Saturday, March 4, 2023

Waziri Mkuu Mstaafu Msuya aonya uharibifu wa mazingira

Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya ameonya kuwa iwapo hatua kali hazitachukuliwa wilaya ya Mwanga huenda ikawa jangwa kutokana na kasi ya ukataji miti unaoendelea wilayani humo.

Msuya alitoa tahadhari hiyo juzi, katika hotuba iliyotolwa kwa niaba yake na Balozi Fadhili Mmbaga wakati wa uzinduzi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa misitu pamoja na masuala ya kilimo hai Mwanga Environment Guard And Agricultural Development (MEGAD) hafla iliyofanyika katika kijiji cha Msewa kata ya Usangi wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

“Ukataji wa miti kwenye maeneo ya misitu ya hifadhi unaendelea kwa kasi ya ajabu; mito iliyokuwa ikitiririsha maji mwaka mzima kwa sasa mingi imekauka na iliyobakia inatiririsha maji machache sana na yote haya ni kutokana na uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanyika kila siku”, alisema Waziri mstaafu Msuya.

Aliongeza, “Wataalam wanatueleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri maeneo mengi hapa nchini hivyo kunahitajika juhudi kubwa katika kupanda miti, kutunza iliyoko kwa kuhakikihsa haiharibiwi tena”.

Mzee Msuya aliendelea kusema kuwa uwepo wa shughuli za kibinadamu kwenye misitu ya hifadhi kinyume cha Sheria na Kanuni kumepelekea pia kuathiri ukuaji na hata maangamizi ya viumbe hai vilivyoko kwenye hifadhi za misitu.

“Watu wanaachwa wakiendelea kulima mpaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kinyume chaSheria  na Kanuni zinazolinda mazingira, kwa hali hii hatutabaki na kitu zaidi ya jangwa”, alionya Mzee Msuya.

Alitoa wito kwa uongozi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA) kuwa kitovu katika maswala yanayohusu uhifadhi wa mazingira na viumbe hai vivyoko kwenye hifadhi ya milima ya Tao Mashariki eneo la Mwanga.

“Ni vyema mkajikita hapa na kufanya tafiti za hali ya juu zitakazo tambulikana ndani na nje ya nchi ya Tanzania na hivyo kuchangia uhifadhi wa mazingira eneo la milima ya Tao la Mashariki”, alisema.

Aliongeza kuwa“Ni vyema mkafanya tafiti zitakazowezesha kubaini miti na viumbe hai vilivyoko kwenye milima ya Tao la Mashariki na kuvitangaza jambao ambalo litapelekea maboresho katika uhifadhi wa eneo hilo kupitia wadau mbalimbali”, alishauri.

Akiongea wakati wa shughuli hiyo Mkuu wa Chuo cha Mweka Prof. Jafari Kadeghesho, alisema tayari wametembelea eneo hilo ili kuangalia maswala ya uhifadhi ya bayoniwai, aina ya mimea iliyoko na wanyama pori walioko eneo hilo.

Naye Mshauri wa taasisi hiyo ya (MEGAD) Balozi Fadhili Mmbaga alisema kuna hatari kubwa kwa miaka mitano ijayo kama serikali ya wialaya hiyo haitaweza nguvu kubwa za kuzuia ukataji wamiti , watu wanaoishi maeneo ya milimani kuanzakuyahama  makazi yao kutokana na ukame utakaosababishwa na  kukoswa maji.

Naye mlazi wa taasisi hiyo Profesa Yunis Mgaya, alisema maeneo ya ukanda wa milimani hususan kata ya usangi ilikuwa ikipata mvua kwa mwaka misimu mitatu lakini kwa sasa hivi mvua zimepungua na hivyo kusababisha kilimo kupungua .

Katika mahubiri yake Askofu mstaafu wa Jimbo la Same Jacob Venance Koola alisema Mungu aliwakabidhi wanadamu ardhi, miti, milima na mazingira mazuri, ili wayatunze lakini watu hao, wamekengeuka na kuikata miti hiyo kwa ajili ya kupata kuni , mbao na mkaa.

“Watu wanatakiwa kumrudia Mungu na kukiri kwamba wameharibu mazingira na kuanza kuotesha upya miti kwani Mungu ni mwenye huruma na msamaha atawasamehe na baala ukame, njaa litakwenda kutoweka.

Akizindua taasisi hiyo Kamishina wa Uhifadhi wa Misitu Nchini (TFS) Prof. Dos Santos Silayo, alitoa wito kwa wananchi kubuni aina ya biashara ambazo ni endelevu ambapo alisema zitawaepusha kuingia misituni kwa ajili ya kukata miti ili kujipatia kipato.

“Ni vyema wakabuni njia za kibiashara ambazo zitakuwa ni endelevu na ambazo zinaweza kuwapatia mapato bila kuharibu mazingira”, alisema.

Aidha Prof. Dos Santos  Silayo, alisema kuwa asilimia 73 ya misitu duniani ikiwemo hapa nchini hupotea kutokana na watu kukata miti ili kupata maeneo ya kilimo.
Kutoka kushoto Prof. Yunus Mgaya, Prof. Dos Santos Silayo, Prof. Jaffary Kideghesho,Balozi Fadhil Mmbaga, na Mhifadhi wa TFS Kanda ya Kaskazini Edward Shilogile wakiwa katika picha ya pamoja walipozuru nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya, Usangi-Mwanga.


0 Comments:

Post a Comment