Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanzisha mradi wa BOOST ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ya Awali na Msingi hapa nchini, ambapo itajenga na kukarabati miundombinu ya shule za awali na msingi.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
imepokea jumla ya Shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa 48, shule mpya mbili pamoja na matundu ya vyoo 30.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
ya Moshi Kastori Msigala, ameyasema hayo Aprili Mosi, 2023 wakati wa ziara yake
ya kutembelea, kuona na kuangalia maeneo ambayo yatakwenda kujengwa shule mpya
kupitia banjeti ya 2023-2024.
Aliongeza, “Nyingi ya shule hizi
zilizojengwa miaka ya 40 miundombinu yake kwa sasa ni chakavu kiasi cha kwamba
hazina mazingira rafiki kwa matumizi; ziko zinazohitaji ukarabati mkubwa na
zingine ni za kuvunja na kujengwa upya”.
Msigala aliendelea kusema kuwa moja wapo ya shule ambazo zitanufaika na mradi huo ni shule ya msingi Matemboni ambapo alisema katika bajeti ya mwaka 2023/204 jumla ya shilingi milioni 60 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili, jengo la utawala na matundu ya vyoo vinane.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Gaudence Assey, alisema zaidi ya shule za
msingi 190 ambazo ni mali ya serikali wilayani humo ni chakavu, zinatakiwa
kubomolewa na kujengwa upya, zingine zikihitaji ukarabati mkubwa.
"Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
ina jumla ya shule za Msingi 229 ambazo ni za serikali na kati ya hizo shule
190 zina uchakavu mkubwa ambazo zilijengwa toka miaka ya 1940 ambazo kwa sasa
zinahitaji kuvunjwa kutokana na miundombinu yake kuwa
chakavu,"alisema.
Pia afisa elimu huyo alisema zipo
shule za msingi 98 zenye uchakavu mkubwa wa vyoo vya wanafunzi ambavyo
vimejengwa juu ya shimo na hivyo kuhitajika kujengwa upya.
Awali Kaimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Matemboni Sofia Lyatuu, alisema yako madarasa matatu hayatumiki kwa
miaka 10 waliyafunga kutokana na kuta zake kupasuka na kuhofia kuleta madhara
kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla na kuiomba serikali kuyavunja.
Mbali na hayo Kastori alisema serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia ambapo katika halmashauri ya Moshi kwa mwaka 2022-2023 ilipokea shilingi milioni 340 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya ya madarasa 12 kwenye shule za msingi Kilolotoni, Kochakindo, Mieresini, Ngangu, Mruwia, Kyaseni, Fumvuhu, Kisuluni na Maendeleo, pamoja na kujenga matundu ya vyoo 82 yenye thamani ya shilingi milioni 113. 4.
0 Comments:
Post a Comment