Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto imekuwa ya pekee nchini, kupeleka wagonjwa waliopona kifua kikuu , kwenye hifadhi za Taifa kuwatibu kisaikolojia.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo , Dkt. Leonard Subi, ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo, katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa wateja, ambapo amesema takribani wagonjwa 76 wamepelekwa kutembelea hifadhi mbalimbali za taifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Subi amesema wagonjwa hao walitembelea hifadhi ya Taifa Tarangire, Arusha na Mamlaka ya Ngorongoro kwa lengo la kujionea vivutio na kuhamasisha utalii wa ndani.
“Dhamira ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ya kuutangaza utalii wetu, ni kukuza utalii wa nchi yetu na kuongeza idadi ya watalii nchini, ambao wanafika kuja kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi zetu,”.
Amesema “Katika kumuunga mkono , sisi tumeanzisha utaratibu wa kuwapeleka wagonjwa wetu ambao walikuwa wakitibia katika hospitali ya Kibong’oto na wamepona , kwenda kutembelea hifadhi hizi,”alisema Dkt. Subi.
Amesema mwaka 2022 wagonjwa wapatao 40 walitembelea hifadhi na kwa mwaka huu takribani wagonjwa 36 watakwenda kutembelea hifadhi ya taifa Tarangire.
Amesema Rais Dkt. Samia amekuwa mstari wa mbele kuutangaza utalii kuptia Filamu ya Tanzania: The Royal Tour, ambayo imekuwa maarufu nchi nyingi kiasi cha kuongeza watalii na biashara za utalii kwa ujumla.
Dkt. Subi amesema ili serikali ipate fedha nyingi za kigeni na kuimarisha uchumi wa nchi, Watanzania ni vizuri wakajenga utamaduni wa kutembelea vivutio hivyo kwani ni jambo la msingi na ndiyo maana Tanzania haijawahi kuyumba .
Amesema unapokuwa na kiongozi wa nchi mahiri ni moja ya mambo ya msingi ambayo anaendelea kujifunza kwake.
Amesema wagonjwa si tu kuwapatia dawa , sindano au kuwapatia Huduma za tiba kila siku, badala yake ni vyema pia wapate Huduma za kisaikolojia baada ya kupona kabisa.
Aidha Dkt. Subi amesema Huduma hizo za kisaikolojia ni sehemu ya Huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi ya Kibong’oto katika kuwapa faraja wagonjwa hao.
“tunapowapeleka wagonjwa hawa katika hifadhi ya Taifa, kwanza kiyu cha kwanza tunazingatia sana uzuiaji wa maambukizi , hatuwapeleki wagonjwa ambao tayari wana maambukizi , hapana sisi tunafanya ufuatiliaji wa karibu sana wa matibabu kwa wagonjwa wetu, tunawaelimisha na hiyo ni kutokana na utaratibu,”amesema.
Katika hatua nyingine Dkt. Subi amewataka watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha, mambo ya msingi wanayakumbuka na wajibu wa mtoa Huduma.
Amewataka kuwa na nidhamu kazini, kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, kuheshimu watu, kuonesha upendo na kutumia taaluma yake kwa ufasaha katika kuwahudumia Wananchi.
“Tambueni hata sisi iko siku tutaugua, kile unachokihitaji wewe uhudumiwe na daktari wakati ukiwa mgonjwa ndicho hichohicho na wewe mtoa Huduma ya afya unatakiwa kuendelea kumhudumia mwananchi.
Kwa upande wake Muuguzi msaidizi wa Cliniki ya gari tembezi Dkt. Finias Mkulia amesema gari hilo hadi mpaka sasa limewafikia watu 15,000 katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, ambapo kwa kipindi cha miaka mitano kutoka Mwaka 2017 hadi Juni 2022 iliweza kuwafikia wachimbaji wa madini 8,000 na kati yao 850 waligundulika kuwa na kifua kikuu na kuweza kuwaweka kwenye matibabu.
Alisema Huduma hizo zinatolewa bila malipo kwani serikali inagharamia gharama zote za watumishi kuweko katika eneo la kazi na kuweza kufanya kazi katika mikoa mbalimbali.
“Tayri gari hili limeweza kuhudumia katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songwe, Kagera, Mara na mkoa wa Geita,”amesema.
Nao baadhi ya wagonjwa wa kifua kikuu ambao walinufaika na ziara ya kutembelea hifadhi ya taifa Tarangire Rhoda Timotheo, mkazi wa Arusha Salehe Shaban, Robert Singani kutoka Rukwa na Shukrani Salehe Mwatendeli kutoka mkoa wa Mbeya, wameushukuru uongozi wa Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, kuweza kuwapeleka katika hifadhi hiyo na kuweza kujionea vivutio mbalimbali kwani tangu kuzaliwa hawajawahi kuwaona wanyama kama tembo, twiga , simba na ndege wa aina mbalimbali.
0 Comments:
Post a Comment