Friday, April 30, 2021

Anusurika kichapo kwa kujifanya mjamzito akiiba sokoni Memorial, Moshi

 

KUNA methali moja ya Kiswahili isemayo, “Hakuna anayemshinda mwanaume kama mwanamke,” hii imedhihirika katika soko la Memorial mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro hivi karibuni kwa mwanamke ambaye alifahamika kwa jina moja la Elizabeth kunusurika kichapo kutoka kwa wafanyabiashara wanaume waliokuwa na hasira kali kumkamata akiiba mzigo katika soko hilo.
 
SASA ENDELEA.......
 
Mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 42, mwenye kimo cha futi tano na kidogo hivi alinusurika kichapo sokoni hapo asubuhi ya saa mbili Aprili 28 baada ya kujifanya mjamzito na kwamba ana ujauzito wa miezi minane mbele ya wanaume waliomkamata akiiba mzito huo.
 
Pia Elizabeth alijifanya kuwa ujauzito huo unakaribia kwenye hatua zake za mwisho aliutengeneza mdomo wake na kuwa mkavu kama kina mama wajawazito wanavyokuwa na aliposachiwa alikutwa na tochi, kisu kidogo na karata za kuchezea.
 
Utata ulizidi kuhusu ujauzito wa mwanamke huyo baada ya mwanamke mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, mjasiriamali na aliyesomea masuala ya utabibu kwenda na kumchunguza kwa dakika chache na kubaini kuwa hana ujauzito wowote.
 
Tukio hilo lilianza hivi, baada ya mwanamke huyo anayesemekana ni mkazi wa Kibosho alipoingia sokoni hapo mapema na kuongozana na vijana wanaobeba mizigo kwa matoroli alipofika katika mojawapo ya meza ya mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Dominika Temba (24) maarufu Mama Samir alimtaka kijana aubebe mzigo huo na kwenda nao nje ya lango.
 
Wakati hayo yakifanya mlinzi wa soko aliyejitambulisha na mwandishi wa habari hii kwa jina la Mudy alisema alimshtukia mwanamke huyo na kumuuliza kuhusu mzigo huo.
 
“Nilimshtukia, mimi ni mlinzi wa hapa ninawafahamu wenye meza na mizigo yao; sasa nilipomuona nikamkimbilia kumuuliza kwani vijana hawa wa Kimasai (wabeba mizigo) wengine sio wazoefu na soko hili; akanijibu hapana hapo ndipo ngoma ilipoanza,” alisema mlinzi Mudy.
 
Mlinzi huyo alithibitisha kumkuta mwanamke huyo mwizi na karata, kisu kidogo na tochi na alipoanza kumsachi ndipo mwanamke huyo alipojifanya kuzidiwa na ujauzito ambapo Mudy alijivika ujasiri na kutaka kuthibitisha kama kweli ni mjamzito lakini akaona mambo siyo kama alivyotegemea.
 
“Niliamua kumsachi kwa nafasi yangu kama mlinzi na kumhoji kama kweli ni mjamzito na sokoni amekuja kutafuta nini, akanipa mkanda wote kuwa ni shida tu zimemfanya afikie hapo na sio kwamba ni mjamzito, ukubwa wa tumbo lake akaniambia kuwa alirogwa na ndugu zake, hivyo huonekana kama mjamzito,” alisema Mudy.
 
Hata hivyo mwanamke huyo mwizi alipoona watu wanazidi kuwa wengi alijifanya kuzidiwa kiasi cha kushindwa kunyanyuka kutokana na ujauzito wake ambao uliwahadaa wanaume waliokuja na jazba ili wamtandike vibao kwa kusema ukweli.
 
Wanawake wajasiriamali sokoni hapo walipoona wanaume hao wanataka kutoa kichapo hicho walimzingira mwanamke huyo na walishauriana kumpeleka hospitalini kwa kuchangishana fedha ambapo kilipatikana kiasi cha shilingi 10,000/= kwa ajili ya usafiri.
 
Wanaume walikataa wazo la kuchangia kwani mwanamke huyo mkazi wa Kibosho ni mwizi kama wizi wengine na angetakiwa kufikishwa polisi kwanza kwa ajili ya kujieleza, wanawake wengine walitaka jambo hilo limalizike sokoni hapo kwa maana mzigo umekatwa salama ili kukomboa wakati katika utafutaji wa hela.
 
Ilichukua saa takribani mbili na nusu kumuona Afisa wa Jeshi la Polisi mwanamke ambaye hakutaka jina lake litajwe kuonekana katika tukio hilo baada ya juhudi zilizofanyika na viongozi wa soko la Memorial ili kunusuru maisha ya mwanamke huyo mwizi.
 
Makamu Mwenyekiti wa soko la Memorial Jeremia Adram aliongeza kuwa wezi katika soko hilo wamekuwa wakitumia vijana wa Kimasai na kuwarubuni kwa kiasi kidogo cha pesa kisha kuingia nao ndani na kuubeba mzigo ambao tayari walishaufanyia utafiti na kutokomea nao nje.
 
“Kama uongozi wa soko tunaendelea kuimarisha suala la ulinzi huku tukiendelea kubaini mbinu chafu za wezi katika soko letu, Wamasai wasio na nia njema wamekuwa wakirubuniwa na wezi hao kwa pesa kidogo katika zoezi hilo, huyu mwanamke ni somo kwa wengine wenye tabia hiyo,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Soko.
 
Kwa upande wake Mama Samir alisema, “Ningependa suala hili limalizike hapa hapa, lakini kwasababu limefika mikononi mwa vyombo vya sheria basi, lakini nimetoka kukata beli jana, beli ambalo nimelinunua kwa laki nne na nusu hata laki sijauza mambo haya yanajitokea, imeniuma sana.”
 

0 Comments:

Post a Comment