Serikali mkoani Kilimanjaro, imeridhishwa na ujenzi wa barabara ya lami inayojengwa kutoka Sanya Juu hadi Elerai yenye urefu wa kilomita 32.2.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira, aliyasema
hayo wakati alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ambao
umekamilika na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 52, mradi ambao unajengwa
na mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa mradi huo Geo Engineering
Corporation, kutoka nchini China.
Dkt Mghwira alisema
ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa barabara ambayo ilikuwa
inajengwa na kampuni ya Geo Engineering Corporation ya nchini China, ambapo
ujenzi wake umekamilika kwa kiwango cha hali ya juu.
“Nimeridhishwa na kazi hii ya
ujenzi wa barabara ya lami kutoka Sanya Juu hadi Elerai , mradi huu umejengwa
kwa uhodari mkubwa, hivyo naipongeza kampuni ya Geo Engineering Corporation kwa
kukamilisha mradi huu wa barabara kwa kiwango cha juu,”alisema Dkt Mghwira.
Alisema kukamilika kwa
barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa walaya ya Siha na
mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla, kwani itarahisisha usafiri kwa wakulima wa
mazao ya biashara pamoja na wale wa sekta ya utalii.
Akitoa taarifa ya mradi
huo, Meneja wa Tanroads mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Nkolante Ntije, alisema
kwamba barabara hiyo yenye urefu wa kilimita 32.2 ambayo ujenzi wake ulianza
mwaka 2017, ambapo hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni
52.
“Kukamilika kwa barabara
hii kutaongeza kasi ya Utalii katika eneo la mkoa wa Kilimanjaro, kutoa fursa
za ajira pamoja na kuongeza uzalishaji katika mashamba,”alisema Mhandisi Ntije.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa halmashauri ya Wilaya ya Siha, Godson Ngomuo, alisema wilaya ya Siha ilikuwa
inakabiliwa na changamoto kubwa ya barabara kwa muda mrefu, hali ambayo
wafanyabiashara wengi walikuwa wakishindwa kuja kuwekeza katika wilaya hiyo.
Ngomuo alisema pamoja na
uwepo wa fursa za kiuchumi, kupitia kilimo, utalii na mashamba
makubwa, wilaya ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya uwepo wa
barabara zisizopitika kwa urahisi nyakati za mvua.
“Wapo watu wengi
walitamani kuwekeza kwenye viwanda, vituo vya mafuta, na kilimo, lakini
walishindwa na kwenda kuwekeza maeneo mengine, kutokana na ubovu wa barabara,
hivyo kukamilika kwa barabara hii itakuza sekta ya utalii kwa sababu
itawawezesha watalii na wafanyabiashara kufika kwa urahisi.
STORY BY: Kija Elias
0 Comments:
Post a Comment