Monday, May 3, 2021

Ubahili sio sifa njema

Ubahili, au kujizuia kutoa vitu kwa watu wengine na kujikusanyia mali na utajiri kwa ajili yake mwenyewe mtu, ni moja ya alama ya mapenzi ya dunia.

Ubahili ni uovu wenye kuchukiza kiasi kwamba kama mtu akiathiriwa nao, huiweka familia yake katika umasikini, huchukia wageni kuja nyumbani kwake, hujizuia kuwatembelea watu wengine ili mtu yeyote asimtembelee, hujiepusha kushirikiana na watu wakarimu na hujisikia vibaya kuhusu ukarimu wa watu wengine. Mtukufu Mtume (saw) amesema: “Hakuna bahili atakayeingia Peponi.”

Sa’id Ibn Harun, mwandishi kutoka Baghdad na wa zama moja na Ma’mun, Khalifa wa Bani Abbas, alikuwa akivuma vibaya kwa ubahili wake.

Abu Ali Dibil Khazaai, mshairi mashuhuri (alikufa 245 A.H.) anasema: “Nikiwa nimefuatana na baadhi ya washairi, nilikwenda nyumbani kwa Sa’id na tulikuwa pamoja naye kuanzia asubuhi mpaka mchana. Wakati adhuhuri ilipokuwa inakaribia, alianza kusikia njaa na matokeo yake akawa anahangaika.

Sa’id alikuwa na mtumwa mzee, ambaye alimuambia, “kama kuna kitu cha kula, hebu tuletee.” Yule mtumwa aliondoka na kurudi muda mfupi akiwa amechukuwa kitambaa kichafu cha chakula.

Alikitandika mbele yetu na akaweka juu yake kipande kimoja tu cha mkate mkavu. Kisha akaleta bakuli lililovunjika midomo yake lililojazwa maji ya moto, na ambalo lina jogoo mzee asiyepikwa na asiye na kichwa!

Wakati yule mtumwa anaweka lile bakuli kwenye kitambaa cha chakula, acho ya Sa’id yakaangukia juu yake na akaona yule jogoo asiye na kich- wa, alifikiria kwa muda kidogo na kisha akasema, “Ewe Mtumwa! Kikowapi kichwa cha jogoo huyu?” Yule mtumwa akajibu: “Nimekitupa.”

Alivyosikia hivi, Sa’id alipiga kelele: “Simruhusu yeyote mwenye kutupa miguu ya jogoo, achilia mbali kichwa chake. Kitendo hiki (chako) huwashiria ubaya (kwangu) kwani kichwa cha jogoo kina faida nyingi: Kwanza, kutokana na kichwa chake hutoka sauti ambayo huwajulisha waja wa Mwenyezi Mungu kuhusu muda wa Swala; kwa njia yake hii, waliolala huamka na wale wanaofanya ibada wakati wa usiku kujiweka tayari kwa sala za usiku.

“Pili, taji lake ambalo liko juu ya kichwa chake hufanana na taji la wafalme, na hivyo ana heshima ukilinganisha na ndege wengine. Tatu, hushuhudia malaika kwa njia ya macho mawili ambayo yamewekwa kwenye fuvu lake. Kwa nyongeza, washairi hufananisha rangi ya mvinyo na macho yake, kwa sababu wanapotaka kuelezea mvinyo mwekundu, wanasema: ‘Mvinyo huu ni kama macho mawili ya jogoo.’

“Nne, ubongo katika kichwa chake ni tiba ya matatizo ya mafigo. Aidha, hakuna mfupa ulio mtamu mno kama mfupa wa kichwa chake. Kama ulikitupa kwa mawazo kwamba sitakila, umekosea sana, na hata kama sikuki- la, familia yangu wangekila na kama hawatakila, hawa wageni wangu, ambao hawajakula chochote tangu asubuhi, wangekila.”

Aliendelea kwa hasira, “Nenda ukakilete na ukishindwa kufanya hivyo, nitakuadhibu.” Yule mtumwa akaomba kwa kusihi: “Wallahi! Mimi sijui ni wapi nilipokitupa.” Sa’id akasema kwa hasira: “Wallahi! Najua ni wapi umekitupa, umekitupa kwenye huo mtumbo wako mbaya!” “Wallahi! Mimi sikukila,” alilalama yule mtumwa, “wewe ndiye unaongopa.”

Huku akiwa amechukia, Sai’id alisimama na akamkamata yule mtumwa kwenye shingo kwa nia ya kumtupa chini kwenye sakafu, lakini katika harakati hizo mguu wake ukakanyaga lile bakuli likageuka na vyote vilivyokuwa ndani vikamwagika. Paka ambaye alikuwa amekaa karibu, alitumia fursa hiyo na kuokata yule jogoo asiye na kichwa na kuondoka naye. Sisi pia tukatoka ndani ya nyumba ile, tukamuacha Sa’id akizozana na mtumwa wake.

Imetayarishwa na; Sayyid Ali Akbar Sadaaqat wa Al Islam.org

0 Comments:

Post a Comment