Wednesday, March 3, 2021

MAKTABA YA JAIZMELA: Zamalek ilipoidungua Yanga 1-0 jijini Cairo

Machi 3, 2012; Mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baina ya Zamalek na Yanga ya Tanzania ilichezwa katika jiji la Cairo. Mechi hiyo ilikuwa ya marudiano baada ya ile ya jijini Dar es Salaam.

Ilichezwa kwenye viwanja vya Jeshi jijini humo ambapo Zamalek waliizabua Yanga kwa bao 1-0 na kusonga katika raundi ya pili. Zamalek ilishuka dimbani ikiwa haina mashabiki kutokana na kukabiliwa na adhabu kutoka  Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Bao la mshambuliaji aliyewahi kutamba na vilabu mbalimbali barani Ulaya na kurejea nyumbani kwao Misri, Ahmed Hossam Hussein Abdelhamid ‘Mido’ lilitosha kuwaondoa Yanga katika mashindano ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Yanga walimaliza mchezo wakiwa pungufu baada ya kadi nyekundu ya Athuman Iddi ‘Chuji’ katika dakika ya 55, walionyesha kiwango kizuri katika kipindi cha pili jijini Cairo.

Mido alitupia bao katika dakika ya 31 ya mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali. Yanga walishindwa kutumia nafasi katika dakika ya 46 ya mchezo dakika chache baada ya kuanza kipindi cha pili huku Zamalek wakikosa mkwaju wa penalty katika dakika ya 74 ya mchezo.

Wachezaji wa Yanga walioanza katika mchezo huo walikuwa Shaban Kado, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, Stephan Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athuman Iddi, Juma Seif, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Keneth Asamoah na Nurdin Bakari.

Mechi hiyo ilichezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba alikuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.

Ikumbukwe katika mechi ya Februari 18, 2012 walitoka sare jijini Dar es Salaam  baada ya Hamisi Kiiza ‘Diego’ kutangulia kuifungia Yanga katika dakika ya 36 ya mchezo.

Bao la kusawazisha la Zamalek lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Hull City na Wigan Amr Zaki katika dakika ya 58 akitokea katika benchi kuchukua nafasi ya Ahmed Samir.

 

0 Comments:

Post a Comment