Tuesday, March 21, 2023

Hospitali ya Kibong’oto yawatoa hofu wananchi kusambaa kwa vimelea kutoka maabara ya kisasa

 

Mitambo maalum katika maabara mpya ya kisasa katika Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, Siha mkoani Kilimanjaro


Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, Siha mkoani Kilimanjaro imewatoa hofu wananchi wanaozunguka maabara mpya ya kisasa iliyojengwa kwa ajili ya uchunguzi wa vimelea vya magonjwa ambukizi baada ya sintofahamu kuibuka ya uwezekano wa kusambaa kwa vimelea hivyo kwenye makazi ya watu.

Akizungumza hivi karibuni na wajumbe wa Serikali wa Kijiji cha Mae, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ibaeny pamoja na viongozi wa dini waliotembelea  maabara hiyo  Dk. Bingwa na mtafiti wa magonjwa ambukizi Peter Mbelele aliwahakikishia viongozi hao kwamba mitambo iliyowekezwa kwenye maabara  hiyo hairuhusu  vimelea kutoka nje ya jengo hilo na kwenda kwenye makazi ya watu kwenda kuwaambukiza.

Dk. Mbelele alisema serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 12.5 kwa ajili ya kujenga maabara hiyo lakini pia imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kununua mitambo iliyofungwa kwenye jengo hilo.

"Kukamilika kwa Maabara ya Afya ya Jamii ngazi ya 3 ya usalama iliyoko kwenye hospitali maalumu ya magonjwa Ambukizi-Kibong'oto Itachangia katika udhibiti wa kusambaa kwa mgonjwa duniani na hivyo kuimarisha uchumi na usalama wa binadamu,"alisema Dk. Mbelele

Aidha, Dk. Mbelele alisema maabara hiyo itafanya ufutiliaji wa usugu wa vimelea kwa dawa zinazotumika kwenye matibabu ya magonjwa mbalimbali na kufanya tathimini ya kiwango cha dawa mwilini.

Kwa upande wa utafiti Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa maabara hiyo itafanya pia tafiti mbalimbali na ubunifu (innovation) katika sayansi ya tiba na kinga katika ugunduzi wa Dawa, Vitendanishi, Vifaa tiba pamoja na kutengeneza chanjo mbalimbali za kuzuia na kukinga magonjwa ambukizi.

Pia aliongeza Hospitali ya Kibong’oto itatunza vimelea vya magonjwa mbalimbali ikiwemo vinasaba vya vimelea mbalimbali Kutoa mafunzo ya kiuchunguzi na ubunifu kwa wataalamu mbalimbali katika sekta ya Afya.

Hata hivyo alisema maabara hiyo inatarajia kuboresha huduma za tiba, kupunguza gharama ambazo Serikali inaingia katika kupeleka sampuli nje ya nchi kwa uchunguzi.

Kwa upande wake Meneja wa Maabara ya Afya ya Jamii Kibong’oto Dk. Shaban Mziray, aliwatoa hofu viongozi hao kwamba mitambo na vifaa vilivyowekwa katika jengo hilo iko kwenye uangalizi wa halai ya juu.

“Usalama wa miundo mbinu ya maabara imeimarishwa ili kuthibiti upotevu vimelea, ambapo kuna mitambo ya Sisteam camera pamoja na walinzi kutoka kampuni binafsi,” alisema Dk. Mziray. 

Dk. Mziray alisema uwepo wa teknolojia  za kisasa zaidi kwenye.kifua kikuu imesaidia kubainisha aina ya kifua kikuu, kimelea cha kifua kikuu, pamoja na usugu wake wa dawa.

Diwani wa Kata ya Ivaeny Elinisaa Kileo aliushukuru uongozi wa hospitali  hiyo kwa kuweza kuwapokea na kuweza kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika kata yake, amemshukuru mtafuti kwa  kuwatoa hofu wananchi kwamba hakuna madhara yeyote ambayo yanaweza kutokea kwa wananchi walio karibu na maabara hiyo kuambukizwa na vimelea.

Katibu wa CCM Kata ya Ivaeny Reuben Munuo na mwenyekiti wa kitongoji Grace Mmari, wamemshukuru Rais samia kwa kufanikisha ujenzi wa maabara hiyo kwani itakwenda kusaidia watanzania wengi.

Aidha Mchungaji Osca Tarimo na Lameck Kileo, walimshukuru Diwani wa kata hiyo kwa kuwaandalia ziara ya mafunzo kwa ajili ya uwekezaji uliofanywa na serikali ndani ya wilaya ya siha.

Hospitali ya Kibong’oto ina jukumu la kutoa huduma za Afya ya jamii na ufuatiliaji wa magonjwa yote yenye umuhimu katika jamii yaliyoaninishwa na Shirika la afya Duniani (WHO) na yale ya mlipuko.





0 Comments:

Post a Comment