Monday, May 1, 2023

Mlemavu abakwa atiwa ujauzito Moshi Vijijini

Binti wa miaka 19 mwenye mtindio wa ubongo tangu kuzaliwa kwake amebakwa na kutiwa ujauzito na kijana (jina tunalo) ambaye ni baba wa watoto wawili.

Ametendewa ukatili huo katika kitongoji cha Machombo, kijiji cha Mnini kilichopo Kata ya Uru Mashariki wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Hadi taarifa hii inaandikwa binti huyo ana ujauzito wa miezi sita huku mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji wa unyanyasaji wa kijinsia na wenye ulemavu zikikaa kimya.

Binti huyo anayefahamika kwa jina la Flora Hilary Kwayu ni mwenye ulemavu tangu kuzaliwa kwake kwa wazazi Mzee Hilary na mama Elnina Kwayu.

Akizungumza na JAIZMELA, mama wa binti huyo mwenye watoto wanane (8)  anasema binti yake alizaliwa tarehe 29/3/2003 na kusoma shule ya msingi Mnini  ambapo kwa sasa hadi kutendewa ukatili huo alikuwa akisoma katika Shule ya Mazoezi ya Patandi-Tengeru iliyopo mkoani Arusha.

Mama Flora anasema mtoto wake alifanyiwa ukatili wakati akiwa likizo na alitambua kuwa mtoto wake yu taabani baada ya kupigiwa simu na uongozi wa Shule ya Mazoezi ya Patandi ambako amekuwa huko kwa mwaka wa tatu sasa ambapo walimtaka aende shuleni kwa ajili ya kumwona binti yake.

“Siku hiyo nilipigiwa simu kutoka shuleni wakinitaka niende nikamwone motto, hawakutaka kunifahamisha nini ambacho kimemtokea, nilienda haraka kujua nini kimemkuta mwanangu,” anasema Mama Flora.

Anasimulia mama huyo aliyezaliwa mnamo mwaka 1962 kuwa alipofika shuleni Patandi alielezwa kuhusu hali ya mtoto na siku hiyo hiyo alirudi naye nyumbani Machombo ambako binti huyo alitoa maelezo ya mhusika aliyemfanyia kityendo hicho na alienda mbali zaidi kwa kwenda kumwonyesha mama yake alikofanyiwa ukatili huo.

Mama Flora anasema alikaa na wana familia na kuamua kulipekea suala hilo Polisi Majengo mjini Moshi na kupewa RB Na. MAJ/RB/541/2023 iliyogongwa na Chumba cha Mashtaka Kituo cha Polisi Majengo.

“Machozi yalinitoka kwa unyama aliofanyiwa motto wangu, ikanibidi nikae na wanafamilia kujadili suala hili; tukaamua twende kituo cha polisi Majengo natukapewa RB,” anasema mama huyo.

Aidha Mama Flora mwenye watoto wa kike watano na wakiume watatu anasema Polisi walifika Machombo na kumkamata mtuhumiwa ambaye kwa sasa yupo nje huko mama huyo akipigwa danadana kuhusu suala hilo kuhusu tarehe ya kupanda mahakamani ili kuanza kuunguruma kwa kesi hiyo.

Mama Flora ameendelea kufuatilia ambapo vielelezo mbalimbali ameshavipeleka kituo cha polisi ikiwamop kipimo cha ultra sound na uthibitisho wa mtoto wake  mwenye mtindio wa ubongo kutoka CCBRT; File No. FB 24-CCBRT

“Nasikitika kuona Polisi wanalizungusha suala hili, huku mtuhumiwa tunamfahamu, hakuna suala la kwenda mahakama, ukiwauliza wanakwambia uplelezi haujakamilika; tunaona kama kuna kitu kinafanyika hapa haki yetu isipatikane,” anasisitiza mama Flora.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku upelelezi ukiendelea kwa ajili ya hatua zaidi.

Awali katika maelezo ya Mama Flora anasema binti yake alimficha mama yake baada ya kufanyiwa ukatili na baba huyo mwenye watoto wawili mwishoni mwa mwaka 2022 kwani alitishiwa na mtuhumiwa (jina tunalo) kwamba angetoa siri hiyo angemkata koromeo.

Siku ya tukio Flora alikwenda dukani kununua soda baada ya kupewa fedha na baba yake Mzee Hilaryhivyo wakati wa kurudi alikutana na mtuhumiwa ambaye akiwa na panga kiuno alimlazimisha kuingia katika pagale (nyumba isiyokaliwa na watu)ambako alimbaka na kumtia ujauzito.

Kaka wa binti huyo aliyetambulisha kwa jina la Antonioanasema anachokihitaji ni haki itendekena mtuhumiwa apelekwe mahakama kwani mpaka sasa wa kama familia wanao kuna mahali panapindishwa katika utekelezaji wa jambo hili ili kuficha ukweli.

Baba wa binti huyo Mzee Hillary anasema awali alifichwa kuhusu kilichomkuta binti na alipojua walikuwa tayari wameshalifikisha katika ngazi za uongozi ikiwamo polisi.

Mzee Hillary anasema angejua mapema   angeenda kumtoa roho mtuhumiwana yeye kuishia jela kwani kitendo alichokifika ni cha simanzi na hasira.

Hadi sasa Flora haendi tena shule kutokana na ujauzito kuwa mkubwa, anakaa tu nyumbani na dada yake kwa ajili ya ulinzi kutokana na hofu iliyotanda baada ya kufanyiwa ukatili huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Machombo Valentine Gabriel Massawe anasema matukio kama hayo katika kijiji hicho yamekuwa yakitokea lakini mpaka sasa ana taarifa za binti huyo kutendewa ukatili huo na kuongeza kuwa tamaa na ushirikina vimekuwa ni sababu kubwa ya wenye ulemavu kutendewa ukatili.

0 Comments:

Post a Comment