Wednesday, March 3, 2021

Bunny Wailer is no more (1947-2021)

 

Wasanii mbalimbali wanaendelea kutoa salamu za rambirambi zao kutokana na medani ya muziki wa reggae ulimwenguni kuondokewa na miongoni mwa mwanzilishi maarufu wa muziki huo Bunny Livingiston Wailer. Ziggy Marley, Gramps Morgan, Shaggy ni miongoni mwa waliotoa salamu hizo na kukaririwa na vyombo vya habari duniani. 

Bunny Wailer amefariki dunia ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kufikisha miaka 74. Bunny Wailer alifariki jana asubuhi katika hospitali moja mjini Kingston nchini Jamaica. 

Kiongozi wa Jamii ya Wasanii wa Reggae nchini Jamaica Olivia Grange alithibitisha kutokea kwa kifo cha nyota huyo. 

Mtoto wa Bunny Wailer Abijah Asadenaki Livingston aliweka bayana katika akaunti yake ya Facebook sababu za mauti kumkuta baba yake ni msongo wa mawazo ambao ulisababisha kupata stroke ambapo Julai 2020 alipata mshtuko wa pili. 

Aidha mwanaye huyo alisema kuondokewa na Jean Watt maarufu Sis Jean ndiko kulikosababisha apate msongo wa mawazo. Muziki wa reggae usingepata umaarufu wake wa sasa kama isingekuwa juhudi za mkongwe huyo. Bunny Wailer alikuwa na kipaji cha hali ya juu na mtu aliyekuwa akiimba kwa hisia kutoka rohoni mwake. 

Haikutosha alikuwa mtunzi na mpiga gitaa na vyombo vingine vya muziki kama haitoshi alikuwa mwanamichezo. Alikulia katika Parish ya Mt. Ann pale Nine Mile ambako alikutana na Bobert Nesta Marley maarufu Bob Marley na waliketi pamoja tangu walipokuwa watoto. Bunny Wailer ndiye aliyemfundisha Bob Marley kuimba. 

Peter Tosh alijiunga nao mnamo mwaka 1963 wakati ambao tayari alishaunda kundi la muziki wa reggae The Wailers mnamo mwaka 1962. Enzi za uhai wake Bunny Wailer alishinda tuzo tatu za Grammy. Alizaliwa Aprili 10, 1947.

0 Comments:

Post a Comment