Tuesday, November 21, 2023

Mutatembwa ahimiza uzalishaji Bora wa vipi vya TV kuhusu Utalii



Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa amewahimiza wenye dhamana ya uzalishaji wa vipindi kuzingatia viwango vya kimataifa katika vipindi vinavyoandaliwa ili malengo ya uanzishwaji yatimie


Naibu  Katibu  Mkuu huyo  ameeleza  hayo  katika  kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu iliyokutana Jijini Dodoma kwa lengo la kujadili mikakati ya kuendeleza channel hiyo ambapo ametoa wito kwa Wizara zote zinazohusika na  wadau wa Chaneli hiyo kuhakikisha zinailea.


Amesema Channel hiyo ya kujivunia inatajwa kuwa na mvuto wa kipekee ambapo mipango na mikakati yake inapaswa kusimamiwa vizuri ili kufanikisha uendelezaji wa chaneli hiyo muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa.


“Kuanzishwa kwa chaneli hii inayotengeneza vipindi na kuonesha vivutio hivi ndani na nje ya Tanzania itasaidia watalii huko waliko kujua huu utajiri wetu na kuchagua kuja kutalii nchini.  Tuzingatie uandaaji wa vipindi vyenye ubunifu na ubora vinayovutia watazamaji,” Ameeleza Bw. Mutatembwa.


Akiwasilisha taarifa ya Utendaji Kazi  wa  Tanzania  Safari  Channel  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba amebainisha kwamba kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu waliotembelea chaneli hiyo katika mitandao ya kijamii kuanzia Julai 2023 hadi Oktoba 2023.


“Wafuatiliaji katika tovuti wamefikia 154, 996 kutoka 153,873 katika mitandao ya kijamii kama vile Youtube wamefikia 5,530 kutoka 5,030, Instagram kutoka 36,800 hadi 39, 704, facebook kutoka 26,582 hadi 27,907 wakati Twitter wakifikia 1,076 hadi 1,318 na Progamu tumizi wamefikia 137,399 kutoka 137, 297,”Amefafanua Dkt. Rioba.


Kwa upande wake Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Said Shaib Mussa ameleza kwamba Chaneli hiyo inaweza kutumika kubadilisha mtazamo wa  baadhi ya watalii kwa kuonyesha vivutio, utamaduni uliopo nchini bila kuathiri dini au mila za watu wengine.


Aidha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakele amepongeza hatua kubwa inayopigwa tangu kuanzishwa kwa chaneli hiyo licha ya uwepo wa changamoto hasa zinazotokana na bajeti ambapo amesema miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni kuendelea kuunga mkono uendeshwaji wake.


Tanzania Safari Channel,ni miongoni mwa channel za Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC) ambayo ilianzishwa Desemba  15 mwaka 2018, ikiwa ni channel pekee inayojikita katika suala zima la kutangaza  rasilimali za maliasili na utalii.







0 Comments:

Post a Comment