Wednesday, April 19, 2023

Moshi DC yaipongeza AKO Tanzania Community Support

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi DC akifunua mfuniko wa mojawapo ya Sufuria la chakula kwa ajili ya watoto wa shule ya msingi Sungu wakati wa ziara ya kukagua ukarabati wa shule hiyo kwa hisani ya Ako Community Tanzania

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi Moris Makoi ameipongeza na kuishukuru taasisi isiyo ya kiserikali ya Ako Tanzania Support kwa msaada wao walioutoa kuzikarabati Shule za Msingi Sungu na Uchau zilizopo Kibosho huku akitoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi za wahisani hao.

Makoi ameyasema hayo tarehe 19 Aprili 2023 wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua kazi iliyofanyika baada ya wahisani hao Ako Tanzania Community Support kwa ushirikiano na Ako Community Support kutoka Ujerumani kufanikisha ujenzi na ukarabati wa majengo za shule hizo.

Akiwa na timu ya elimu kutoka katika halmashauri hiyo Makoi amesema shule hizo zimejengwa muda mrefu lakini zimekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo vyoo, vyumba vya madarasa, majiko hali ambayo imekuwa ikisababisha mazingira magumu kwa wanafunzi wanaosoma humo walimu wanaowafundisha.

“Tumefika Sungu na Uchau na tumeona kazi kubwa waliyoifanya kwa gharama kubwa, baada ya mazungumzo nao kwa kina wameniahidi sasa watakarabati na madarasa karibu matano na ofisi za mwalimu; kikubwa katika ziara hii ilikuwa ni kutambua mchango wao katika jamii hii, kuwashukuru na kuonyesha kwamba serikali iko nao katika shughuli hizi ambazo wanafanya,” amesema Makoi.

Hata hivyo Makoi amesema haikua rahisi kukubali msaada wa kufanyiwa ukarabati katika shule hizo kwani sio kila msaada ni wa kuukubali kutokana na hofu iliyotanda ya misaada ambayo imekuwa ikienda kinyume na utamaduni wa Watanzania.

“Kama mwenyekiti wa halmashauri nimefika hapa kwa ajili ya kujiridhisha kama msaada unakidhi vigezo vya msaada; misaada tunayoitaka kama nchi sasa isije ikawa misaada ya kigeni ambayo inakuja kuingilia utamaduni, mila na desturi zetu, nimejiridhisha kwamba Ako Tanzania Community Support wako tu kwa ajili kusaidia na sio kuja kutuingiza katika mambo yasiyofaa,” ameongeza Makoi.

Pia Makoi ameitaka jamii inayozunguka shule hizo kuwa walinzi huku akiwataka walimu kuhakikisha rasilimali hizo inatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Akizungumza na JAIZMELA mwakilishi wa AKO Community Support ya Ujerumani Dieter Jaenicke katika program ya ujenzi wa jiko, ukumbi wa chakula na ukarabati wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Uchau amesema elimu ndio tumaini pekee kwa kila jamii hapa ulimwenguni.

“Kwa niaba ya Ako, nataka kueleza kwa nini tupo hapa, tunaamini kwamba watoto ni mustakabali wa nchi, na elimu kwa watoto ni muhimu zaidi kwa kila nchi duniani na tuna furaha kubwa tunaweza kukusaidia kidogo. kidogo kwa nguvu na vyanzo vyetu kufanya elimu ya watoto kuwa nzuri iwezekanavyo,” amesema Jaenicke.

Mwakilishi huyo aliongeza kuwa alipofika na kuyaona mazingira ya shule alihisi kugusw akufanya kitu kwa ajili ya watoto wa Kitanzania

“Niliona shule hii haiko katika hali nzuri na nikaona ni lazima tufanye kitu… na kipaumbele cha kwanza wanahitaji jiko la shule na sasa jiko lipo…”amesema Jaenicke

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Sungu Redempta Assey amesema wanaushukuru uongozi na wahisani AKO Community Support pande zote mbili ya Tanzania na Ujerumani kwa kuwaona na kuleta misaada ambayo ina nia ya maendeleo kwani watoto watasoma katika mazingira bora na Tanzania itajengeka.

“Tunawashukuru sana wafadhili kutoka Ako Ujerumani kwa msaada wao kwa kutukarabati shule hii ilikuwa na changamoto ya madarasa kuwa mabovu sana tunaahidi tutayatunza, huu ukarabati utasaidia taaluma itazidi kupanda juu,” amesema Assey.

Mkuu wa Shule ya Msingi Uchau Agnes Mbwambo amesema kuwajengea jiko linalotunza mazingira, ukumbi wa chakula na ukarabati unaotarajiwa kuanza wa vyumba vya madarasa ni jambo zuri la lenye faida kwa watanzania.

“Tunawashukuru sana, sana, sana tunaomba waendelee kuwa karibu nasi na Mungu awabariki,”amesema Mbwambo.

Miradi hiyo imegharimu kiasi cha Shilingi mil. 340 za Tanzania kati ya hizo mradi wa Sungu umegharimu kiasi cha shilingi mil. 100 na wa Uchau umegharimu kiasi cha shilingi mil. 240

Mwonekano wa mojawapo ya majengo ya Shule ya Msingi Uchau. Shule hiyo ilijengwa mnamo mwaka 1948 na wamisionari kutoka Ujerumani.

Mwakilishi wa Ako Community Support ya Ujerrumani Dieter Jaenicke akizungumza jambo kwa viongozi wa Halmashauri ya Moshi DC waliozuru katika Shule ya Msingi Uchau kujionea program maalumu ya kuikarabati shule hiyo


0 Comments:

Post a Comment