Jamii mbalimbali zimekuwa na hadithi simulizi katika
maisha yao hususani zilizopo barani Afrikani. Hadithi simulizi ni utanzu wa kimasimulizi
ambao umekuwapo katika jamii tangu kale.
Utanzu huo umekuwa ukitumika katika jamii, ili
kuiburudisha hadhira pamoja na kufikisha ujumbe ikiwamo kuwataka wanajamii
waishi kwa umoja na mshikamano, kufanya kazi kwa bidii ili kuyajenga maisha
yao. Hadithi simulizi hugaiwa kutegemea mtazamo wa mtaalamu husika.
Kwa mfano, Ndungo na Wafula (1993), wanamnukuu Thomson
(1946), akipendekeza kuwa, ngano zinaweza kutambulika kutegemea matukio muhimu
yanayotokea katika ngano hizo.
Mvungi (2010) anaeleza kuwa, hadithi simulizi ni
masimulizi marefu kidogo yanayolenga kuadilisha. Pia, Hadithi simulizi huonesha
tukio la kawaida. Amesisitiza kuwa, matukio yake aghalabu huwa mazuri kwa
baadhi ya wahusika na mabaya kwa wengine.
Mtafiti Hafsa Abdallah Ali mnamo mwaka 2015 alifanya
utafiti wake katika mila na desturi za Wapemba ili kusawiri au kutathmini
nafasi ya mwanamke katika jamii hiyo.
Wataalamu kadhaa wamemchora mwanamke katika hali tofauti,
kuna waliomchora kuwa ni kiumbe duni, shujaa, mlezi wa familia na nafasi nyingine
nyingi. Afrika au Tanzania, Sengo (2009) alimchunguza mwanamke ndani ya familia
na akabaini kwamba vyeo tisa vya mwanamke vya heshima na thamani kubwa.
Wanaume wote wa Afrika wanawake wanawaita mama, mke, binti,
dada, nyanya, mamkwe, mkwe, shangazi, na shemeji Kwa mtazamo huu mwanamke
amebeba hadhi kubwa kupindukia.
Farsy (1956), katika kazi yake amemsawiri mwanamke
kuwa, ni kama pambo na kuhusu hili anasema: “Zamani biharusi alipokuwa,
akioneshwa alasiri, alipohudhurishwa mbele ya wanawake wenziwe huanza kupambwa
tangu mchana, zama hizo walivishwa kiarabu…”
“Wakisukwa ususi wa behedani, kutiwa wanja usoni na
machoni na nakshi nzuri nzuri…. kichwa kizima…..puani hutwa kipini……shingoni
mkufu…….. mapambo yote haya hutiwa kwa ajili ya kumpendezesha mumewe.” (uk.
38).
Robert (1966),anaendelea kuwaelimisha wale wanaosema
kuwa, mwanamke ni kiumbe aliyeleta laana na janga duniani. Katika Pambo La
Lugha,anasema,
“Wanawake wana laana; jibu lako ufedhuli, Tena mimi
naona lawama lastahili; Kuwa, hujui kunena u mchache wa akili; Wanawake bora
sana ni hazina ya awali.”
Hali hii yote mwandishi anaonekana kumkweza mwanamke
na kuachana na dhana ya kumdunisha.
Mohamed (1984) katika utangulizi wa kazi yake ya Kina
Cha Maisha amegusia suali zima la nafasi ya mwanamke.
Mwandishi anasema: “….kwa
kuendelea kumsanifu mwanamke kwa sifa kama mwenye shingo ya upanga mwendo wa
maringo, ama kumfananisha na ndege au tunda kwa kusudi la kuusifia uzuri wake
tu, kumepotosha na kugubika ukweli wa maisha wanavyoishi wanawake katika jamii
nyingi za Kiswahili…”
Mwandishi anatuonesha kuwa, wakati umefika wa
kuzifanya kazi za fasihi kujikita zaidi katika kumkomboa mwanamke, ama
kumkweza. Kazi za fasihi zinazomdunisha mwanamke kwa kiasi fulani zimepitiwa na
wakati.
Mtobwa (1984), alimchora mwanamke katika nafasi kadhaa
kupitia kazi yake ya ‘Pesa Zako Zinanuka’.
Katika kazi hiyo, mwanamke amechorwa kuwa, ni mtu duni
na tegemezi kwa mwanaume, hasa kwa vile anatumika kuwa, ni chombo cha starehe.
Kwa mfano, Mauwa alimstarehesha Born Kandili pamoja na
Daktari. Mwandishi anasema: “Sasa nini?
Kuwa uudhike? Unachotaka ni nini zaidi ya faraja ya kimwili kwa muda wa siku
moja?
Aidha, Mbogo (1993) amemchora mwanamke kuwa ni jasiri
na mwanamapinduzi.
Hali hii ameionesha kupitia Jalia ambaye aliyeongoza
kikosi kumkamata Nungunungu aliyeogopwa na watu wote kupitia umaarufu wake.
Pia, alimpiga Nungunungu bila ya kuogopa vitisho vyake
atoavyo kwa wengine tena bila ya wasi wasi.
Taswira hiyo, ilikuwa ni msingi imara katika kusukuma
mbele umuhimu wa mwanamke.
Kwa mfano, katika hadithi ya Mkaidi Hafaidi, inasema: “Hapo zamani za kale alikuwepo bibi na
wajukuu wake wawili wanawake, watu hao, waliishi msituni ulipofika wakati wa
usiku bibi aliwaambia wajukuu wake wasitoke nje, wajukuu walimuuliza bibi
tusitokenje kwa nini?
Hadithi hiyo inatuonesha kuwa, bibi ni mlezi wa watoto
na kawaida katika ulezi mtoto huweza kuambiwamabaya namazuri ili kuyafuata au
kuyaacha kama bibi alivyotumia nafasi yake katika hadithi hii.
Hivyo basi Wapemba kwa asilimia kubwa wameonyesha
katika hadithi zao kuwa mwanamke ni chombo muhimu hivyo hawana haja ya
kujidharau na kujiona hawafai. Wiki hii ni maalum kwa wanawake; Jambo la msingi
mwanamke anapaswa ajitambue na ajiamini tayari kwa ajili ya kuisaidia Tanzania
kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.