Monday, May 22, 2023

Mgogoro wa shule, mwekezaji wazuia wanafunzi kuingia madarasani

 

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Masumbeni wakiwa katika viunga vya shule yao kabla ya kuzuia kuhudhuia masomo kutokana na mgogoro wa shule, kijiji, na mwekezaji.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Masumbeni iliyopo Kata ya Kifula wilayani Mwanga, Kilimanjaro wameshindwa kuhudhuria masomo katika vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa takribani siku 100 kutokana na mgogoro wa eneo baina ya shule, kijiji na mwekezaji.


Hayo yalijiri kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa halmashauri  ulioketi katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Mwanga, kwa ajili ya kujadili shughuli mbalimbali  za maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/23.


Akizungumza katika mkutano huo Diwani wa Lembeni Alex Mwaipopo aliwasilisha hoja yake binafsi ya kutaka kufahamu ni kwa namna gani serikali inasaidia ili eneo la shule linabaki kuwa mali ya shule hiyo.


“Kwa kipindi kirefu kumekuwepo na mgogoro hususani kwenye eneo la shule ya msingi Masumbeni iliyopo kata ya Kifula kumegwa na kupewa taasisi ya Islamic Development Foundation , mgogoro huu ambao serikali ya kijiji bila ya kuishirikisha shule, au halmashauri ya wilaya, kijiji kilimega eneo la shule kwa taasisi binafsi , taasisi hii ilipeleka shauri mahakamani na kushinda shauri hilo,” alisema Diwani Mwaipopo.


Diwani huyo aliongeza kuwa IDF ilipolipeleka shauri hilo mahakamani na kushinda, Mahakama Kuu iliikabidhi taasisi hiyo eneo ambalo ndani yake lina madarasa , myumba moja ya mwalimu.


Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Dina Ezekiel wa Shule ya Msingi Masumbeni aliyeitwa katika mkutano huo alisema, “Eneo hili ni mali ya shule limeporwa na watu wanaojiita ni IDF na mgogoro huu ulianza tangu mwaka 2014 , tulienda Mahakama ya Mwanzo Mwanga, na hukumu ikatoka tukawa tumeshinda kesi hiyo.”


Mwalimu Mkuu huyo aliongeza kuwa mwekezaji huyo hakukata rufaa ya shauri hilo akaenda katika mahakama kuu mkoa wa Kilimanjaro na kufungua mashtaka mapya kuhusu eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuishtaki serikali ya kijiji.


“Serikali ya kijiji ndiyo waliohusika kumpa hilo eneo la shule kinyemela bila kuishirikisha kamati ya shule wala uongozi wa wowote. Mali zilizochukuliwa na mwekezaji huyo ni pamoja na vyumba viwili vya madarasa ya wanafunzi wa shule ya awali, nyumba ya mtumishi yenye vyumba vitatu na sebule,  miti , ofisi ya mwalimu,” alisema Mwalimu Mkuu.


Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga  Mwajuma Nasombe alikiri kuwepo kwa wanafunzi ambao wameshindwa kuingia madarasani kwa miezi mitatu baada ya kufungwa utepe na kusimamisha shughuli zote zilizokuwa zikifanyika katika eneo hilo ambalo taasisi ya IDF ililichukua.


“Watoto wa darasa la awali hawana madarasa ya kusomea kwa sababu mwekezaji huyo alifunga utepe, na ni marufuku kuingia eneo hilo, madarasa hayo…kwa sasa hayawezi kutumika, mali mbalimbali za shule ikiwemo miti, imechukuliwa, pamoja na nyumba ya mtumishi, imechukuliwa,” alisema Nasombe


Akitoa ufafanuzi wa kisheria, Mwanasheria wa Halmashauri hiyo Edwin Rusa alisema baada ya taarifa kupatikana kwa eneo la shule kumegwa shule walianza kufanya ufuatiliaji ambapo walizuia IDF kuingia katika eneo hilo.


“Ilipofika mwaka 2018 Taasisi ya Islamic Develompment Foundation ilipeleka shauri mahakama kuu ikiishtaki serikali ya kijiji pamoja na Bw. George Mfagavo na ilipofika mahakamani kwa bahati mbaya kijiji hakikuitaarifu halmashauri kwamba kuna kesi ambayo inaendelea mahakamani,” alisema mwanasheria huyo.


Aidha Rusa aliongeza kuwa mnamo mwaka 2019 mahakama ilitoa maamuzi kwamba eneo hilo ni mali ya IDF na baada ya halmashauri kupata taarifa hizo ilipeleka maombi mahakama kuu (objection proceeding)  na mahakama iliyakataa maombi hayo.


“Baada ya kuwa imekataa maombi hayo taasisi ya IDF ilipeleka maombi ya kutekeleza hukumu, ilipofika mwaka 2022 tulirudi tena mahakamani kama halmashauri tukapeleka maombi ya kupinga eneo hilo kukabidhiwa kwa taasisi hiyo, lakini kwa mara ya pili tena maombi yetu yakawa yameshindikana,” alifafanua mwanasheria huyo.


Hadi sasa haijajulikana ni lini zuio hilo litaondolewa ili wanafunzi waendelee na masomo yao kama kawaida katika shule ya Msingi Masumbeni.




0 Comments:

Post a Comment