Monday, March 8, 2021

MAKTABA YA JAIZMELA: Florentino Perez ni nani?

 


Machi 8, 1947 alizaliwa Rais wa sasa wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez. Huyu ni mfanyabiashara, mhandisi na mwanasiasa wa zamani nchini Hispania. 


Haitoshi Perez ni mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Muunganiko wa Makampuni ya ACS yanayojihusisha na uhandisi. 


Alizaliwa Hortaleza, miongoni mwa wilaya 21 zinazounda jiji la Madrid. Perez alisoma katika chuo kikuu cha Polytechnic cha jijini Madrid. 


Alijiunga na harakati za kisiasa mnamo mwaka 1979 pale alipojiunga na chama cha Union of the Democratic Centre na kukitumikia kama walivyokuwa wakifanya wenzake katika baraza la Jiji la Madrid.


Mnamo mwaka 1986 Perez alipambana katika uchaguzi mkuu akigombea akiwa na Chama cha Reformista Democrático akihudumu katika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.


Mnamo mwaka 1993 alitajwa kuwa makamu wa rais wa OCP Construcciones na ilipofika mwaka 1997 alikuwa rais wa kampuni jipya la Actividades de Construcción y Servicios, S.A. (ACS) baada ya kuungana kwa OCP na Gines y Navarro.


Mwaka 2018 aliongoza muungano wa makampuni wa ACS  lilikiwa ni kampuni kubwa la ujenzi nchini Hispania na wakati huo alikuwa na utaji wa kiasi cha dola za kimarekani bil. 2.3.
Perez alijitosa katika kinyang'anyiro cha urais wa klabu ya Real Madrid na kutwaa kama rais mnamo mwaka 2000 baada ya kushindwa mara ya kwanza. Alimshinda Rais wa klabu hiyo wakati huo Lorenzo Sanz. 


Sanz alikuwa na matumaini makubwa ya kushinda nafasi hiyo kutokana na Real Madrid kushinda mataji ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mnamo mwaka 1998 na 2000. Kilichomwangusha ni matatizo ya kifedha na usimamizi mbovu wa bodi ulikuwa kigingi kilichompa mwanya Perez. 


Kwa upande wake Perez aliwaahidi wanachama wa Merengues kuwa atamleta nyota wa Ureno Luis Figo klabuni hapo ambaye kwa wakati huo alikuwa akihudumu na mahasimu wao Barcelona. Alichaguliwa tena mwaka 2004 kwa asilimia 94.2 za kura. 


Ujio wa Figo klabuni hapo ilikuwa alama muhimu katika utawala wa Perez kalabuni hapo na ulikuwa mwanzo wa nyota bora kutua kila msimu kwa miamba hiyo. 


Hapo ndipo ujio wa wachezaji ghali na bora ulifahamika kwa jina la Galácticos; badala ya Zidanes y Pavones kwa kifupi Canteranos. 


Mnamo mwaka 2001 Zinedine Zidane alisajiliwa akitokea Juventus kwa kuweka rekodi ya usajili ghali duniani wakati huo kwa Euro milioni 77.5 Mnamo mwaka 2002 Ronaldo de Lima alitua katika viunga vya Madrid akifuatiwa na David Beckham mnamo mwaka 2003; Michael Owen alitua mwaka 2004 na kwa kipindi kifupi alitua Robinho mnamo mwaka 2005. 


Sera za Perez zilionekana kufanya kazi  na kwa mafanikio makubwa akiweka uzani mzuri katika kila idara katika dimba ikiwa na maana ya ushambuliaji na safu ya ulinzi.

 
Katika miaka ya mwanzoni Real Madrid ilishinda mataji mawili ya La liga na kuweka rekodi ya kutwaa taji la tisa la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. 


Maendeleo makubwa aliyafanya Perez kwa kulipa madeni makubwa ambayo Los Blancos ilikuwa nayo, licha ya wakati fulani kutofautiana na mkurugenzi Ramón Calderón. 


Baada ya miaka kadhaa kupita Fernando Hierro aliyekuwa mchezaji klabuni hapo aliwahi kusema kuwa uwepo wa nyota Claude Makelele ulikuwa wa muhimu licha ya kutopewa umuhimu na kukubalika, " Kumpoteza Makelele ndio ulikuwa mwanzo wa kupotea kizazi cha Los Galácticos....Hilo unaweza ukaliona kuwa ulikuwa ndio mwanzo wa zama mpya nzuri za Chelsea."


Kutoka msimu wa 2003/04 na kuendelea kukosekana kwa kocha Vicente del Bosque na Makelele kuliifanya Real Madrid ishindwe kutwaa mataji. 


Sera za Perez zilikosolewa mara kwa mara kwamba zimejikita katika masoko badala ya mpira kwani Perez alipanua wigo wa Real Madrid hususani barani Asia. 


Mnamo Februari 27, 2006 alitangaza kujiuzulu, akiishukuru klabu hiyo na timu kuwa inahitaji kupata mwelekeo mpya.


Hata hivyo mnamo Mei 14, 2009; Perez alitangaza kuwania tena urais wa klabu hiyo kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa katika ukumbi wa Hoteli ya Ritz jijini Madrid.
Juni 1, 2009 alitangazwa kuwa Rais wa klabu hiyo akiwa ni mgombea pekee alifanikiwa kutoa kiasi cha euro mil. 57.4


Kushika nafasi hiyo kwa msimu wa pili hakukubadili sera na falsafa yake ya kuwaleta nyota bora ambapo siku saba tu baada ya kuwa rais wa klabu hiyo alimsajili Mbrazil Ricardo Kaka akitokea AC Milan kwa ada ya pauni mil. 60.


Mnamo Juni 11, 2009 alimleta Cristiano Ronaldo kwa ada ya pauni milioni 80 akitokea Manchester United akiweka rekodi nyingine ya usajili duniani. Juni 25, 2009 alimleta mlinzi wa kati Raul Albiol akitokea Valencia kwa euro milioni 15. 


Hakuishia hapo Julai 1, 2009 alimleta mshambuliaji Karim Benzema akitokea Olmpique Lyon kwa ada ya pauni milioni 30 ambayo ilikuja kupanda na kufikia pauni milioni 35 kutokana na kiwango chake namna kilivyokuwa kikipanda. 


Mnamo Agosti 5, 2009 Real Madrid ilithibitisha ujio wa Xabi Alonso akitokea Liverpool kwa ada ya pauni milioni 30 akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kutua Los Blancos akitokea Liverpool baada ya mlinzi wa pembeni Arbeloa mnamo Julai kwa ada ya pauni milioni tano.
 

Mei 31, 2010 Perez alimtangaza kocha Jose Mourinho kuwa kocha mpya ya Real Madrid kwa ada ya pauni milioni 6.8 


Ujio wa Mourinho ulikuja na sura mpya misimu mitatu baadaye nyota Mesut Ozil, Angel di Maria ambao walikuwa na mvuto baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini


Mnamo Juni 2, 2013 Perez alimwondoa Mourinho na kumleta Carlo Ancelotti ambapo Ozil na Gonzalo Higuain waliuzwa kwenda Arsenal na Napoli mtawalia. Kuondoka kwa nyota hao kuliwapa nafasi Benzema na Luka Mdric kuwamo katika kikosi cha kwanza. 


Perez aliendelea kununua wachezaji bora kwa bei ghali ambapo Gareth Bale alitua Santiago Bernabeu akitokea Tottenham Hotspur kwa ada ya pauni mil. 86akivunja rekodi ya dunia kwa mara nyingine. 


Isco na Asier Illarramendi watoto wa Hispania walipata nafasi katika kikosi cha Real Madrid; misimu iliyofuata ilidhihirika sera zake ambapo Real Madrid ilitwaa mataji ikiwamo Kombe la Mfalme na taji la 10 la Ligi ya Mabingwa.


Majira ya joto mwaka 2014 baada ya Kombe la Dunia nchini Brazil, Perez aliwaleta nyota wengine James Rodriguez, Toni Kroos Keylor Navas na Javier Hernandez 'Chicharito' akitua kwa mkopo kutoka Manchester United huku Di Maria akiondoka na kutua Manchester United na Alonso akijiunga na Bayern Munich.


Huyo ndiye Florentino Perez.

Ujio wa Figo klabuni hapo ilikuwa alama muhimu katika utawala wa Perez kalabuni hapo na ulikuwa mwanzo wa nyota bora kutua kila msimu kwa miamba hiyo. 




0 Comments:

Post a Comment