Mahakama ya Mwanzo Mjini Moshi imemhukumu mwanaume mmoja
mkoani Kilimanjaro kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kutelekeza familia yake.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Adnani Kingazi alisema mshtakiwa anayefahamika
kwa jina Dickson Ndimangwa Mbwambo (54) mkazi wa Moshi aliitoroka familia yake
miaka tisa iliyopita na kumuacha mkewe aliyefahamika kwa jina la Frida Evarist
Mushi (43) akitaabika na watoto.
Awali ilidaiwa mahakama hapo kuwa mshtakiwa
huyo alikuwa akiishi na mwanamke huyo maeneo ya Longuo A wilayani Moshi lakini
akatoweka kusikojulikana bila sababu yoyote ya msingi.
Dickson alikuja
kuonekana baada ya kutokea kwa msiba wa mmojawapo wa watoto wake ambaye
alifariki baada ya kugongwa na gari wakati akienda shuleni. Ilidaiwa mahakamani
hapo mtoto aliyefahamika kwa jina la Evarist ambaye ni miongoni mwa watoto sita
aliozaa na mwanamke huyo alipoteza maisha mwaka 2018. Baada ya msiba kutokea
mshtakiwa alijitokeza kuzika na ndipo polisi ilipomsubiri afanye mazishi hayo
kisha kumtia mikononi.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alipokamatwa
alipelekwa kwa Ustawi wa Jamii kutokana na kwamba muda wote aliotoweka hakuwahi
kutoa hata senti kwa ajili ya kuitunza familia yake.
Walipofika Ustawi wa jamii
walifikia makubaliano kwamba anapaswa kutoa 200,000 kila mwezi kwa ajili ya
matunzo ya familia lakini hadi anapandishwa kizimbani tarehe 7 Mei 2019 alikuwa
hajatoa kiasi chochote cha fedha. Mshtakiwa alijitetea baada ya adhabu hiyo
kutolewa ambapo alidai kuwa kilichomwondoa nyumbani ilikuwa ni ugomvi baina
yake na mkewe na kwamba anaiomba mahakama impunguzie adhabu kwani amezaa watoto
sita na mlalamikaji na bado wanapendana.
Aidha mshtakiwa alidai kuwa ana wazazi
hawajiwezi na wanamtegemea na kwamba kazi yake ni mpasua mbao. Ilielezwa
mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alifunga ndoa halali mwaka 1993 na kisha
kumtelekeza mwanamke huyo mwaka 2009.
0 Comments:
Post a Comment