Wednesday, November 22, 2023

Warsha ya Wadau wa Uhamiaji Tanzania wafanyika Moshi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani afungua

 


Jeshi la Uhamiaji na wadau wa Uhamiaji wametakiwa kusimamia mahusiano mazuri ya Kidiplomasia katika utoaji wa Huduma za Uhamiaji kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kwa ujumla.


Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku mbili ya masuala ya usimamizi wa Uhamiaji nchini yaliyofanyika katika chuo cha Uhamiaji mjini Moshi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya amesema udhaifu wa mtu mmoja isiwe sababu ya kuharibu diplomasia ya nchi.


Mmuya ameongeza kuwa utoaji wa Huduma za Uhamiaji unapaswa uwe rafiki kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya Utalii ambao ni muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi.


Hata hivyo Katika Warsha hiyo iliyojumuisha Taasisi 100 wadau wa Uhamiaji nchini Katibu Mkuu amekemea vitendo vya rushwa kwa ustawi wa uchumi wa nchi.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala amesema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.


“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,” amesema Dkt. Makakala


Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan amesema, “Uwekezaji ambao unaofanyika Tanzania Bara msije mwekezaji huyo huyo kama anataka kwenda Zanzibar msije mkapata kigugumizi itakuwaje kibali kimetoka Tanzania Bara kiende na Zanzibari ni barua tu muwe na amani msije mkadhani atatiwa ndani.”


Aidha Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji (TRITA) SP Ignatius Mganga amesema, “Hii ni forum pekee nchini ambayo inajadili mustakabili wa shughuli za uhamiaji nchini na kutafutya solutions kwa ajili ya Maendeleo ya nchi yetu.”


Akiwasilisha salamu za wadau wa Taasisi hizo Juma Dossa amesema muunganiko ambao wamefanya na Idara ya Uhamiaji umewasaidia kupata jukwaa la kuwadilisha kero zao na pia kusikia kwa ukaribu zaidi kutoka Uhamiaji.


Warsha hiyo ni ya Tatu kufanyika kwa kuwaleta wadau wa Uhamiaji kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi na kuweka mazingira rafiki ya kulinda usalama wa nchi; kwa mara ya kwanza ilifanyika mnamo mwaka 2021.








0 Comments:

Post a Comment