Baraza la Jumuiya ya Wazazi (WAZAZI) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kimempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita kwa kazi nzuri ambayo imeboresha maisha ya Watanzania wengi ndani ya miaka miwili ya utawala wake.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa WAZAZI wilaya ya Hai Joseph Mselle, wakati wa kikao cha Baraza la Wazazi wilayani humo kilicholenga kujadili mpango mkakati wa Jumuiya hiyo kwa miaka mitano ijayo.
“Pamoja na maazimio tuliyopitisha yanayohusiana na ajenda maalum tuliyokuwa nayo ya kikao hiki, wajumbe wa kikao pia tuliazimia kumpongeza Rais Dk. Samia kwa kazi nzuri alizofanya ndani ya miaka miwili ya uongozi wake kwani mabadiliko mengi na yenye tija kwa taifa yanayotokana na utekelezaji wa ilani na serikali iliyoko chini ya uongozi wake yanaonekana”, alisema Mselle.
Alisema “Kwenye sekta ya elimu tumeshuhudia uboreshaji wa miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa shule mpya nyingi nchini kote; hali imewezesha wanafunzi wengi kupata nafasi ya kupata elimu kuanzia ile ya awali hadi elimu ya juu”, alisema.
Aidha Mselle alisema mafanikio mengine katika sekta hiyo ni uamuzi wa serikali ya awamu ya sita unaomuwezesha mwanafunzi wa kike aliekatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kupata ujauzito kurudi shuleni na kuendelea na masomo jambo ambalo alisema litawasaidia wanafunzi wengi wa kike kuendelea na ndoto zao pamoja na kupata ujauzito walipokuwa wakiendelea na masomo yao.
Mselle aliendelea kusema kuwa eneo lingine ni kwenye sekta ya afya ambapo kuongezwa kwa bajeti ya wizara ya afya chini ya uongozi wa Rais Samia kumewezesha huduma za afya kuboreshwa nchini na kuwaondolea wananchi kero nyingi walizokuwa wakikabiliana nazo wanapokwenda kufuata huduma za afya.
“Kwa upande wa miundombinu ya barabara tumeshuhudia bajeti ikiongezwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA pamoja na TANROADS, hali hii imepelekea barabara nyingi hapa nchini zikiwemo zile za vijijini, kuwa katika hali nzuri nyakati zote za mwaka jambo ambalo pia limechangia kukuza uchumi wa Taifa”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia pia imefanya kazi nzuri katika kutekeleza miradi ya kimkakati kama ule wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, ambalo kukamilika kwake kutachangia pamoja na mambo mengine, kushuka kwa bei ya umeme na hivyo kuwapa Watanzania wengi unafuu wa kimaisha.
0 Comments:
Post a Comment