Wanyaturu
ambao awali walijulikana kwa jina la Warimi ni watu wanaoishi karibu wilaya
zote za mkoa wa Singida yenye tarafa saba.
Kwa Mujibu wa Patrick Mdachi katika kitabu cha Wanyaturu wa Singida, Mila na Desturi zao, Wanyaturu ni moja ya makabila yanayojumlishwa katika kundi la Nilo-Hamites, lenye asili ya Wabantu walioishi Abysinia ambayo sasa inajulikana kama nchi ya Ethiopia.
Mdachi anasimulia kwamba Wanyaturu hao walikaa hapo kidogo na ndio eneo hilo ambalo watu hao waligawanyika tena, lengo likiwa ni kupeana nafasi ya kilimo, ufugaji na kuweka makazi ya kudumu. Mwilwana akielekea kaskazinimashariki eneo la Ilongero ambapo alistawisha makao yake hapo na hapo ukawa mwanzo wa Mwilwana huku Masanja akienda upande wa mashariki eneo la Kisaki na kujenga juu ya jiwe liitwalo Wahi, anasimulia Mdachi.
SOURCE: Asanterabbi Mtaki
Kwa Mujibu wa Patrick Mdachi katika kitabu cha Wanyaturu wa Singida, Mila na Desturi zao, Wanyaturu ni moja ya makabila yanayojumlishwa katika kundi la Nilo-Hamites, lenye asili ya Wabantu walioishi Abysinia ambayo sasa inajulikana kama nchi ya Ethiopia.
Watu hao
waliihama Abysinia (Ethiopia) kutokana na njaa kubwa kiasi ambacho hawakuweza
kustahimili kukaa tena hapo. Njaa ndiyo iliwalazimisha watu hao kufikia kula
nzige, katika harakati za kutafuta nzige hao ndio ukawa mwanzo wa safari yao ya
kuhama.
Mdachi
anasema katika kitabu chake hicho kilichochapishwa na Benedictine Publicationss
Nandanda - Peramiho mwaka 1991, kuwa Wanyaturu waliingia Tanzania kupitia
sehemu ya kaskazini kutokea Kenya na Uganda na kufanya maskani yao eneo la
Uzinza, Mwanza, baadaye walihamia eneo la Pasiansi na mwaka 1700 walikutwa na
Wasukuma ambao waliwafukuza na kuwafanya wakimbilie Ntunzu.
Baadhi ya
watu hao (yaani Mwilwana na Masanja) wakiwa na wake zao na watu wengine wa
kuwasaidia kazi hawakuweza kukaa Ntunzu, waliendelea na safari pamoja na
ng’ombe wao mpaka mkoani Singida, eneo la mashariki lijulikanalo kama Sepuka.
Mdachi anasimulia kwamba Wanyaturu hao walikaa hapo kidogo na ndio eneo hilo ambalo watu hao waligawanyika tena, lengo likiwa ni kupeana nafasi ya kilimo, ufugaji na kuweka makazi ya kudumu. Mwilwana akielekea kaskazinimashariki eneo la Ilongero ambapo alistawisha makao yake hapo na hapo ukawa mwanzo wa Mwilwana huku Masanja akienda upande wa mashariki eneo la Kisaki na kujenga juu ya jiwe liitwalo Wahi, anasimulia Mdachi.
Kwa mujibu
wa masimulizi hayo, Masanja alijaaliwa kuwa na watoto wanne ambao aliwapa
majina yao kulingana na kazi walizofanya au tabia. Watoto hao ni Sengasenga
aliyepewa jina hilo kutokana na kuwa baba yao alipoanza akiwa maskani alifyeka
mapori. Kufyeka pori kwa Kinyaturu ni ‘Usenga’.
Mtoto
mwingine aliyefuatia aliitwa Mpuma ambaye alipewa jina hilo kutokana na eneo
hilo kuwa na tumbili wengi. Mpuma kwa Kinyaturu ni tumbili. Mtoto wa tatu
alipewa jina la Hati kutokana na jiwe ambalo baba yao alitumia kujenga nyumba
na wa mwisho alijulikana kwa jina la Mkahiu kutokana na furaha ya wazazi wao.
Watoto hawa
walitawanyika ikiwa ni suluhu ya ugomvi wao na kila mmoja alianzisha ukoo wake
ambazo zilikuja kujulikana kama Senga, Anyahati, Puma na Ukahiu. Utafiti
unaonesha kuwa jina la kabila la Wanyaturu ni la hivi karibuni, awali kabila
hili lilijulikana kama Warimi. Jina hilo walipewa na watani wao Wanyamwezi
ambao walikuwa wakiwinda pamoja.
Siku moja
wakiwa katika kuwinda walimpiga mshale wa sumu mnyama wa porini, mnyama huyo
akakimbia na Wanyaturu wakiwa wanamkimbiza walikuwa wakisema ‘Mughuu turu,
turu’ wakimaanisha mguu huu hapa.
Wanyamwezi
wakaanza kuwaita Banyaturu jina likaendelea kukolea mpaka leo wanaitwa kwa jina
hilo na lile lao la asili, yaani Warimi, likapotea. Wanyaturu ni watu
wanaopakana na makabila ya Wanyiramba na Winyisanzu (magharibi), Wamang’ati
ambao pia huitwa Wabarbaig (kaskazini-mashariki), Wasandawe (mashariki), Wagogo
(kusini) na Wanyamwezi na Wasukuma upande wa Kusinimagharibi.
Muundo wa
utawala wa Wanyaturu Mfumo wa utawala wa kisiasa wa kabla na baada ya kuingia
wakoloni unahusu imani na utaratibu wa dini za kiasili. Tofauti na makabila
mengi hapa nchini, Wanyaturu hawakuwa na utawala wa kichifu. Katika kabila hili
kila ukoo ulikuwa na wazee (ambao kwa siku hizi tungewaita halmashauri) ambao
kazi yao kubwa ilikuwa ni kushauri pamoja na kupatanisha mashauri mbalimbali.
Koo
zinapokuwa nyingi zilipata kiongozi mmoja ambaye alichaguliwa kutokana na kazi
yake, pamoja na ujasiri wake wa kivita. Uongozi wa namna hiyo haukuwa wa
kurithi, bali ulipatikana kama Wanyaturu wanaovyoamini hutokana na bahati au
neema ya jua.
Jinsi
kiongozi anavyopatikana husemakana kuwa na nyota ya pekee sana hasa kutokana na
kuwa na waganga au waaguzi ambao humsaidia katika kazi zake. Waaguzi hao ambao
huchaguliwa kutoka kwenye ndoto na uteuzi wake hujulishwa na miungu au mungu
mwenyewe na kazi yao kubwa ilikuwa ni kutabiri mambo ya baadaye katika jamii.
Hivyo
kumfanya kiongozi kutekeleza mambo yake kwa mwongozo wa ndoto za waganga hao.
Waaguzi hao ndio waliokuwa viongozi wa kiroho. Kila kiongozi wa kivita alikuwa
na kiongozi wake wa kiroho ambaye pia alikuwa akimpa dawa za kinga. Mganga au
muuguzi mkuu alikuwa akiitwa Saigiro ambaye inasemekana alikuwa akitoka kabila
la Tatong.
Ujio wa
wakoloni Stanley alionekana katika eneo la Wanyaturu mwaka 1874 baada ya kuweka
bomba na chuma juu ya jiwe la Damankia, eneo la Dung’unyi, katika tarafa ya
Ikungi. Stanley alitanguliwa na Waarabu ambao inasemakana walikuwa wa kwanza
kukanyaga ardhi ya Wanyaturu. Hawa walikwenda kutafuta mtama.
Watu hao
wote waliwaona Wanyaturu kuwa ni watu wanaopenda vita. Mwaka 1900 ndio mwaka
ambao Wajerumani walianza kuingia taratibu na mbinu waliyoitumia kuingia
ilikuwa ni kwa kuwavutia viongozi wa vita ambao walikwenda kama wajumbe wa
biashara ya ng’ombe na mtama kwa nguo na shanga.
Hata hivyo,
ujio wa wakoloni, ulitabiriwa na mganga Sakilo ambaye aliishi katika mlima
Hanah na ambaye alikuwa aidha anatoka katika kabila la Tatog au Kimbugwe ambao
walitabiri ujio wa wekundu wasio na vidole miguuni, kwani walivaa viatu. Jina
lingine walilopewa wazungu na Wanyaturu ni ‘Anyeke’, yaani watu walio na miguu
kama tunda bivu kutokana na kuvaa viatu.
Baadhi ya
Wanyaturu hawaukufuatilia utabiri huo kutokana na kupendelea sana utabiri wa
Mahindi wa Isuna ambaye alitabiri kuwa Maksai mwekundu alionekana katika
maamkio yake na kukatokea vifo vingi, njaa, vitisho na fujo za kila namna.
Kwa Wanyaturu rangi nyekundu ni hatari na ng’ombe mwekundu huwa hatumiki kwenye sadaka ya aina yoyote.
Kwa Wanyaturu rangi nyekundu ni hatari na ng’ombe mwekundu huwa hatumiki kwenye sadaka ya aina yoyote.
SOURCE: Asanterabbi Mtaki
0 Comments:
Post a Comment