Friday, April 7, 2023

Wadau wafunguka Lengai Ole Sabaya kufungwa kifungo cha nje

Zikiwa zimepita siku mbili tu baada ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, ambaye amekuwa akikabiliwa mashtaka saba ikiwemo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu kufungwa kifungo cha nje, wadau wa siasa mkoani Kilimanjaro wameibuka na mitazamo tofauti.

Mitazamo ya wadau hao wa siasa imegawanyika katika pande mbili zinazokinzana huku wengine wakimuona shupavu na wengine wakiona kama hakustahili kupata kifungo hicho cha masharti.

Jesse Tunuka anasema kuachiwa kwa Sabaya ni funzo kwa vijana wenye maono ya kutaka kuwa viongozi wa wananchi  huku akisisitiza kutenda kazi kwa haki pasipo kumuonea mtu wala majigambo ni mambo makuu ya kuzingatia

“Unajua fika Sabaya alikuwa na majigambo mengi wakati wa utawala wake huko Hai, hata hivyo inatoa somo kwa vijana wapenda madaraka kuwa wanapaswa kujizatiti kwa kutomuangalia mtu bali kwa kujali haki na wajibu wa uongozi,” alisema Tunuka.

Aidha mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mary Tarimo anasema, kifungo cha nje kwa Sabaya hakitoshi kwani alipaswa afungwe jela na kuongeza kuwa Sabaya katika mapambano yale hayuko peke yake wapo na wengine ambao wanapaswa kutafutwa na kufunguliwa mashtaka.

Hata hivyo upande mwingine wa mitazamo ya watanzania inamuona Sabaya kama kijana shupavu katika siasa za Tanzania huku akifananishwa na wanasiasa wakongwe waliowahi kushika nyadhifa kadhaa nchini.

“Mara nyingi wanasiasa Mashupavu kama akina Shaka na Lengai Ole Sabaya wanapitia katika masahibu mengi sana hata kufungwa jela hata kunusurika kuuwawa lakini hiyo haiwezi kuzima ndoto zao za kupigania vitu wanavyoviamini...Mapambano ya Kisiasa ni kufa na Kupona wakati mwingine hata kupoteza Maisha,” alisema (jina limehifadhiwa).

“Lengai Ole Sabaya ni Shujaa Kijana na kiongozi Mahiri wa Baadae wa Chama cha Mapinduzi huko Kaskazini mwa Tanzania anachopaswa kufanya ni kutuliza akili na kujijenga ndani ya chama na kuachana na Vyeo vya Uteuzi. ..Lengai Ole Sabaya atakuja kuwa moja ya Wanasiasa wakubwa katika Ukanda wa Kaskazini kama akina Edward Sokoine, Edward Lowassa na Cleopa David Msuya,” aliongeza mdau huyo

Mara kadhaa Sabaya kupitia kwa mawakili wake, Mahuna na Emmanuel Anthony, amekuwa akilalamikia kucheleweshwa usikilizwaji wa kesi hiyo na kuna wakati alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingia kati suala hilo.

Mnamo Aprili 5 mwaka huu, mahakama ilitoa uamuzi wa Lengai Ole Sabaya kulipa kiasi cha shilingi milioni 5 kama fidia kwa mwathirika na hapaswi kufanya kosa lolote la jinai kwa muda wa mwaka mmoja.

Sabaya ambaye mapema asubuhi ya leo alifika kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Moshi, kabla uamuzi wa kuachiwa haujatangazwa, kupitia Kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 91 kifungu cha 1A, kesi yake ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022 ilifanyiwa marejeo kama upande wa mshtakiwa ulivyoomba.

Mawakili upande wa Jamhuri waliiomba mahakama kubadilisha mashtaka ya Lengai Ole Sabaya kutoka kuwa ya kesi ya Uhujumu Uchumi na kufungua kesi yenye Mashtaka ya Makosa ya Jinai baada ya Lengai Ole Sabaya kuomba kufanya mazungumzo nje ya mahakama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ombi hilo la Sabaya lilikubaliwa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha baada ya Mawakili wa Lengai Ole Sabaya kuridhia na kufutwa kwa kesi yake namba 2 ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2022.

Baada ya kuridhia hilo, kesi mpya aliyofunguliwa Sabaya ni kesi kesi ya Jinai Namba 31/2023 ambayo ndani yake kulikuwa na mashtaka mawili mapya dhidi yake, kosa la kwanza likiwa ni kuchukua madaraka ambayo siyo yake.

Sakata la Lengai Ole Sabaya huyo lilielezwa kuwa akiwa na wenzake mnamo Januari 19, 2021 katika eneo la Masama Mbosho wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, bila kibali walivamia duka la Alex Evarest SwaI na kuchukua mali na kuzizuia na kujipatia kiasi cha fedha shilingi milioni 50.

Kosa la pili ni kuzuia upatikanaji wa haki ambapo Januari 19, 2021 katika maeneo tofautitofauti katika Wilaya ya Hai na Tulia jijini Arusha na maeneo tofauti ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama za kumfanya Alex Swai kuwa ametenda kosa la kukwepa kodi.

Baada ya kusomewa mashtaka, Sabaya alikiri kufanya makosa yote hayo mawili mbele ya hakimu Salome Mshasha.

Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, walikuwa wakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Shitaka la kwanza ilielezwa kwamba Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni, Arusha, washtakiwa hao waliiba Sh2.769 milioni, mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, washtakiwa waliwashambulia Numan Jasin, Harijin Saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga kwa kutumia bunduki, ili kufanikisha wizi huo.

Katika shtaka la pili, Sabaya na wenzake walidaiwa kuiba Sh390,000 kutoka kwa diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi wakiwa katika Mtaa wa Bondeni.

Shitaka la tatu lililokuwa linawakabili Sabaya na wenzake ni la kuiba Sh35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno kutoka kwa Ramadhan Rashid wakiwa katika mtaa huohuo.

Ole Sabaya ni miongoni mwa wanasiasa vijana waliokuwa na nguvu wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano , marehemu John Pombe Magufuli.

Baada ya kuwa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa vijana wa Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi, (UVCCM) Arusha, kwa muda kuingia kwake kwenye nafasi ya Wilaya ilimtambulisha zaidi.

Nguvu zake kubwa zilionekana baada ya Rais Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Julai 28, 2021, akionekana kuendesha operesheni mbalimbali ambazo baadhi zilionekana kulalamikiwa na watu.

Mara kadhaa kwenye utendaji wake, alikuwa anaeleza anachokifanya ni maelekezo kutoka juu bila kutoa ushahidi, hata kama masuala hayo aliyokuwa akiyafanya yalionekana kwenda kinyume na sheria.

0 Comments:

Post a Comment