Thursday, March 23, 2023

"Twenzetu Serengeti Kilimanjaro Watumishi wa Royal Tour" yazipeleka taasisi 10 za umma kutalii Serengeti

Watumishi wa taasisi mbalimbali za umma mkoani Kilimanjaro katika picha ya pamoja katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wakijiandaa kuondoka kwenda kufanya utalii wa ndani katika Mbuga ya Serengeti wakibeba kauli mbiu ya "Twenzetu Serengeti Kilimanjaro Watumishi wa Royal Tour" kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.  

Fahari ya Simba katika Hifadhi ya Serengeti


Taasisi 10 za umma mkoani Kilimanjaro zimepelekwa kutalii mbuga yenye maajabu makubwa duniani ya Serengeti ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha watanzania kufanya utalii wa ndani. 

Hatua hiyo inaelezwa na wadau wa utalii nchini kuwa ni hamasa waliyoipata kutoka kwa Rais wa Awamu ya sita Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili tangu alipopokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Dk. John Pombe Magufuli. 

Machi 23,2023 Serikali ya mkoa wa Kilimanjaro ilitoa baraka zote zote kwa watumishi hao kwenda Serengeti, kuitambulisha dunia juu ya mazuri yaliyofanywa na rais Samia tangu alipoingia madarakani Machi 19 mwaka 2021. 

Mbuga ya Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 30,000 ipo katika maajabu saba ya Afrika na ipo katika orodha ya maajabu kumi ya vivutio vya asili duniani. 

Zaidi ya watumishi 40  kutoka taasisi mbalimbali za umma mkoani Kilimanjaro, wameanza ziara yao ya kwenda kutembelea hifadhi ya taiafa Serengeti ambayo inatajwa kushika nafasi ya kwanza  kwenye ukusanyaji wa mapato ikifuatiwa na hifadhi ya mlima Kilimanjaro. 

Akiwaaga Watumishi hao Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dk.  Vedasto Makota, amesema Samia amefanya juhudi kubwa katika kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi, kitendo walichokifanya watumishi hao ni jitihada za kumuunga mkono rais Samia katika kuhamasisha utalii. 

"Ninyi kama watumishi wa umma mmejenga taswira njema kwa serikali yenu ya kuhamasisha utalii wa ndani, hivyo mtakaporudi tunatarajia mtakuwa mabolozi wazuri wa kuutanza utalii wetu,"amesema Dk. Makota. 

Amefafanua kuwa "Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  imejizolea umaarufu mkubwa duniani baada ya Simba mkongwe maarufu "Bob Junior" aliyeuawa na wanae ili kumaliza utawala wake duniani baada ya kuwa mfalme wa nyika akiongoza zaidi ya Simba 3000 walioko katika hifadhi hiyo,"amesema. 

Kwa upande wake Mratibu wa "Twenzetu Serengeti Kilimanjaro Watumishi wa Royal Tour" Rashid Ally Rashi amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia yako mafanikio makubwa aliyoyafanya ikiwemo kuondoa kodi kwenye bodi ya mikopo, pamoja na kupandisha madaraja kwa walimu. 

Akizungumza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Nicholas Francis, amesema kuwa Serikali imeweza kuwaongezea bajeti kwa asilimia 185 ambapo TARURA  ilikuwa ikipata shilingi bilioni 9.2 lakini katika bajeti ya  2022/2023 wameongezewa shilingi bilioni 33.19. 

Nao baadhi ya Watumishi wanaoshiriki ziara hiyo Exzaud Mtei, Julia's Kibwana na Basila Mmbaga, wamesema kwenye sekta ya elimu wameshuhudia uboreshaji wa miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa shule mpya nyingi nchini kote; hali ambayo imewezesha wanafunzi wengi kupata nafasi ya kupata elimu kuanzia ile ya awali hadi elimu ya juu. 

Aidha wamesema eneo lingine ni kwenye sekta ya utalii, kilimo na afya ambapo wamesema kuongezwa kwa bajeti kwenye sekta hizo chini ya uongozi wa Rais Samia kumewezesha huduma za kijamii kuboreshwa nchini. 

TANESCO, TARURA, MUWSA, POLISI, ARDHI, MALIASILI, ELIMU, AFYA ni miongoni mwa taasisi za umma zinashiriki ziara hiyo katika Mbuga ya Serengeti kwa udhamini wa Zara Tours. 








0 Comments:

Post a Comment