Wanakijiji wa Yamu Makaa wakifunga barabara kuzuia malori ya mchang kuingia kijiji kwao, mpaka taarifa ya Mapato na Matumizi ya Kijiji itakaposomwa.
Wanakijiji wa Yamu Makaa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wamefanya maandamano makubwa kijijini hapo yaliyosababisha mwenyekiti wa kijiji hicho kukimbia kwa kile kinachodaiwa ufujaji wa rasilimali za kijiji yakiwamo machimbo ya moramu.
Maandamano hayo yasiyo rasmi yalipelekea Jeshi la Polisi kufika kijijini hapo, baada ya wanakijiji hao kuzuia malori ya mchanga yaliyokuwa yakipita kwenda kuchukua moramu katika kitongoji cha Kiuo ‘A’ yalipo machimbo hayo.
Aidha wanakijiji hao walisema kumekuwa na ubadhirifu wa fedha kutokana machimbo hayo, utoaji wa risiti za kieletroniki haufanyi huku risiti zinazotolewa kwa karatasi ukipewa msisitizo jambo ambalo linaongeza mianya ya rushwa.
“Ofisi ya Kijiji tumekuwa tukiisisitiza kutusomea mapato na matumizi, hususani kwenye haya machimbo kwani wanaochimba hatuoni risiti wakipewa na tunahisi kuna upigaji mkubwa wa fedha ambayo mwenyekiti na ofisi yake wanahusika,” alisema mwanakijiji (jina tunalihifadhi).
“Kuna siku tumeshuhudia hapa ndani ya siku mbili tripu 80 za mchanga zimesombwa hapa, lakini tulipomuuliza mwenyekiti akatuambia ni tripu 10 tu, jambo ambalo si kweli, tumechoka na ndio tukaona bila kutumia nguvu tutaibiwa kila siku,” alisema Joachim Kessy.
Sakata la Mwenyekiti wa Kijiji hicho Omary Mdee kukimbia lilianza baada ya kutakiwa na Jeshi la Polisi lililofika mahali hapo kutuliza ghasia hizo kuitisha mkutano wa kijiji na kuwasomea mapato na matumizi wanakijiji hao.
Siku ya pili Mdee alikiri kuwa angeitisha mkutano huo majira ya saa tatu asubuhi lakini cha kustaajabisha ni pale alipotoa taarifa kuwa mkutano hautaweza kufanyika kutokana na msiba uliotokea kijijini hapo.
Ndipo wanakijiji walipoamsha hasira zao na kufunga safari kwenda kwa Mwenyekiti huyo ambapo walimtaka aitishe mkutano huo na baada ya kumaliza watakwenda wote kwenye huo msiba ambao maziko yalitarajiwa kufanyika saa nane za mchana.
Kwa kuona hivyo mwenyekiti hakuonekana mbele yao kwa kuwataka wasubiri kidogo kisha atatoa jibu rasmi ambapo taarifa zilizotufikia baadaye zikabainisha kuwa mwenyekiti huyo amesafiri kwenda Tanga kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana na alipotafutwa kwa simu hakupatikana.
Awali kabla ya maandamano hayo kufanyika, wananchi hao walilazimika kuyazuia malori hayo kwa saa mbili, baada ya kuchoshwa na uongozi wa serikali ya kijiji hicho baada ya kushindwa kuwapa taarifa za makubaliano ya mikataba walioingia na mkandarasi wa Kampuni ya Kyara Construction Co.Ltd, ya kuchimba madini hayo na ubovu wa barabara yenye urefu wa kilometa moja na nusu.
Mkazi wa Kijiji hicho Veronica Mvungi, alikaririwa akisema kina mama wajawazito na wagonjwa, wamekuwa wakiteseka kutokana na ubovu wa barabara hiyo hususan katika kipindi cha mvua, licha ya kwamba madini hayo yamekuwa yakichimbwa katika eneo lao huku magari yenye uzito mkubwa yakipita na kuchukua moramu hiyo bila kuwatengenezea barabara.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiuo 'A' Ramadhan Mgonja, alisemachangarawe hiyo inachimbwa amesema walikubaliana na mkandarasi huyo kuweka moramu roli sita kwenye barabara hiyo jambo ambalo amelitekeleza lakini anashangazwa kuona na wananchi hao kuyazuia magari yake.
Kwa upande wake mkandarasi huyo Prosper Kyara, alisema ameshangazwa na wananchi kuzuia magari yake kwani taratibu zote alipewa na ofisi ya Kijiji na kwamba makubaliano yalikuwa kila tripu moja ya Lori alikuwa akiwalipa serikali ya Kijiji Tsh 25,000 hadi sasa ameshachukua tripu 25 na pesa hizo amekwishailipa serikali ya Kijiji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Yamu Makaa Omary Mdee (katikati) Mojawapo ya mkazi wa kijiji ch Yamu Makaa akihoji kuhusu mapato na matumizi ya kijiji. Baadhi ya wanakijiji wa Yamu Makaa walizuia uchimbaji wa moramu usiendelee mpaka pale Mwenyekiti wa Kijiji atakapoweka bayana mapato na matumizi.
0 Comments:
Post a Comment