Thursday, May 4, 2023

Luhemeja ataka Tathmini ya kina Makandarasi Miradi ya Maji



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akikagua nyaraka za mradi wakati wa ziara yake wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro Mei 2, 2023.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa Wizara hiyo itaanza kuwafanyia tathimini ya kina Wakandarasi wote wanaotuma maomi ya kutekeleza miradi inayohusiana na Wizara hiyo ili kuepuka ucheleweshaji wa utekelezeji wa miradi hiyo. 

Mhandisi Luhemeja aliyasema hayo jana mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro wakati wa kikao kazi cha kujadili maendeleo ya mradi mkubwa wa maji wa kimkakati wa Same-Mwanga-Korogwe, kilichofanyika ofisi za (MUWSA) Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

 

“Tathmini hizo zitakuwa zinalenga kuhakikisha miradi ya maji inayotokelezwa hapa nchini inakamilika kwa muda uliowekwa kwa mujibu wa mikataba inayohusiana na miradi hiyo na pia iwe imetekelezwa kwa ubora”, alisema.

 

“Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji halafu wananchi wanakosa maji hayo kwa muda mrefu huku waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi hiyo wakisusua na kutoa visingizio visivyo vya kuridhisha”, alisema.

  

Alisema kuwa Wizara hiyo pia itaanza mpango wa kufanya tathmini ya kila mwezi kwa kila mradi wa maji unaotekelezwa ili kufuatilia kwa karibu mienendo ya utekelezaji wa miradi hiyo jambo ambalo alisema litasaidia utekelezaji wake kuwa wa ubora na kukamilika kwa wakati.

 

“Jicho la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan liko kwenye miradi ya maji inayotekelezwa hapa nchini ukiwemo huu wa Same-Mwanga-Korogwe, hivyo sisi kama Wizara hatutalala usingizi ili kuhakikisha inatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma za maji kama wanavyotarajia”, alisema.

 

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Same-Mwanga-Korogwe, Mhandisi wa maji kutoka Wizara hiyo Mhandisi Pyarali alisema kuwa utakapokamilika unatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wananchi 456,931 ifikapo mwaka wa 2038.

 

Aliongeza, “Awamu hii pia itahuisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika vijiji vya Ruvu Mferejini na Ruvu Jiungeni vilivyoko wilaya ya Same na vijiji saba vya Handeni, Lang’ata Bora, Lang’ata Kagongo, Nyabinda, Kiti cha Mungu, Njia Panda na Kirya, vilivyoko wilaya ya Mwanga”.

 

Aidha alisema awamu ya pili ya mradi huo itahusisha ujenzi wa miundombinu katika vijiji 24, ambapo kati ya hivyo 14 viko mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Same, 10 Wilaya ya Mwanga (Kilimanjaro) na vijiji tano viko katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

 

Alisema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yenye urefu wa kilometa 566.






0 Comments:

Post a Comment