Wednesday, November 29, 2023

Kaburi lafukuliwa lakutwa na Sanda nyeusi, Nazi Tatu na Yai Viza



Wananchi wa Mtaa wa Mafuriko, iliyopo Kata ya Mzizima Mkoani Tanga wamepata taharuki baada ya kusambaa kwa taarifa za uwepo wa kaburi la Mwanamke mmoja mwenye asili ya kiarabu aliyeuawa na kuzikwa  kwenye eneo la Mwekezaji kitendo kilichopelekea Serikali kuamua kufukua kaburi hilo ili kujiridhisha.


Akiongea baada ya zoezi la uchimbaji wa kaburi hilo Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji amesema Mara baada ya kupata taarifa walichukua hatua za kufukua kaburi hilo kwa kibali cha Mahakama ambapo baada ya  kufukua kaburi wamekuta sanda nyeusi, nazi tatu na yai viza


“Ni kaburi ambalo lilionekana lipo ndani ya eneo la Mwekezaji lakini sambamba na hilo wakati tunaendela na ufukuaji tumekuta Wananchi wengi wamevamia eneo la Mwekezaji ambalo limepimwa viwanja kwa kisingizio kwamba hawana maeneo ni kana kwamba wametengeneza tukio hilo ili kumtisha Mwekezaji na Watu waliopimiwa viwanja”


DC Kaji amepiga marufuku Mwananchi yeyote kuonekana katika eneo hilo la Mwekezaji akisema kumekuwa na tabia ya Wananchi kuvamia maeneo ya wazi na baadaye kuomba fidia kwa Serikali jambo ambalo linapelekea matatizo makubwa ya migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi ni uvamizi wa Wananchi  kwenye maeneo yenye hati miliki


“Nimetoa onyo  na hatutamvumilia Mtu yeyote na wengi wamekuwa wakikimbilia kwa Wanasiasa kwamba ni Wapiga kura wetu hilo halitakuwepo na hatutalivumilia, Tanga tunaweza kuishi bila migogoro” amesema James Kaji


#Khadija Bagasha, Tanga.

0 Comments:

Post a Comment