“Watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa. Naomba jamii ya watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha bora kama watanzania wengine, kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini," Dotto Olafsen.
Imeelezwa
umaskini ni sababu kubwa inayochangia kuvunjwa kwa haki za watoto hali ambayo
imewafanya wazazi na walezi kukosa muda maalum wa kuwasikiliza watoto katika changamoto
na kujikuta wakiingia katika ukatili.
Ukatili
huo umesababisha watoto hao kuathirika kimwili, kimaadili au kihisia ikiwemo
vipigo, kutukanwa matusi, kubaguliwa, kutojaliwa unyanyasaji wa kingono na
utumikishwaji.
Hayo
yalizungumzwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo Magret Reuben mwishoni
mwa wiki iliyopita katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika
shule ya sekondari ya Majengo iliyopo katika Manispaa ya Moshi kwa ushirikiano
kati ya ofisi ya Manispaa ya Moshi na azaki zisizokuwa za kiserikali zinazojihusisha
na masuala ya haki za watoto.
“Kama
mnavyojua, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoadhimisha siku ya
mtoto wa Afrika duniani ikiwa na lengo la kumkomboa mtoto kimaisha, matatizo ya
ukatili mkoani hapa hasa katika Manispaa ya Moshi yanaonekana kuongezeka kila
kukicha, hivyo nawaomba tuendelee kushirikiana kutokomeza hilo…” alisema Magret.
Afisa
huyo alizidi kufafanua kuwa, wazazi wengi wamejikita zaidi kwenye uzalishaji ili
waweze kuongeza uchumi wao na kusahau wajibu wa malezi na ulinzi wa watoto
kitendo kinachowafanya kukosa muda wa kuwalinda watoto wao ili wasikumbwe na
athari hizo.
“Matukio
mengi ya wazazi kutelekeza watoto wao kwa kutowapatia mahitaji muhimu kama
chakula, mavazi na malazi yaliripotiwa katika kipindi cha mwaka 2018/19,”
aliongeza Afisa huyo.
Kwa
upande wake, Wakili Mwandamizi wa Serikali ambaye pia ni Mwanasheria kutoka
ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali Tamari Mndeme, alifafanua kwa kutambua
umuhimu wa Mahakama za Watoto (Juvenile Court), serikali imetenga mahakama hizo
maalumu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mahakama
za watoto ni muhimu sana, ila changamoto kubwa tunayoipata ni wakati wa kutekeleza vifungu vya adhabu
kwa watoto kwani wazazi wenye watoto waliotendewa makosa kama ya ubakaji ama
ulawiti hawatuelewi; wengi hutamani kuona mtoto aliyetiwa hatiani akipewa
adhabu ya Kifungo cha miaka 30 kama watu wazima ilhali watoto wote wanalindwa
na wana haki zao kisheria hata pale inapobainika kuwa wametenda makosa ya
jina,” alisema Mndeme.
Akihutubia
mamia ya watoto, walimu, wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Asasi
mbalimbali zisizo za kiraia zinazojihusisha na masuala ya Haki za watoto kwa
niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba, Katibu Tawala wa Wilaya ya
Moshi (DAS) Angelina Marko alisema, “Elimu kwa watoto ndio imekuwa mada kuu kwa
nchi nyingi katika kumuinua mtoto wa Afrika, ambapo wadau hutumia siku hii
kutoa nasaha zinazolenga kuhamasisha serikali na mashirika binafsi na yale ya
kimataifa kusaidia watoto wa mitaani na wale yatima walioachwa na wazazi wao
kutokana na sababu mbalimbali kama vile maambukizi ya virusi vya HIV na
ukimwi.”
Marko
alitumia nafasi hiyo kuwataka watoto kusoma kwa bidii kuwaenzi watoto wenzao
waliouawa kikatili huko Soweto nchini Afrika Kusini wakipigania Haki ya kupata
Elimu, huku wakiitumia vyema fursa ya ‘Elimu Bure’ nchini Tanzania chini ya
Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Dees Bridal and Entertainment
inayojishulighulisha na masuala ya utoaji elimu kwa vijana, wanawake na watoto
kwa masuala mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, Dotto
Olafsen, alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu hasa kwa mtoto wa kike, taasisi
yake imekuwa ikitoa elimu kuhusu ukatili kwa watoto kupitia sanaa na burudani
mbalimbali ikiwemo muziki.
Olafsen
aliongeza kuwa, katika kampeni hiyo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo
kubaini baadhi ya watoto wameshakubuhu katika vitendo vya ngono hali ambayo
inawalazimu kutumia nguvu kubwa ya kisaikolojia kuwaondoa.
“Pia
katika kampeni yetu hiyo ya kuzuia mimba za utotoni tumegundua kuwa, baadhi ya
watoto tayari wameshaathiriwa na tatizo hilo na kuachishwa masomo kwani
serikali hairuhusu mwanafunzi aliyezaa kuendelea na masomo, hivyo wito wangu kwa
serikali ni kuandaa shule maalumu za kuwasaidia waathirika wa aina hiyo kwani
wengi wao hupata Mimba katika mazingira wasiyotarajia kutokana na kutopevuka
vyema akili zao,” alisema Olafsen.
“Watoto
wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa
matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa. Naomba jamii ya
watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha
bora kama watanzania wengine, kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini,"
alisema Olafsen.
Akizungumza
kwa niaba ya watoto wengine, mtoto Selina Mushi alisema, “Tunaomba kufikisha
kilio chetu kwa serikali na jamii nzima juu ya masuala mbalimbali yanayohusu
watoto katika nyanja zote ambazo ni malezi makuzi ,matunzo na usalama wa
watoto; tunanyanyasika, tunatoroka majumbani, tunateswa na vipigo pia tunaomba
kupatiwa walimu wazuri wa masomo ya sayansi
ili tuweze kuchangia uchumi wa
viwanda ipasavyo.”
Mnamo
mwezi Novemba 20, 1989, Uamuzi wa kihistoria ulifikiwa pale viongozi wa dunia
waliporidhia mkataba kuhusu haki za mtoto katika mkutano mkuu wa Umoja wa
Mataifa. Tangu kuridhia kwake miaka 27 iliyopita, mkataba huu umevunja rekodi
kwa kuwa mkataba wa haki za binadamu uliowahi kuridhiwa na mataifa mengi kuliko
yote katika historia.
Tanzania
ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa zilizoridhia mkataba huu katika
mwaka 1990. Kwa kufanya hivyo Tanzania ilitambua rasmi kwamba watoto wote
wanayo haki ya kuishi na kukua, kupatiwa ulinzi dhidi ya vurugu, matendo mabaya
na unyanyasaji, kuheshimiwa kwa mawazo yao na kuzingatiwa kwa maslahi yao
katika maamuzi yote yanayohusu ustawi wao.
Mwezi
wa Novemba 2009, miaka kumi na tisa baadaye, bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania lilipitisha sheria ya mtoto ya mwaka 2009, inayozingatia kikamilifu
mkataba wa haki za mtoto kulingana na muktadha wa Tanzania pamoja na kuweka
mazingira ya kufanikisha kupatikana kwa haki muhimu.
Siku ya mtoto wa Afrika
huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na
umuhimu wa mtoto duniani na maadhimisho haya hufanywa kila Juni 16 tangu
ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 kutokana na tukio baya la kuuawa
kikatili watoto huko Soweto nchini Afrika Kusini wakidai haki yao ya kupata
elimu bila ubaguzi wowote.
FEATURING
STORY BY: Kija Elias
EDITED
BY: Jabir Johnson