Wednesday, March 22, 2023

KUELEKEA SIKU YA KIFUA KIKUU MACHI 26: Hospitali ya Kibong’oto kufanya usafi makaburi ya wahanga wa kifua kikuu, kutoa elimu Mererani

Gari tembezi la Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, ambalo mpaka sasa limewafikia watu 15,000 katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu, ambapo kwa kipindi cha miaka mitano kutoka Mwaka 2017 hadi Juni 2022 iliweza kuwafikia wachimbaji wa madini 8000 na kati yao 850 waligundulika kuwa na kifua kikuu na kuweza kuwaweka kwenye matibabu.


Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, inatarajiwa kufanya usafi katika makaburi ya wahanga wa kifua kikuu waliofariki na kuzikwa hospitalini hapo enzi za ugunduzi na majaribio ya dawa waliokuwa wakiletwa hospitalini hapo.

Akizungumza hivi karibuni na wajumbe wa Serikali wa Kijiji cha Mae, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ibaeny pamoja na viongozi wa dini waliotembelea hospitalini hapo kuelekea maadhimisho ya kimataifa ya kifua kikuu Daktari bingwa na mtafiti wa magonjwa ambukizi Peter Mbelele alisema kwa takribani miaka 60 tangu kugunduliwa kwa kimelea cha ugonjwa huo kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanapunguza uwezekano wa kusambaa zaidi kwa kifua kikuu.

“Wagonjwa wa kifua kikuu walikuwa wanatengwa na kuletwa hapa kibong’oto takribani miaka 60 tangu kugunduliwa kimelea cha kifua kikuu toka mwaka 1882 na mwaka 1943 ndipo kuligundulika kwa dawa ya kifua kikuu,” alisema Dk. Mbelele.

Dk. Mbelele alisema tangu kuanza kwa Hopsitali ya Kibong’oto mnamo mwaka 1926 wahanga wa ungonjwa huo walikuwa wakiletwa hapo na waliofariki walizikwa katika eneo lililotengwa hospitalini hapo ambayo sasa imekuwa sehemu ya historia.

“Mwaka 1926 ilipoanza kibong’oto ilianza kwa majaribio ya kifua kikuu katika kuadhimisha siku ya kifua kikuu Machi 26 kibongo’oto ina sehemu ya kihistoria ambako wahanga wa ugonjwa wa kifua kikuu waliokuwa wakiletwa hapa kabla ya kugundulika kwa dawa hizo na wakati wa majaribio ya dawa wengine walikuwa wanafariki na waliokuwa wanafariki walikuwa wanazikwa hapa Kibong’oto,” aliongeza.

Hata hivyo Dk. Mbelele alisisitiza kuwa mwaka huu 2023 katika kuadhimisha siku ya kifua kikuu Machi 26 watumishi wa hospitali hiyo watafanya usafi katika makaburi hayo ya kihistoria.

“Hekari nane za makaburi ambapo miili ya watu wa ugonjwa waliofariki kwa ugonjwa wa kifua kikuu wamelazwa. Tutafanya usafi hapo,” alisema Dk. Mbelele.

Pia aliongeza kuwa watakwenda mkoani Manyara katika machimbo ya Tanzanite eneo la Mererani kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu Kifua Kikuu.

Hospitali ya Kibongo’oto inaongoza kwa nchi za kiafrika kwa kupunguza muda wa matibabu

Mwaka 2017 hadi Juni 2022 iliweza kuwafikia wachimbaji 8000 na kati yao 850 waligundulika kuwa na kifua kikuu na kuweza kuwaweka kwenye matibabu.

Watu 716 kati yao waligundulika kuwa na ugonjwa wa siko seli. Watu 15000 wamefikiwa kwa kutumia gari tembezi la Hospitali ya Kibong’oto.




0 Comments:

Post a Comment