UMOJA wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, wameahidi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura nyingi uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Aidha Wajumbe hao wamewataka wale wote wenye nia ya kugombea nafasi ya Urais mwaka 2025 wapishe kwanza kwa sasa kwani mgombea waliyenaye ni Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa Mei 03,2023 na Mwenyekiti wa (UWT) Wilaya ya Moshi Vijijini Ruwaichi Kaale, wakati akizungumza na Wajumbe wa UWT Kata ya NjiaPanda, ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kuwashukuru wanachama hao kwa kumchagua kushika nafasi hiyo.
“Pamoja na kwamba kipindi cha mwaka 2021 Rais Samia aliingia kwenye nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi wa mwaka 2025, Rais Samia ataingia kwa kupata kura nyingi kwa kazi alizozifanya kwenye taifa la Tanzania,”alisema Kaale.
Amesema "Rais Samia anapaswa kupongezwa kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kutumia ubunifu wake wa kupeleka fedha za nyingi za Uviko-19 kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu jambo ambalo limewezesha kuondoa msongamano kwa wanafunzi darasani.
"Sisi kama Umoja wa Wanawake Tanzania wilaya ya tumejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Rais Samia Suluhu Hassan atapata kura za kishindo kutokana na mambo makubwa aliyoelekeza ndani ya wilaya yetu ya Moshi Vijijini, "amesema.
Amesema Wananchi wa kata ya Njiapanda, walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa Maji safi na Salama, hali ambayo ilikuwa inawalazimu akina mama hao kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kumtua mama ndoo kichwani, kata pekee ya Njiapanda ameleta fedha Sh. bilioni 2 ambazo zimewezesha kujenga mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda,".
Pia Mwenyekiti huyo aliwataka Wanawake hao wasijiweke nyuma, wasimame kidete katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024 kwani ni demokrasia na kila mtu anayo haki ya kuchukuwa fomu ya kugombea.
"Niwaombe akina mama wenzangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 utakapofika tujitokezeni kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini pia niwaombe wanawake walio mstari wa mbele kutetea haki za wanawake wenzetu jitokezeni kuwashawishi wanawake wenye uwezo wa kugombea nafasi za uongozi waweze kuchukua fomu,"amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Njiapanda Loveness Mfinanga, amesema kuwa ndani ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan yako mambo mengi ambayo ameyafanya ndani ya kata hiyo hususan kwenye sekta ya maji, afya na elimu.
"Kata ya Njiapanda ilikuwa na changamoto kubwa ya Maji safi na Salama, serikali ya awamu ya sita imetuletea Sh bilioni 2 za mradi wa maji Miwaleni-Njiapanda, Sh bilioni 1 za ujenzi wa kituo cha afya, imetupatia Sh molioni 387 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi,"alisema Loveness.
Naye Katibu wa UWT Wilaya ya Moshi Shakila Singano, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa watoto katika malezi bora ili kupunguza wimbi la watoto wa mtaani pamoja na kuzuia mmomonyoko wa maadili.
Wajumbe wa UWT kata ya Njiapanda, Moshi DC wakifuatilia jambo katika mkutano wao wa hivi karibuni |
0 Comments:
Post a Comment