wa mapambano dhidi ya UKIMWI (ATF) sambamba na wakati huo huo kuutangaza utalii wa ndani. 

Dk. Kigwangalla aliipongeza Bodi ya Kili Trust ambayo alisema kwa kushirikiana na GGM Limited, Tume ya Tanzania ya UKIMWI (TACAIDS) pamoja na wadau wengine katika kuiendesha kampeni ya GGM Kilimanjaro Challenge kumechangia ustawi wa Watanzania wengi haswa wale walioambukizwa na walioathiriwa na VVU pamoja na UKIMWI kwa njia moja au nyingine.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGM Limited Br. Richard Jordinson, alisema hadi sasa jumla ya shilingi Bilioni 13 zimeshakusanywa tangu kuanzishwa kwa kapeni ya GGM Kilimanjaro Kili Challenge mwaka wa 2002.

"Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, mpango huu umekuwa na jukumu kubwa na bado inaendelea na jukumu lake la kupambana na VVU na UKIMWI hapa nchini Tanzania”, alisema.

Alishukuru taasisi zote na watu binafsi ambao alisema wameshirikiana na na bado wanaendelea kushirikiana na GGM Limited katika mpango huo, ambapo aliwahimiza wadau wengine kuendelea kujitokeza ili kunga mikono kampeni ya Kilimanjaro Challenge kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kwa mujibu wa Bw. Jordinson, jumla ya watu 80 watashiriki katika kampeni hiyo iliyoko kwenye makundi mawili ya kupanda wapanda Mlima Kilimanjaro na wale watakaoendesha baiskeli kama sehemu ya GGM Kilimanjaro Challenge 2019, ambapo alibainisha kuwa 17 kati ya washiriki wanatoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dk. Leonard Maboko, aliishukuru GGM Limited na wadau wengine kwa michango yao katika kampeni dhidi ya VVU na UKIMWI nchini kwa kupitia GGM Kilimanjaro Challenge.

"Ushirikiano wenu katika mpango huu ni ushahidi wa wazi na mfano mzuri wa Ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP)", alisema na kuongeza, mpango huu pia ni mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi kwa TACAIDS na Serikali katika jitihada za kupambana na VVU na UKIMWI hapa nchini.

Aliongeza, "Ushirikiano huu ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI hapa nchini hususan ikitiliwa maanani ya kuwa takwimu zinaonyesha maambukizi mapya 200 kila siku".

Dkt. Maboko aliendelea kusema kwamba idadi hiyo ni sawa na maambukizi mapya 73,000 kwa mwaka, wengi wao wakiwa ni vijana, jambo ambalo alisema linaonyesha ya kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI hapa nchini bado ni muhimu sana.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Jabir Johnson

0 Comments:

Post a Comment