Taasisi isiyo kuwa ya kiserikali ya Beta Charitable Trust ya nchini Uingereza kwa kushirikiana na Lions Club Tanzania, wametoa ufadhili wa huduma ya matibabu ya uchunguzi wa kupima macho bure kwa wazee 120 , lengo likiwa ni kuwawezesha watu wenye vipato vya chini kupata huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa Juni 1,2023 na Kiongozi Mkuu wa Lions Club Tanzania Mustansir Ghulam Hussein wakati wa akizungumza na wazee waliofika kutibiwa katika hospitali ya Kibosho, iliyoko Wilaya ya Moshi
Taasisi ya Beta Charitable Trust kwa kushirikiana na LionsClub Tanzania, imedhamiria kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi wenye matatizo ya mtoto wa jicho, hivyo wanashirikiana na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya Kibosho, ambapo zaidi ya wazee 120 watapatiwa matibabu bure ya upimaji wa macho pamoja na upasuaji.
Amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Mei 2023 zaidi ya watanzania 1,000 kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini wamepatiwa matibabu ya bure ya macho kupitia taasisi hiyo.
Aidha amesema katika mkoa wa Shinyanga wilaya ya Kahama taasisi hiyo iliweka kambi na kutoa huduma ya bure kwa wazee 333 wenye matatizo ya macho na kwamba wanatarajia kuweka kambi ya namna hiyo katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza ambako hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa takribani wazee 250 wamebainika kuwa na changamoto hiyo ya macho.
Kwa upande wake Katibu wa Lions Club Moshi Kibo Inderjeet Rahan ‘NITU’ ameushukuru uongozi wa hospitali ya Kibosho kwa kukubali kuwapokea wazee hao na kuweza kuwapatia matibabu hayo, huku pia akiishukuru taasisi ya Beta Charitable Trust, kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia matibabu hayo kwa wazee.
Awali akizungumza Daktari bingwa wa macho Christian Mlundwa kutoka hospitali ya Kibosho na Matroni wa hospitali hiyo Sister. Francis Okido wameishukuru taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kugharamia matibabu hayo kwa wazee.
Aidha wamesema wagonjwa wengi wanaofika kupata matibabu ya macho wengi wao wanasumbuliwa na tatizo la mtoto wa jicho, ambapo alishauri jamii hiyo kujenge utaratibu wa kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili wanapopatikana na tatizo watibiwe kwa mapema ili kuepuka changamoto kubwa zaidi ikiwemo upofu.
Wakizungumza baadhi ya wagonjwa wa macho waliofika kupata huduma hiyo, Michael Massawe Peter Oisso na Suzi Shayo, wameishukuru taasisi ya Beta Charitable Trust kwa kufadhili matibabu hayo na kusema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa linawasumbua wazee wengi.
0 Comments:
Post a Comment