Saturday, April 1, 2023

MIAKA 2 YA RAIS SAMIA SULUHU: Wilaya ya Mwanga kuondokana na changamoto ya Hospitali

 

Changamoto ya muda mrefu ya wakazi wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu inakaribia kufikia kikomo baada ya serikali kupeleka kiasi cha shilingi bilioni 2 kukamilisha ujenzi wa hospitali.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mwajuma Nasombe, aliyasema hayo Machi 30,2023  wakati wa utoaji wa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani Rais Samia Suluhu Hassan.

Nasombe alisema moja ya mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani Rais Samia ni ujenzi wa Hospitali mpya ya kisasa ya Wilaya ambayo inaendelea kujengwa katika ukanda wa tambarare ambapo hadi kukamilika kwake kiasi cha shilingi bilioni 3 kitatumika.

“Ujenzi wa hospitali hii tayari umekwisha kuanza, serikali imeshatupatia kiasi cha shilingi  bilioni mbili  na kwamba hadi kukamilika kwa ujenzi huo inakadiriwa kutumia shilingi  bilioni tatu,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dk. Salehe Mkwizu, kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo itakwenda kuondoa adha ya wananchi waliokuwa wanalazimika kuwapeleka wagonjwa wao  kwenye hospitali ya wilaya  iliyoko maeneo ya milimani Usangi.

“Mgonjwa alikuwa akitolewa Kifaru na kupelekwa Usangi na akifikishwa huko na kuonekana amezidiwa alikuwa anapewa rufaa ya kwenda KCMC  na  Mawenzi hali ambayo ilikuwa inawapa usumbufu na gharama mkubwa wananchi,”amesema Dk.Mkwizu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha nyingi ndani ya wilaya hiyo ambazo zimeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa, ikiwemo miradi ya kimkakati kama ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya.

“Ujenzi wa hospitali hii utawasaidia wananchi wa ukanda wa tambarare  ambao walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 22 kwenda katika hospitali ya wilaya iliyoko ukanda wa milimani kata ya Usangi,amesema Mwaipaya.

Mbali na kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya hospitali, Nasombe alisema halmashauri hiyo pia imepokea kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Utawala ambapo toka nchi ipate Uhuru mwaka 61 wilaya hiyo haikuwahi kuwa na ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na kwamba hadi kukamilika kwake litagharimu kiasi cha shilingi bilioni tatu.

Aidha alisema ndani ya kipindi hicho halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imepokea kiasi cha shilingi bilioni 3.4 za ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ununuzi wa vifaa tiba, pamoja na maboresho yake.

Alisema ndani ya miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya rais Samia, halmashauri hiyo imetoa kiasi cha shilingi milioni 900 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikindi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi.

“Huko nyuma takribani miaka mitatu halmashauri ya wilaya ya Mwanga haijawahi kupokea ajira mpya, ndani ya miaka miwili ya Rais Samia halmashauri hiyo imepokea ajira mpya 105, pamoja na kupandisha vyeo na madaraja kwa wafanyakazi  wapatao 250.




 


0 Comments:

Post a Comment