Thursday, November 23, 2023

TRITA kuongoza wadau Uhamiaji kuzuru Arusha National Park


Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Tanzania(TRITA) kilichopo Moshi mjini Mkoa wa Kilimanjaro, kinatarajiwa kuongoza ujumbe wa Wadau wa Uhamiaji nchini kuzuru Hifadhi ya Taifa Arusha, ikiwa ni madhumuni ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini na kuchangia ukuaji wa mapato yanayotokana na utalii nchini.


Akizungumza jana na Mwandishi wa Tanzania Leo, Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji nchini, Mrakibu Paul John Msele, alisema lengo la ziara hiyo katika hifadhi ya Taifa Arusha ni kuhamasisha watanzania kujiwekea desturi ya kuzitembelea hifadhi za taifa zilizopo karibu na maeneo yao  ili kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya hifadhi hizo.


Mrakibu Msele alisema, ziara hiyo itaongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) SP Ignatius Mganga, ambapo ataongoza taasisi 100 ambao ni wadau wa Uhamiaji nchini, waliopo mkoani humo kwa ajili ya kushiriki warsha inayohusiana na Masuala ya Usimamizi wa Uhamiaji nchini yanayofanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA), Kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro.


Alisema imechukulia kwa umuhimu mkubwa tukio la uzinduzi wa Filamu ya The Royal Tour kwa sababu ni hatua ambayo Rais Samia mwenyewe alichukua jukumu la kuieleza dunia  vivutio  mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini ili kuweza kutoa Uwekezaji na masuala ya utalii katika kuongeza pato la Taifa.



Akifungua Warsha ya siku mbili ya Masuala ya Usimamizi wa Uhamiaji nchini iliyofanyika katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA), Mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya, alisema Rais Samia amefanya jitihada kubwa sana ya kuitangaza nchi ya Tanzania duniani kuwaambia ni nchi yenye vivutio vingi, vya kiutalii nchi yenye fursa za kiuwekezaji, na kuna amani na utulivu.



“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya jitihada kubwa sana za kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kuwaambia kuwa ni nchi yenye vivutio vingi vya kiutalii, nchi yenye furza za kiuwekezaji na kuna amani na utulivu,”alisema Mmuya.


Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala alisema Warsha na taasisi hizo umepunguza kwa kiasi kikubwa vishoka katika utoaji wa vibali mbalimbali nchini hatua ambayo imesaidia mapato kupatikana kwa manufaa ya wengi.



“Awali tulikuwa tunapata shida wadau wetu wanapata huduma lakini wakati mwingine wanaangukia katika mikono ambayo siyo salama lakini tangu tumeanza programu hii mwaka 2019 tumekuwa na magrupu mbalimbali kutoka kwenye taasisi tumekuwa tukikaa nao kwa pamoja tunazitatua hizo changamoto,na idadi kubwa ya wageni imekuwa ikiongezeka,” alisema Dkt. Makakala.



Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Juma Dossa, kutoka  Hospitali ya Aga Khan anayesimamia vibali vya wageni wote wanaokuja kutoa huduma  katika  hospitali hiyo  kama  vile madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wa mitambo, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo ina vivutio vingi vya kutembelea kwa ajili ya utalii na watu wengi duniani wameitambua kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour.



0 Comments:

Post a Comment