Wanawake mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuheshimu ndoa zao kwa kuacha kupiga waume zao kwa kisingizio kuwa wanaume hao hawatimizi majukumu ya kulea familia kwa ujumla.
Akizungumza katika ziara ya siku moja ya kuimarisha chama hivi karibuni, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Moshi Mjini Frida Kaaya alisema kuwapiga wanaume sio suluhu ya kutatua changamoto ndani ya familia kwa kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao.
“ Tunapaswa kuendelea kuelimisha suala hili la ukatili wa kijinsia hilo linawezekana, kuna maeneo ambako watu wanaonewa lakini akitaka kupata haki hakuna mtu wa kumsaidia. Wanaume wanapigwa wanaugulia mioyoni,” alisema Kaaya.
Aidha Kaaya aliongeza kuwa kwenye dini kuna maandiko ya kutosha namna ya kutunza familia na kwamba inapotokea mwanamke anafanya hivyo anaibomoa nyumba yake mwenyewe.
“Mwanaume anakufa na pressure kwasababi hana mahali pa kulipeleka, dawati la jinsia lipo peleka hapo; kina mama na sisi tuache kuwafanyia ukatili eti hana mahali pa kupeleka; mwanamke mpumbavu anavunja nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe,” alisema Kaaya.
Kaaya alisisitiza kuwa katika Jeshi la Polisi kuna dawati la jinsia ambalo pia lipo kwa ajili ya kusikiliza changamoto wanazokutana nazo wanaume katika masuala ya ukatili wa jinisia na kusisitiza kwamba inapotokea wanafanyiwa hivyo wasiache kwenda kueleza yanayowasibu badala ya kukaa kimya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini Faraji Swai alisema vitendo vya ukatili kijinsia vinatakiwa kupigwa vita kila kukicha na kwa nguvu zote ili kujenga jamii yenye kuheshimiana
“Vitendo hivi sio vya kunyamazia, serikali yetu ya awamau ya sita ina utataribu mzuri imeweka madawati ya jinsia kwa ajili ya kupinga vitendo kama hivyo ili kujenga jamii yenye kuheshimiana, ndugu zangu maendeleo yanaanzia nyumbani,” alisema Swai.
Wakazi wa Moshi wametoa maoni yao ambapo wanasema vitendo kama hivyo vipo mkoani Kilimanjaro lakini wanaume wanakaa navyo moyoni bila kupeleka kokote.
“Suala hili lipo miongoni mwa wanajamii, ni vigumu kwa mwanaume kutoka na kwenda kulalamika mbele ya jamii kuwa amedundwa na mkewe, nashauri wajaribu kubadilisha maisha kuzungumza na wake zao, licha kwamba wanawake wengine ni jeuri,” alisema Boniface Nyanda.
Kanuni ya usawa wa kijinsia imejumuishwa ndani ya Katiba ya Tanzania na marekebisho yaliyofuata; na dhamira ya serikali ya Tanzania kwa usawa wa kijinsia inathibitishwa katika kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi wa aina zote.
0 Comments:
Post a Comment