Friday, October 27, 2023

KAHAWA FESTIVAL 2023: Vijana watakiwa kurudisha mnyororo wa thamani wa zao la Kahawa

Vijana wanaoishi katika mikoa mipya ya kahawa nchini wametakiwa kurudi shambani kwa ajili ya uzalishaji wa zao la kahawa ili kuongeza mnyororo wa thamani na maendeleo yao kwa ujumla.

Akizungumza na JAIZMELA katika ufunguzi wa Maonyesho ya Kahawa (Kahawa Festival 2023) yanayoendelea katika viunga vya Coffee Curing Moshi, Kilimanjaro Meneja Mradi wa CODE-P Emmanuel Mahululu amesema mkakati wa kuwarudisha vijana katika uzalishaji wa zao la Kahawa katika mikoa ya Songwe, Ruvuma na Mbeya inakuja kutokana na dhana kwamba wakulima wa zao hilo ni wazee.


“Tumekuwa tukitumia tool mbalimbali kuwafikia vijana ikiwamo kujumuisha familia namna inavyopanga majukumu yao wanashirikiana pia tunahamasisha vijana wazungumze na wazee wawape mashamba yao wayalime,” alisema  Mahululu.


Aidha Mahululu amesema uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukitegemea soko la nje na ndio sababu mradi wa CODE-P ambao umejikita katika wakulima wadogo wa zao hilo umekuwa ukipata ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya.


“kahawa inayozaliwa Tanzania asilimia 97 inasafirishwa kwenda nje, Hili ni zao la kimkakati ambalo linatusaidia sisi kupata fedha za kigeni,” alisema Meneja Mradi CODE -P


Mahululu amesema miaka mitano iliyopita mikoa ya Mbeya, Songwe na Ruvuma mti wa kahawa ulikuwa ukitoa gramu 540 ukilinganisha na mikoa ya Magharibi nchini ambayo ilikuwa ikitoa kilogramu 1.8 na kwamba malengo Mradi wa CODE-P ni kufikia wakulima 24,000 wa rika la vijana kati ya miaka 18-35 miongoni mwao vijana wa kiume 9,600.


Kwa upande wake Mgeni Rasmi wa Kahawa Festival 2023 Profesa Aurelia Kamuzora amesisitiza ulazima wa vijana kujikita katika uzalishaji wa zao hilo ili kuimarisha soko la ndani na soko la nje.


“Mahitaji ya unywaji wa kahawa duniani yameongezeka kadri watu wanavyoongezeka na unywaji wa kahawa unaongezeka, soko la kahawa lipo endapo tutajipanga kutumia mbinu zinazotakiwa,” alisema Profesa Kamuzora.


JAIZMELA imezungumza na mdau wa Kahawa Ibrahimu Mbwana kutoka AFRICAFE ambaye ni muuzaji wa bidhaa zinazotokana na kahawa amesema fursa kwa vijana zipo kutokana bidhaa za kahawa zinatumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo mahoteli.


“Kikubwa ninachowaomba watanzania tuweze kutumia vitu vyetu vya ndani; hapa Moshi kuna mashamba mengi yanayoweza kuzalisha kahawa tuanze kwanza kutumia sisi ndipo tuwaeleze na wengine,” alisema Mbwana wa AFRICAFE


Kilimo cha Kahawa kinaanza na maandalizi ya shamba jipya la kahawa, ama kwa kusafisha ardhi mpya au kukarabati shamba la zamani lenye kahawa zilizozeeka na lisilo na tija au kupanda shamba jipya kutokana na mashamba mengine ambayo yalitumika kwa mazao mengine na kuandaa shamba huko kunatakiwa kufanyike wakati wa kiangazi na kwa kutumia trekta au jembe la mkono.






0 Comments:

Post a Comment