Sunday, March 7, 2021

Wanawake timizeni wajibu wenu, saidia Tanzania

Jamii mbalimbali zimekuwa na hadithi simulizi katika maisha yao hususani zilizopo barani Afrikani. Hadithi simulizi ni utanzu wa kimasimulizi ambao umekuwapo katika jamii tangu kale.

Utanzu huo umekuwa ukitumika katika jamii, ili kuiburudisha hadhira pamoja na kufikisha ujumbe ikiwamo kuwataka wanajamii waishi kwa umoja na mshikamano, kufanya kazi kwa bidii ili kuyajenga maisha yao. Hadithi simulizi hugaiwa kutegemea mtazamo wa mtaalamu husika.

Kwa mfano, Ndungo na Wafula (1993), wanamnukuu Thomson (1946), akipendekeza kuwa, ngano zinaweza kutambulika kutegemea matukio muhimu yanayotokea katika ngano hizo.

Mvungi (2010) anaeleza kuwa, hadithi simulizi ni masimulizi marefu kidogo yanayolenga kuadilisha. Pia, Hadithi simulizi huonesha tukio la kawaida. Amesisitiza kuwa, matukio yake aghalabu huwa mazuri kwa baadhi ya wahusika na mabaya kwa wengine.

Mtafiti Hafsa Abdallah Ali mnamo mwaka 2015 alifanya utafiti wake katika mila na desturi za Wapemba ili kusawiri au kutathmini nafasi ya mwanamke katika jamii hiyo.

Wataalamu kadhaa wamemchora mwanamke katika hali tofauti, kuna waliomchora kuwa ni kiumbe duni, shujaa, mlezi wa familia na nafasi nyingine nyingi. Afrika au Tanzania, Sengo (2009) alimchunguza mwanamke ndani ya familia na akabaini kwamba vyeo tisa vya mwanamke vya heshima na thamani kubwa.

Wanaume wote wa Afrika wanawake wanawaita mama, mke, binti, dada, nyanya, mamkwe, mkwe, shangazi, na shemeji Kwa mtazamo huu mwanamke amebeba hadhi kubwa kupindukia.

Farsy (1956), katika kazi yake amemsawiri mwanamke kuwa, ni kama pambo na kuhusu hili anasema: “Zamani biharusi alipokuwa, akioneshwa alasiri, alipohudhurishwa mbele ya wanawake wenziwe huanza kupambwa tangu mchana, zama hizo walivishwa kiarabu…”

“Wakisukwa ususi wa behedani, kutiwa wanja usoni na machoni na nakshi nzuri nzuri…. kichwa kizima…..puani hutwa kipini……shingoni mkufu…….. mapambo yote haya hutiwa kwa ajili ya kumpendezesha mumewe.” (uk. 38).

Robert (1966),anaendelea kuwaelimisha wale wanaosema kuwa, mwanamke ni kiumbe aliyeleta laana na janga duniani. Katika Pambo La Lugha,anasema,

“Wanawake wana laana; jibu lako ufedhuli, Tena mimi naona lawama lastahili; Kuwa, hujui kunena u mchache wa akili; Wanawake bora sana ni hazina ya awali.”

Hali hii yote mwandishi anaonekana kumkweza mwanamke na kuachana na dhana ya kumdunisha.

Mohamed (1984) katika utangulizi wa kazi yake ya Kina Cha Maisha amegusia suali zima la nafasi ya mwanamke.

Mwandishi anasema: “….kwa kuendelea kumsanifu mwanamke kwa sifa kama mwenye shingo ya upanga mwendo wa maringo, ama kumfananisha na ndege au tunda kwa kusudi la kuusifia uzuri wake tu, kumepotosha na kugubika ukweli wa maisha wanavyoishi wanawake katika jamii nyingi za Kiswahili…”

Mwandishi anatuonesha kuwa, wakati umefika wa kuzifanya kazi za fasihi kujikita zaidi katika kumkomboa mwanamke, ama kumkweza. Kazi za fasihi zinazomdunisha mwanamke kwa kiasi fulani zimepitiwa na wakati.

Mtobwa (1984), alimchora mwanamke katika nafasi kadhaa kupitia kazi yake ya ‘Pesa Zako Zinanuka’.

Katika kazi hiyo, mwanamke amechorwa kuwa, ni mtu duni na tegemezi kwa mwanaume, hasa kwa vile anatumika kuwa, ni chombo cha starehe.

Kwa mfano, Mauwa alimstarehesha Born Kandili pamoja na Daktari. Mwandishi anasema: “Sasa nini? Kuwa uudhike? Unachotaka ni nini zaidi ya faraja ya kimwili kwa muda wa siku moja?

Aidha, Mbogo (1993) amemchora mwanamke kuwa ni jasiri na mwanamapinduzi.

Hali hii ameionesha kupitia Jalia ambaye aliyeongoza kikosi kumkamata Nungunungu aliyeogopwa na watu wote kupitia umaarufu wake.

Pia, alimpiga Nungunungu bila ya kuogopa vitisho vyake atoavyo kwa wengine tena bila ya wasi wasi.

Taswira hiyo, ilikuwa ni msingi imara katika kusukuma mbele umuhimu wa mwanamke.

Kwa mfano, katika hadithi ya Mkaidi Hafaidi, inasema: “Hapo zamani za kale alikuwepo bibi na wajukuu wake wawili wanawake, watu hao, waliishi msituni ulipofika wakati wa usiku bibi aliwaambia wajukuu wake wasitoke nje, wajukuu walimuuliza bibi tusitokenje kwa nini?

Hadithi hiyo inatuonesha kuwa, bibi ni mlezi wa watoto na kawaida katika ulezi mtoto huweza kuambiwamabaya namazuri ili kuyafuata au kuyaacha kama bibi alivyotumia nafasi yake katika hadithi hii.

Hivyo basi Wapemba kwa asilimia kubwa wameonyesha katika hadithi zao kuwa mwanamke ni chombo muhimu hivyo hawana haja ya kujidharau na kujiona hawafai. Wiki hii ni maalum kwa wanawake; Jambo la msingi mwanamke anapaswa ajitambue na ajiamini tayari kwa ajili ya kuisaidia Tanzania kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.


 

0 Comments:

Post a Comment