Monday, May 3, 2021

Vivutio lukuki Msitu Asilia Rau kuibua fursa za maendeleo Moshi

 

Mvule wa ajabu unaopatikana katika Msitu Asilia wa Rau ni miongoni mwa vivutio ambao kwa sasa (2021) una zaidi ya miaka 200. Umekuwa ukitumiwa kwa ibada na matambiko ambapo vitu mbalimbali zikiwamo fedha hurushwa hapo na magome ya mti huo hubanduliwa kwa matumizi ya tiba.

UWEPO wa mvule wa maajabu, panya wenye masikio makubwa kama ya tembo, chemichemi ya maji ya maziwa, vinyonga weupe, katika hifadhi ya asili ya Rau iliyopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ni vivutio tosha kwa watalii ndani na nje ya nchi kuzuru na kuibua fursa za maendeleo kwa wakazi wanaozunguka hifadhi hiyo.

Ikumbukwe kuwa, maliasili na utalii ni miongoni mwa sekta za uchumi nchini ambazo zinatoa mchango mkubwa katika ukusanyaji wa mapato na kuendeleza maisha ya Watanzania wengi ikiwepo fursa za kutoa ajira.

Mathalan, Sekta Ndogo ya Utalii kupitia vivutio mbalimbali inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha zote za kigeni na kuajiri zaidi ya watu milioni 5.5 kwa mwaka. Kutokana na umuhimu huo.

Aidha uwepo wa msitu asilia wa Rau ni miongoni mwa kile kinachofahamika kama utalii wa ndani ambao, ni muhimu kwa sababu tatu kuu. Kwanza, unatoa fursa ya wananchi kupumzika kwa namna nzuri zaidi. Pili, unasaidia kufanya wananchi wathamini zaidi vivutio tulivyonavyo na hivyo kuongeza mwamko wa kuhifadhi na kuvitunza. Tatu, ni chanzo cha mapato kwa taasisi zetu za uhifadhi, jambo ambalo ni muhimu sana.

 

KWANINI UBORESHAJI UNATAKIWA MSITU WA RAU?

Akizungumza na waandishi wa habari waliozuru msitu asilia wa Rau, Mhifadhi Mkuu wa Msitu Asilia wa Rau, Godson Ollomi alisema Msitu asilia wa Rau una ikolojia nzuri inayoweza kuwavuta watalii, "Kutoka mwaka 2014 hadi 2020 watalii wamekuwa wakiongezeka kutoka 11 waliofika kwa mara ya kwanza tangu kuanza kutunzwa kwa takwimu hadi  kufikia 475. Ambapo jumla ya watalii 1593 wamefika kujionea vivutio vya msitu huu kwa miaka hii yote sita."

Aidha alisema kumekuwa na changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ili kuongeza kiwango cha watalii na mapato kupitia vivutio hivyo  vya msitu huo asilia. 

"Msitu huo pekee wa asilia uliopo mjini miongoni mwa misitu ya asili umekuwa na vivutio vingi visivyotangazwa vizuri na kufahamika licha ya ukaribu wake na wakazi wa Moshi; ninachokifahamu ni changamoto ya miundombinu ya barabara, pamoja na zile njia za kupita watalii bado hatujaziimarisha vizuri kulingana na maeneo ambako kuna vivutio hivyo," alisema Ollomi

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mnamo mwaka 2014/15 kwa mara ya kwanza watalii 11 walizuru na Manispaa ya Moshi ilijikusanyia mapato ya shilingi 204,000 za Tanzania. Mwaka uliofuata  wa 2015/16 kulikuwa na ongezeko la shilingi 1,464,000 ambapo kiasi cha shilingi 1,668,000 za Tanzania kilikusanywa kutokana na ujio wa watalii 84 waliotembelea vivutio hivyo.

 Mnamo mwaka 2016/17 kulikuwa na ongezeko la shilingi 1,659,500 ambapo kiasi cha shilingi 3,327,500 kilikusanywa kutokana na watalii 213 walitembelea msitu huo asilia ikiwa ni ongezeko la watalii 129 ikilinganishwa na mwaka 2015/16.

Kiasi cha shilingi 9,000,000 za Tanzania kilikusanywa mnamo mwaka 2017/18 kutoka kwa watalii 450 (ongezeko la watalii 237 kwa mwaka 2016/17) ikiwa ni ongezeko la shilingi 5,672,500/=.

Aidha mnamo mwaka 2018/19 mapato yaliyokusanywa ni kiasi cha shilingi 9,497,200/= ikiwa ni ongezeko la shilingi 497,200/= ikilinganishwa na mwaka mmoja nyuma kutoka kwa watalii 475 ongezeko la watalii 75 kutoka 450 mwaka 20117/18.

Hata hivyo kutokana na maradhi ya covid-19 mnamo mwaka 2019/2020 watalii 360 walitembelea msitu huo asilia ikiwa ni pungufu ya watalii 115 ikilinganishwa na watalii 475 kabla ya kulipuka kwa janga hilo la dunia; ambapo kiasi cha shilingi 7,840,000/= kilikusanywa ikiwa ni pungufu ya shilingi 1,657,200 kutoka milioni 9,497,200 mwaka mmoja kabla.

Ollomi alisema uboreshaji unatakiwa katika msitu asilia wa Rau ili kukuza utalii na ongezeko la mapato kwa manufaa ya Watanzania.

"Mbinu nyingi zinatakiwa ikiwamo kutangaza vivutio vilivyopo katika msitu asilia wa Rau kupitia mitandao mbalimbali, kuboresha ulinzi na usalama kwasababu msitu huu unaweza kutalii hata usiku kutokana na viumbe wengine kupatikana nyakati za usiku pekee na jambo jingine ni kuendelea kuvumbua aina nyingine za vivutio kama mimea na wanyama waliopo msituni hapa," alisema Ollomi.

Mpaka sasa makampuni ya kuongoza watalii yamekuwa yakifanya kazi na TFS ikiwamo Leopard Tours, Zara Tours, Kili Bike Adventure, Kili Safari, Nyange Adventure, Milestone Safari, Kibosho Tours and Safari, Gaia Africa Travel, Rau Eco and Cultural Tourism na Key Tours ambayo ukilinganisha na sifa ya mkoa wa Kilimanjaro na viunga vyake katika masuala ya Utalii ni kwamba bado fursa hazijawafikia wengi kwa msitu huo asilia wa Rau.

" Wakazi wa Manispaa ya Moshi wanakaribishwa kufika na kuutembelea Msitu wa Hifadhi wa Rau, Waongoza Watalii kuwatembeza watalii wanaofika katika mji wa Moshi kabla ya kuanza kuupanda mlima Kilimanjaro ni vema kwamba wakawatembeza kwenye hifadhi ya msitu wa Rau, kwani unavivutio vingi ambavyo kwengine havipatikani," alisisitiza Ollomi.

Mhifadhi huyo aliongeza kuwa zipo fursa nyingi ambazo zimetolewa na kwamba kuna sheria ambayo kwa sasa inaruhusu wawekezaji kuwekeza katika misitu ya hifadhi, "Wawekezaji wanakaribishwa kuja kuwekeza ikiwemo kujenga Camps site, na hotel za kitalii katika hifadhi ya asili ya Rau watembelee katika ofisi za TFS ili waweze kuelekezwa."

Mhifadhi Mkuu wa Msitu Asilia wa Rau, Godson Ollomi (kulia) akitoa maelezo kwa kina kuhusu Mvule wa ajabu ambao umekuwa ukitumika kwa ibada na matambiko. Ollomi alisema kubanduliwa kwa magome ya mti huo kunaufanya uwe hatari kutoweka hivyo wana kila sababu ya kuendelea kuutunza mti huo ambao kwa kitaalamu hujulikana 'Milicia excelsa'


 


0 Comments:

Post a Comment