Mbunge wa viti maalum, kundi la
Wanawake mkoa wa Kilimanjaro Esther Maleko, ametoa taulo za kike kwa wanafunzi
wa shule ya sekondari ya wasichana ya Ashira, ili kuwawezesha kuhudhuria masomo
yao wakati wote bila ya kikwazo cha kukosa masomo.
Maleko alikabidhi taulo hizo za
kike katika kilele cha siku ya Wanawake duniani mnamo Machi 8,2023 ambapo alisema amelazimika kutoa taulo hizo za
kike ikiwa ni mkakati wake wa kutatua changamoto za taulo za kike kwa wanafunzi
kwani wengi wao wanatoka kwenye mazingira duni hali inayosababisha kushindwa
kumudu gharama za taulo hizo na hivyo
kukosa masomo.
Aidha Mbunge Maleko alikabidhi
kiasi cha shilingi milioni 1.6 kama ahadi yake aliyoitoa hivi karibu shuleni
hapo alipotembelea na kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ununuzi
wa madawati kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
"Leo nimekabidhi ahadi
yangu ya madawati niliyoiahidi shuleni hapo, msaada huouwa madawati ni sehemu
ya jitihada zangu katika kusaidia jamii ili kuwawezesha wanafunzi hawa waweze
kusoma kwa utulivu,"alisema Mbunge Maleko.
Akizungumza na wanafunzi hao
Maleko aliwataka watoto wa kike kujiwekea malengo ya kusoma kwa bidii ili
kupata maarifa yatakayolisaidia taifa na wao wenyewe kupata maendeleo huku
akiwaasa kujiepusha na vishawishi na mahusiano kabla ya wakati muafaka ili wasikatishe
ndoto zao kwa kupata mimba za utotoni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) Wilaya ya Moshi Rwaichi Kaale,
alimpongeza Mbunge Maleko kwa kutimiza
ahadi yake aliyoitoa shuleni hapo huku akitoa wito kwa wanafunzi hao kujichunga
ili waweze kutimiza ndoto zao za kimasomo.
Naye Mkuu wa shule hiyo Elizabeth
Abdallah, alishukuru kwa msaada huo wa madawati ambayo yatawasaidia watoto
kusoma kwa utulivu huku akitoa wito kwa wadau wengine kuguswa na kuisaidia
shule hiyo.
Wakizungumza baadhi ya wa
wanafunzi waliopatiwa taulo hizo za kike wanaosoma kidato cha tano katika shule
ya sekondari ya wasichana Ashira Zainabu Bomba, Faraja Jackson, Magreth Lugano, walimshukuru Mbunge Maleko kwa
msaada huo wa taulo za kike kwani hedhi
inakuwa ikisababisha baadhi yao kukosa masomo kwa sababu ya kukosa taulo za
kuvaa.
0 Comments:
Post a Comment