Mohammed 'Adolph' Rishard baada ya kustaafu soka na kuwa kocha wa mchezo huo nchini Tanzania.
Young Africans SC (Yanga) ni klabu ya soka nchini Tanzania ambayo iliasisiwa rasmi kwa jina la New Youngs mnamo Februari 12, 1935.
Mnamo mwaka 1938 lilibadilishwa na kuwa Young Africans yaani Vijana wa Afrika. Wakati Yanga inaasisiwa pia kulikuwa na vilabu vingine vya michezo vya Wazungu na WaAsia kama Goans, European Club, Yatch na Aga Khan na baadaye Sunderland ambayo kwa sasa ni Simba SC iliyoasisiwa mnamo mwaka 1936.
Wengi wa wanachama wa Yanga walikuwa ni wazalendo na wenyeji wa Dar es Salaam na vitongoji vyake. Wakti huo vilikuwa vikikaliwa kwa wingi na watu wenye asili ya Uzaramo, Undegereko, Wakwere, Warufiji na Wamakonde wachache.
Wenyeji hawa katika kuishi kwao walitegemea zaidi uvuvi, biashara, kilimo na shughuli za bandarini. Miaka ilizidi kusonga ambapo Yanga ilifanikiwa kuwa klabu yenye kujitegemea na mfumo mpya wa soka ulipoanzishwa nchini mnamo mwaka 1965, Yanga ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki licha ya kombe hilo kunyakuliwa na Simba.
Katika makala haya yatamwangazia miongoni mwa wachezaji wa Yanga; Mohammed ‘Adolph’ Rishard.
Rishard alicheza soka na klabu ya Yanga miaka ile ya 1970; klabu alizochezea ni West German, Hale (1968), Scotland SC (1969-1970), Young Kids (1971-1973), Yanga (1974-1976) hadi iliposambaratika. Baada ya mgogoro alijiunga na klabu ya Pilsner iliyokuwa ikimilikiwa na kiwanda cha bia kisha akajiunga na Pan African. Mafanikio mengine ya soka ni kuchaguliwa timu ya taifa.
Mnamo mwaka 1977-78 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka, kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Austria mnamo mwaka 1984-85 katika klabu ya SK Austria Klagenfurt, kisha mwaka 1986 alirejea nchini na kujiunga na Pamba ya Mwanza kabla ya ya kutimka tena kwenda nchini Oman katika timu ya Oman SC, mnamo mwaka 1988 alihudumu na Al Nasr, Sohar SC (1993-94) kisha Pan African kwa mara ya pili mnamo mwaka 1995. Pia Rishard alishawahi kuitumikia timu ya taifa, kisha kusomea masuala ya ukocha ambapo amewahi kuwafundisha klabu mbalimbali za soka nchini ikiwamo Tanzania Prisons.
KWANINI
ALIKUWA MAARUFU KWA JINA LA ADOLPH?
Wakati akiwa shuleni miaka ile ya 1960 wanafunzi wenzake walimwita Adolph ambapo wakati huo alikuwapo mchezaji mahiri nchini Ureno aliyefahamika kwa jina la Adolfo Antonio da Luz Calisto.
Adolfo Calisto alikuwa nani katika soka nchini Ureno? Nyota huyo alizaliwa Januari 4, 1944 katika Manispaa ya Barreiro huko nchini Ureno. Katika maisha yake ya soka alipewa jina la ‘Barreiro Lokomotiv’ kutokana na uwezo wake wa kukimbia na kukaba katika nafasi ya ulinzi. Adolfo alikuwa akicheza kama beki wa kushoto.
Alijichotea umaarufu mkubwa na kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea nchini Ureno. Aliwika katika soka miaka ile ya 1960 hadi 1970. Akiwa na Benfica alikocheza mechi 300 na kufumania nyavu mara tano alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi.
Alihudumu na Benfica kutoka msimu wa 1965/66 hadi 1974/75. Alikuwa miongoni mwa wachezaji walioifikisha Benfica kwenye Fainali ya Kombe la Ulaya (kwa sasa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya) mnamo mwaka 1968 ambapo walitandikwa kwa mabao 4-1 na Manchester United katika mchezo uliochezwa katika dimba la Wembley.
Adolfo alistaafu soka akiwa na umri wa miaka 33. Hadi
mwaka 2021 Adolfo ni miongoni mwa wachezaji walio hai waliowahi kuhudumu na
timu ya taifa ya Ureno akiwa na umri wa miaka 77.Adolfo
Antonio da Luz Calisto, enzi zake akiwa na Benfica ya Ureno. Alifahamika nchini humo kama 'Barreiro Lokomotiv'.
0 Comments:
Post a Comment