Thursday, June 15, 2023

John Heche aichana Serikali sakata la bandari;

 Heche: Serikali ituambie ilikaa wapi na DP World

Kiongozi Mwandamizi wa Chadema John Heche akihutubia umati wa wakazi wa Moshi Mjini Juni 15, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Posta.


Sakata tata la bandari nchini limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Mbunge wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tarime Vijijini  kuitaka serikali ya awamu ya sita iwaeleze watanzania ni lini na wapi walikaa na wawekezaji wa DP World kuhusu bandari zilizopo nchini.


Sehemu kubwa ya wale wanaolijadili suala hilo wanaitupia macho bandari ya Dar es salaam ambayo licha ya kutoa huduma zake kwa sehemu kubwa ya Tanzania pia imekuwa kiunganishi muhimu kwa mataifa mengine kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda, Malawi, Burundi, Uganda na hata Zimbabwe


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Posta mjini Moshi leo Juni 15, 2023 Heche amesema watanzania wanapaswa kuelezwa kwa uwazi kuhusu mahali walipokaa na DP World kuhusu uwekezaji wa bandari za Tanganyika.


"Tunataka serikali ituambie na Rais atuambie huyu mwarabu wa DP World alipatikanaje, walikutana wapi, walikutana kwenye chai akamwambia mimi nina bandari njoo uchukue? walikutana wapi?"


Kiongozi huyo mwandamizi wa Chadema alisema katika mchakato mzima taratibu na kanuni hazijazingatiwa katika suala la mkataba wa Tanzania na DP World


"Kwasababu utaratibu wa serikali kwa mambo kama hayo yalipaswa kutangazwa...sheria ya manunuzi inasema lazima kuwepo na tangazo tenda shindanishi, kwamba  sisi bandari yetu ya Dar es Salaam au bandari nyingine kama mkataba unavyosema kila mmoja aje."


Heche alisisitiza kuwa swali hilo ni la msingi ambalo watanzania wanapaswa walijuaje na serikali iwaambie kwa ufasaha.


"Huyu mtu mliyempa bandari juzi mmempataje mmejuaje kama ofa yake ingekuwa nzuri kuliko mtu mwingine yeyote hilo ndilo swali la kwanza kabla hatujaingia kwenye masuala ya kimsingi yaliyopo kwenye mkataba," 


Hoja zinazoibuliwa kutoka kwa wakosoaji hao ni pamoja na ukomo wa uwekezaji huo, ugumu wa kujitoa kwenye mkataba endapo kutatokea kutoelewana, huku kampuni ya DP World ikidaiwa kuwa na migogoro na baadhi ya mataifa iliyoingia makubaliano katika mikataba kama hiyo.


Katika mkutano huo wa hadhara Heche aliongoza na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini Jaffary Michael, Mstahiki Meya Mstaafu Raymond Mboya, na Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro Michael Kilawila.











0 Comments:

Post a Comment