Monday, November 13, 2023

Rombo Marathon 2023 kufanyika Desemba 23; kuchangisha fedha za ujenzi wa vyoo na Hospitali

Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia  Adolf Mkenda (wa pili kutoka kushoto) katika Rombo Marathon 2022.

 
ROMBO, KILIMANJARO

Kutokana na baadhi ya shule wilayani Rombo kuwa na changamoto ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi Mbio za mwaka huu za Rombo Marathon zinatarajiwa kuwa sehemu ya kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo ili kunusuru magonjwa ya mlipuko mashuleni.


Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia  Adolf Mkenda alisema  mwaka uliopita Rombo Marathon ilikuwa ya kuvutia lakini mwaka huu wameamua kuifikia jamii inayokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo sekta ya elimu.


“Safari hii tumeamua kwamba marathon hii itakuwa ni kukimbia kwa malengo (Run with a Purpose)tumeomba sponsors kadhaa watufadhili kiasi hicho kidogo cha fedha itatusaidia katika maandalizi ya marathon, hela nyingine zitatumika kumalizia harakati kubwa tuliyonayo Rombo ya ujenzi wa vyoo bora katika mashule yetu,” alisema Mkenda.


Mkenda aliongeza kuwa shulea ambazo zitalengwa katika zoezi hilo ni za msingi na za sekondari zenye changamoto za vyoo bora vya kisasa kutokana na vyoo vinavyotumika sasa ni vya shimo vilivyopitwa na wakati.


“Juhudi hizi tulizianza mapema, kama nilivyokuwa mbunge tumeanza nazo, Warombo wamechangia sana; kwa hiyo yeyote atakayekuwa anafadhili shughuli hii atakuwa anasaidia wakazi wa Rombo katika sekta ya elimu,” aliongeza Mkenda.


Katika suala la Mbio za Rombo Marathon 2023 kuchangia upanuzi wa Hospitali wilayani humo alisema, “Fedha nyingine zitazopatikana tutaenda kusaidia upanuzi wa Hospitali ya Huruma,ambayo ipo pale Mkuu ili iweze kuwa hospitali ya kiwango cha mkoa.”


Kwa upande wake Mratibu wa Rombo Marathon Temy Massae alisema mbio za mwaka huu zitakuwa za Kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5 huku washiriki wote wakitarajia kupokea medali za ushiriki wa mbio hizo.


“Tumefanya maboresho makubwa baada ya zile za mwaka jana, mwaka huu zitafanyika Tarakea katika mfumo wa half marathon ya kilometa 21, lakini pia kutakuwa na kilometa 10 ambayo itakuwa na mikimbio ya msituni, pia kilometa 5 nayo ni msituni inainclude social runners wakiwamo watoto, wazee na watu wengine tu wenye hobby na kukimbia,” alisema Massae.

Mwaka huu mbio hizo zinatarajia kuwaleta pamoja wanariadha 1000 ikiwa ni mara mbili ya mwaka 2022 ambapo washiriki 540 walihudhuria, huku Rombo Marathon 2023 itafanyika siku moja kabla ya usiku wa Christmas.


By Jabir Johnson, JAIZMELA correspondent in Moshi

Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia  Adolf Mkenda akimaliza mbio katika Rombo Marathon 2022


0 Comments:

Post a Comment