Thursday, May 4, 2023

TaTEDO, SESCOM zatoa mafunzo mawakala wa Jiko la Umeme lenye Presha

Majiko ya Umeme yenye presha.

TAASISI ya kuendeleza Nishati asili Tanzania (TaTEDO) kwa kushirikiana na Kampuni ya SESCOM zimetoa mafunzo kwa mawakala wa jiko la umeme lenye presha (JULEP), ili kuihamasisha jamii kutumia jiko hilo na kuondoikana na utumiaji wa nishati ya kuni na mkaa.

Hayo yalisemwa jana Mei 3,2023 na Mkurugenzi mtendaji wa TaTEDO Estomiah Sawe, wakati akizungumza na Mawakala wa jiko la umeme lenye presha JULEP ambalo hutumia presha na mvuke kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwenye ufunguzi wa warsha ya siku tatu iliyofanyika mjini Moshi mkoani humo.

Kwa mujibu wa Sawe alisema takwimu za mwaka 2020, watanzania 100 wanapoteza maisha kila siku kwa kutumia kuni na mkaa,  utumiaji wa jiko hilo utakwenda kuokoa afya za watanzania hususan akina mama na watoto ambao hutumia kuni na mkaa kupikia chakula jambo ambalo limesababisha mazingira na misitu kupotea kila siku.

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya watanzania wanatumia kuni na mkaa kupika na katika kutumia nishati hiyo ya kuni na mkaa kila mwaka watanzania zaidi ya 33, 000 wanapoteza maisha.

“Ili kuwasaidia watanzania wanaopoteza maisha kwa kutumia kuni na mkaa waweze kupungua TaTEDO-SESO na Kampuni ya SESCOM tumetoa mafunzo kwa mawakala wa jiko la umeme lenye presha JULEP, ili kuhamasisha jamii iweze kutumia jiko hilo ili kuokoa mazingira na misitu ambayo inaendelea kupotea kila siku,”alisema.

Alisema watanzania ambao wanatumia majiko ya JULEP wako 600 kwa nchi nzima, ambapo kampuni hiyo kwa  mwaka 2023 imeweka malengo ya kuuza majiko ya JULEP 10,000 ifikapo desemba mwaka huu.

“Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ina jumla ya Watanzania milioni 60 ambao ni  sawa na kaya milioni 12 na kati ya hizo asilimia 40 ya kawa hizo zinatumia umeme,”alisema.

Alisema “Ili kuzifikia kaya milioni tano zitakazo kuwa zikitumia majiko hayo itatuchukua miaka mingi, hivyo lazima sisi kama mawakala, kama kampuni tukazane kuuza majiko haya, kutoka kwenye lengo la kuuza majiko 10,000 kwa mwezi tujitahidi kuuza majiko 20,000 kwa mwezi ili kuzifikia kaya milioni tano zenye umeme waweze kutumia majiko haya,”alkisema Sawe.

Kwa upande wake Afisa miradi  wa TaTEDO Jensen Shuma, alisema nia ya Taasisi hiyo kuendesha mafunzo hayo kwa maewakala hao ni kuhakikisha Watanzania kote nchini waweze kutumia Nishati safi za kupikia na kuondokana na athari ambazo zimekuwa zikiwaathiri akina mama na watoto wakati wanapopika jikoni kwa kutumia kuni na mkaa.

Naye Mratibu wa miradi na Biashara Kampuni ya SESCOM Abina Minja, alisema  warsha ya mawakala wa jiko la umeme lenye presha (JULEP) imelenga kupata mawakala wengi ambao watasambaza majiko hayo, ili kuwafikia watanzania wengi  zaidi hususan waishia vijijini.






0 Comments:

Post a Comment