Halmashauri ya Wilaya ya Moshi katika bajeti yake ya 2023/2024 imetenga kiasi cha shingi milioni 16 kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuchimba bwawa la samaki ambalo litatumika kama shamba darasa ili kukabiliana na uvuvi harama kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Filbert Shayo, kwenye Maadhimisho ya miaka 10 ya Ushirikiano wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Jiji la KIEL nchini Ujerumani yaliyofanyika katika viwanja vya mji mdogo wa Himo.
Amesema kutokana na uvuvi haramu ulioshamiri katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Halmashauri hiyo imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuchimba bwawa ambalo litatumika kama shamba darasa la wananchi kwenda kujifunza ili waweze kuanzisha mabwawa madogo madogo ya ufugaji wa samaki, ambapo kitoweo hicho kimeonekana kuhitaji katika zaidi katika jamii.
Akizungumzia miaka 10 ya ushirikiano kati ya halmashauri hiyo na Jiji la Kiel- nchini Ujerumani Shayo amesema yako mafanikio makubwa ambayo halmashauri hiyo imeweza kunufaika nayo hususan katika nyanja ya elimu, afya, maji na mazingira.
Kwa upande wake Makamu Meya wa mji mdogo wa Himo Richard Njau, amesema mahitaji ya ulaji wa samaki yameongezeka ukilinganisha na upatikanaji wa kitoweo hicho kuwa kubwa.
Naye Mwenyekiti wa mji mdogo wa Himo Robert Karisti amesema mahitaji ya ulaji wa samaki katika mji wa himo ni makubwa hivyo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Moshi kwa kuja na wazo la kuchimba bwawa la samaki kwenye eneo hilo.
Mwaka 2013 Jiji la KIEL-Ujerumani na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi walianzisha Mahusiano na kuingia Mkataba wa Kwanza wa Ushirikiano katika kutembeleana na kupanga mipango mbalimbali ya Maendeleo hususani kwenye sekta za Afya, Elimu na Usafi na Mazingira.
0 Comments:
Post a Comment