Wizara
ya Maliasili na Utalii imesema inaendelea na mpango kazi wa kupunguza
usafirishaji wa magogo nje ya nchi ikiwa
ni mkakati wa kupunguza bidhaa ghafi za mazao ya misitu na kuongeza uwekezaji
wa ndani.
Katika
ujumbe wake Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas Said
uliowasilishwa katika Mahafali ya 26 ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi na Mkurugenzi
wa Utafiti na Mafunzo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema
serikali imejielekeza zaidi katika kuanzisha viwanda hivyo ni lazima kupunguza
usafiri wa mazao ghafi kwendanje ya nchi.
“Ukiangalia sasa hivi serikali mpango wake ni
kupunguza usafirishaji wa magogo nje ya nchi, kupunguza bidhaa ghafi za mazaoa
ya misitu kwenda nje ya nchi ili kuwekeza zaidi ndani, wale wote wanaowekeza
ndani wanapewa kipaumbele cha kupata hizo bidhaa ili waweze kuzalisha hapa”
amesema Dkt. Abbas
Aidha
Dkt. Abbas ameongeza kuwa viwanda mbalimbali nchini vipo mbioni kupatiwa
leseni kwa ajili ya kutumia mazao ghafi
ya misitu hivyo kuongeza ajira kwa vijana nchini.
“Kwa
sasa tayari maeneo ya Mufindi, Njombe, wameanza kujiandaa kupewa leseni kwa
ajili ya viwanda ambavyo vitatumia malighafi hizo hapa nchini badala ya
kusafirisha kwenda nje ya nchi, kwa hiyo kuna muda ambao umewekwa na serikali
baada ya muda huo kupita
hakutakuwa na huo usafirishaji wa magogo ghafi kwasababu viwanda
vingi vitakuwa vimejengwa hapa nchini na vijana wetu wataendelea kupata ajira,”
amesema Dkt. Abbas katika ujumbe wake uliowasilishwa na Dkt. Kohi.
Aidha
Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Deusdeit
Bwoyo alisema kuhusu mabadiliko ya tabianchi kuwa ni suala ambalo kila
mtanzania anapaswa kupambana nalo kwa kupanda miti kwa wingi ambayo itarudisha
sura ya dunia kama awali.
“Misitu
yetu imeathirika sana, leo unaposikia kuna mioto mingi misituni, ni sababu
zingine zinachangiwa na mabadiliko ya tabianchi, ukame unakuwa ni mkubwa kuliko ilivyokuwa awali. Leo unaposikia miti
imeungua ikafa ni kwasababu ya mabadilio ya tabianchi, kuna Wadudu wengine
wamekuja sasa ambao sio wazuri sana na wana athiri sana misitu yetu,” amesema
Bwoyo.
Mkuu
wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) Dkt. Lupala Zacharia alisema tangu
mwaka 1976 chuo hicho kilipojengwa idadi ya watoto wa kike katika masomo ilikuwa
kidogo lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka kwa baadhi ya kozi jambo ambalo
linatia moyo katika kumwinua mtoto wa kike.
“Rais Samia ameifungua nchi kwa utalii imekuwa kipaumbele, watalii wameongezeka sana, fursa za utalii ndani ya maeneo ya vijana wamekuwa wabunifu; Teknolojia ya viwanda vya misitu ilitawaliwa sana na mfumo dume , kutokana na hamasa iliyofanywa imehamasisha sana watoto wa kike kujitokeza kuziona fursa mbalimbali, kwa sasa kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa vijana wa kike kupenda kusoma masomo ya yetu,” amesema Dkt. Lupala.
Kwa
upande wa wahitimu wa ngazi ya cheti na diploma walisema juhudi zinatakiwa kwa
ajili ya kubadili miundombinu ikiwamo kuachana na teknolojia ya zamani katika
masomo na kwenda na wakati ili kufikia malengo.
“Kwa
upande wa mashine zetu, mashine ambazo tunazitumia ni mashine ambazo tayari
zimeshapitwa na wakati kutokana na teknolojia kukua, tunapokwenda kwenye
mazoezi ya vitendo, Unakuta masomo ya darasani tumefanya na mashine ambayo ni
ya zamani, lakini tunapokwenda kwenye mazoezi ya vitendo tunakutana na mashine
zingine ambazo ni mpya,” amesema Edina Kweka, mhitimu wa ngazi ya Astashahada
Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi.
Wahitimu
200 wa astashahada na stahada walihitimu mafunzo katika Chuo cha Viwanda vya
Misitu Moshi.
0 Comments:
Post a Comment