Dkt. John Pombe Magufuli (1959-2021) enzi za uhai wake. |
Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) na viongozi wa mila na desturi kutoka makabila mbalimbali nchini wametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Mama Janeth Magufuli na kwa watanzania wote kutokana na kifo cha Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa UMT Chifu Frank Marealle alisema umoja huo wa machifu nchini umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais mchapakazi wa awamu ya tano Dkt. Magufuli anayetarajiwa kuzikwa Machi 26 mwaka huu.
“Tunatoa pole kwa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, tunatoa pole kwa Mama Janeth Magufuli, watoto na jamii yote husika, tunatoa pole kwa Watanzania na kwa Waafrika wote popote walipo duniani,” alisema Chifu Marealle.
Chifu Marealle mwenye umri wa miaka 85 alisema UMT inamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya Hayati Rais Magufuli kwa uongozi, uzalendo, uthubutu, utendaji na maamuzi yake yalikuwa ni le oleo, hapakuwa na njoo kesho katika kipindi cha uongozi wake.
Aidha UMT ilisema itaendelea kufanya maombi kwa ajili ya Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia ya marehemu na watanzania wote kutokana na msiba mzito wa kwanza kulikumba taifa.
Aidha umoja huo ulitoa rai yake kwa viongozi wa serikali kuyaendeleza mema aliyokuwa amedhamiria Dkt. Magufuli na kwamba UMT itakuwa kipaumbele kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Rais mpya katika kuijenga Tanzania.
Kwa upande wake Chifu wa Waha, Ntware Isambe G. Lugaliburiho alisema kwamba wamejifunza uzalendo wa Dkt. Magufuli wa kujali vya nyumbani hususani pale alipoamua kuliita soko kuu la Morogoro jina la Chifu wa Waluguru Chifu Kingalu.
Aidha Chifu Gilbert Shangali wa Hai/Machame alisema wamekubaliana na hali iliyolikumba taifa kwa moyo wa huzuni lakini wamechukua ujasiri mkubwa wa maamuzi aliyokuwa akiyafanya Dkt. Magufuli enzi za utawala wake wa miaka sita.
UMT ulianzishwa muongo mmoja uliopita kwa madhumuni ya kurudisha utawala wa zamani wa machifu, ambao ulikuwa hatarini kupotea kutokana na jamii kupenda tamaduni nyingine na kusahau tamaduni za kwao.
0 Comments:
Post a Comment