Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi Dkt. Yonazi amesema Serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa wizara zote za kisekta zinashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa miradi iliyopo katika Kijiji cha Msomera inakamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhamia katika eneo hilo ili kuendelea shughuli zao.
Dkt. Yonazi aliyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya Makatibu Wakuu wa Wizara za kisekta waliyoifanya katika Kijiji cha Msomera, Wilaya, Handeni mkoani Tanga kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya kuhamisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari.
Amesema Makatibu Wakuu hao wamekagua ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo maji, umeme, madaraja, barabara, shule, Nyumba za makazi na uboreshaji wa huduma za mawasiliano.
“Niwaombe wanaohamia eneo hili waiamini Serikali kwamba inawatengenezea mazingira yaliyo bora sana hapa Msomera, nyumba zinazojengwa na huduma zote zina ubora ili wananchi wetu wanufaike na Serikali yao waachane na upotoshaji kwa sababu imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama,”Amesema Dkt. Yonazi.
Naye Kamanda wa Kikosi Kazi cha Ujenzi wa nyumba 5000 kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kila taasisi ya kisekta na Wizara zinawajibika ipasavyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati akisema kuwa licha ya changamoto za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali lakini kazi inaendelea vizuri .
“Mpaka sasa ujenzi wa Msomera ambao tumeugawanya katika vitalu kuanzia A mpaka D tuko katika hatua mbalimbali za ujenzi nyumba 1000 katika eneo la Msomera B kitalu F viwanja 768 taratibu zake zimekamilika eneo liko tayari kwa ajili ya uchimbaji na kuanza msingi na kuendelea na hatua za ujenzi,”Ameeleza Brigedia Jenerali Mabena.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando amewashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kutembelea mradi huo hatua inayoongeza kasi yake kusonga mbele akiahidi kusimamia kwa karibu mradi huo ambao umefanyika kama hatua ya kuboresha maisha ya watanzania kila mwananchi kuishi katika hali ya ustawi pamoja na uwepo wa miundo mbinu muhimu pamoja na huduma za kijamii.
“Hii inaonyesha nia ya dhati ya Serikali ya kukamilisha mradi huu muhimu kwa wakati siyo tu kuhamisha watu lakini unaenda kuboresha maisha ya watanzania tunaendelea kuwaahidi kwamba tutasimamia kwa karibu tunajua unatekelezwa wakati wa mvua ambapo kwetu ni fursa ya kuona namna ya kuyavuna maji kwa ajili ya matumizi,”amebainisha
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Bw. Martin Oleikayo Paraketi amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mradi huo akisema umekuja kwa wakati muafaka kwani umesaidia wakazi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo kupata huduma muhimu zikiwemo mawasiliano, ujenzi wa shule za sekondari, kituo cha afya na barabara.
“Hii kwetu ni neema kubwa sana Serikali inafanya kazi kubwa na niwaambie waliopo Ngorongoro wasikubali kupotoshwa na watu wachache wasio na nia njema kijiji cha Msomera ni kijiji mojawapo kati ya Vijiji 91 ndani ya Wilaya ya Handeni mradi huu umeleta faida kubwa kupitia wenzetu waliohamia kutoka Ngorongoro,”Amepongeza Mwenyekiti huyo.
0 Comments:
Post a Comment