Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limevitaka vyama vya michezo nchini kuwasilisha mipango mikakati ya mwaka 2020/21 na visipofanya hivyo hatua kali zitachukuliwa.
Akizungumza na vyombo vya habari Katibu Mtandaji wa BMT George Msonde amesema vyama vya michezo vyote nchini vinatakiwa kuwasilisha taarifa zao na mipango mikakati kati ya Machi 4 na 12 na vitakavyokiuka agizo hilo vitakuwa kinyume na sheria za nchi katika medani ya michezo.
"BMT inaviagiza vyama vya michezo vya kitaifa ambavyo havijawasilisha mipango mikakati yao kwa mwaka 2020/21 kuwasilisha mipango hiyo ndani ya siku saba za kazi kuanzia Machi 4 hadi 12 mwaka 2021; ambapo kutofanya hivyo ni kukiuka agizo la serikali na hatua zitachukuliwa dhidi yao," amesema Msonde.
Msonde amesema hadi Februari 28 mwaka huu ni vya 38 ambavyo tayari vimeshafikisha mipango mikakati kwa baraza hilo na kuongeza kwamba taarifa zao zinaendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu.
Aidha Msonde amesisitiza kuwa madhumuni makubwa ya kupeleka taarifa hizo ni kuziwezesha timu za taifa katika michezo mbalimbali kufanya vizuri kitaifa na kimataifa hivyo taarifa zinapochelewa zinasababisha kufanya vibaya katika mashindano.
0 Comments:
Post a Comment