Thursday, November 23, 2023

Huduma za Uhamiaji zinavyoweza kukuza uchumi wa Tanzania

Idara ya Huduma za Uhamiaji imeanzishwa chini ya Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 1995 Sura ya 54 iliyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 2015.

Kifungu hicho kinaipa Idara mamlaka ya kudhibiti na kuwezesha masuala ya uhamiaji katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Idara hii ni moja ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Kazi kubwa ya Jeshi la Uhamiaji ni Kudumisha Usalama wa Taifa kupitia Udhibiti wa Uhamiaji. Kutoa hati za kusafiria na hati zingine za kusafiria kwa raia wa kweli. Kutoa Vibali vya Ukaazi na Pasi kwa wageni anaoishi nchini. Kurahisisha na kudhibiti mienendo ya watu ndani na nje ya nchi. Kuratibu na kuwezesha maombi ya Uraia wa Tanzania.


Siku hizi diplomasia hutumika kwa masuala ya biashara, uchumi na utamaduni pale nchi zikisainiana mikataba.


Diplomasia inamdai mhusika awe na utaalamu hasa upande wa sheria, pamoja na ustaarabu na sifa nyingine zinazorahisisha mafungamano.


Mnamo mwaka wa 2019, Afrika Mashariki ilikaribisha sehemu kubwa zaidi ya wahamiaji wa kimataifa wanaoishi Afrika (30%), ikifuatiwa na Afrika Magharibi (28%), Afrika Kusini (17%), Afrika ya Kati (14%) na Afrika Kaskazini (11%).


Uhamiaji ulioandaliwa na kupangwa unaweza kuleta maendeleo barani Afrika katika siku zijazo. Miaka michache ijayo, Tanzania itapata ongezeko la wawekezaji wa kigeni na pia watu kutoka mabara mengine; kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.


Dhana ya diplomasia ya uchumi inaweza kumaanisha uwakilishi wa nchi nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi. Mambo haya ni pamoja na yale yahusuyo uwekezaji na biashara. Kila moja kati ya haya ni muhimu kwa nchi yoyote inayojihusisha kiuchumi na mataifa mengine.


Kuna mambo ya msingi ambayo lazima yaeleweke vizuri na yazingatiwe ili diplomasia ya uchumi ifanikiwe.


Mosi; Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali. Ili kuvutia uwekezaji kunahitaji ujuzi maalumu. Pia, lazima kujua fursa na miradi ya uwekezaji iliyopo katika nchi.


Pili; kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kufanya biashara na nchi za nje kwa urahisi. Mambo haya ni pamoja na kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika. Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.


Tatu; shughuli za kuvutia watalii kutoka nje ya nchi kuingia nchini zinapaswa kuwemo.  Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu walio nje ya nchi wanapaswa kuwa wawezeshaji katika kuletwa watalii nchini.


Mnamo Novemba 22, 2023 Jeshi la Uhamiaji nchini  pamoja na wadau wa Uhamiaji ambao ni taasisi za umma na binafsi zipatazo 100 zilikutana katika Chuo cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) kilichopo mjini Moshi kwenye warsha ili kujadili namna Usimamizi wa Huduma za Uhamiaji unavyoweza kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi ya taifa.


Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku mbili Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya alisema udhaifu wa mtu mmoja isiwe sababu ya kuharibu diplomasia ya nchi.


Mmuya aliongeza kuwa utoaji wa Huduma za Uhamiaji unapaswa uwe rafiki kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya Utalii ambao ni muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi.


Hata hivyo Katika Warsha hiyo iliyojumuisha Taasisi 100 wadau wa Uhamiaji nchini Katibu Mkuu amekemea vitendo vya rushwa kwa ustawi wa uchumi wa nchi.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala alisema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.


“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,” amesema Dkt. Makakala


Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan alisema, “Uwekezaji ambao unaofanyika Tanzania Bara msije mwekezaji huyo huyo kama anataka kwenda Zanzibar msije mkapata kigugumizi itakuwaje kibali kimetoka Tanzania Bara kiende na Zanzibari ni barua tu muwe na amani msije mkadhani atatiwa ndani.”


Aidha Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji (TRITA) SP Ignatius Mganga amesema, “Hii ni forum pekee nchini ambayo inajadili mustakabili wa shughuli za uhamiaji nchini na kutafutya solutions kwa ajili ya Maendeleo ya nchi yetu.”


Akiwasilisha salamu za wadau wa Taasisi hizo Juma Dossa alisema muunganiko ambao wamefanya na Idara ya Uhamiaji umewasaidia kupata jukwaa la kuwadilisha kero zao na pia kusikia kwa ukaribu zaidi kutoka Uhamiaji.


Warsha hiyo ni ya tatu kufanyika kwa kuwaleta wadau wa Uhamiaji kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi na kuweka mazingira rafiki ya kulinda usalama wa nchi; kwa mara ya kwanza ilifanyika mnamo mwaka 2021.


Tanzania ni sisi, tunataka muungano, ustawi, amani, kupitia ujasiri wa watu mbalimbali. Pamoja tuna nguvu, na ili kubaki na nguvu ni  lazima tushirikiane, tubadilishane mawazo ujuzi, tufunzane, tuwe na mtazamo mmoja na tusonge mbele pamoja, tuwe na maono sambamba na tusonge pamoja katika njia moja, tuwe na mdundo mmoja.

0 Comments:

Post a Comment