Lori la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga likizuiwa katika mizani ya Njiapanda, Moshi kutokana na kuzidisha uzito. |
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini
(Tanroads) mkoani Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando, anadaiwa kukaidi amri ya
waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa wa kuliachailia gari la halmashauri ya wilaya
ya Mwanga, mkoani humo.
Kwa mujibu wa uongozi wa
halmashauri ya wilaya ya Mwanga, wamesemalori hilo limezuiliwa katika mizani ya
Njiapanda, wilaya ya Moshi kwa madai ya kuzidisha uzito.
Akiongelea swala hilo Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mwanga Mwajuma Nasombe amesema lori hilo
linashikiliwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa, licha ya kuwaomba waliachie huku
wakitafuta hela za kulipa faini hiyo jambo ambalo limekuwa shubiri.
“Lori hili tulilinunua ili kuongeza
mapato ya halmashauri kwa kusambaza madini ya mchanga pamoja na vifaa vya
ujenzi kwa wateja mbalimbali zikiwemo taasisi za umma”, alisema Nasombe.
Alisema “Gari hili lilipata kazi ya
kupeleka mchanga wilaya ya Rombo kwa ajili ya shughuli zinazofanywa na Wakala
wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA, lakini lilipofika mizani ya Njiapanda
lilonekana kuzidisha mzigo, na hivyo kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki mbili
sasa”, alisema.
Mkurugenzi huyo aliendelea kusema
ziko juhudi mbalimbali zilizofanywa na uongozi wa halmashauri hiyo ili liweze
kuachiliwa na kuendelea na shughuli huku uongozi wa halmashauri hiyo ukitafuta
fedha za kulipa faini wanayodaiwa kwa kuzidisha uzito bado hazijafanikiwa hadi
sasa.
“Tumewasiliana na wenzetu wa
Tanroads ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro ili waliachilie lakini haujafanikiwa”,
alisema Nasombe.
Alisema kuwa uongozi wa halmashauri
uliwasiliana na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, kuhusiana na
sakata hilo lakini pamoja na kufanya hivyo bado swala hilo halijaweza
kutatuliwa.
“Mbunge aliwasiliana na
Waziri wa Uchukuzi na taarifa tulizo nazo ni kuwa aliwasiliana na uongozi
wa Tanroads mkoa wa Kilimanjaro, kuhusiana na swala hilo ikiwemo Tanroads
waliachilie lakini hadi sasa halijaachiliwa kutokana na Meneja wa Tanroads
kutokutekeleza agizo la Waziri Mmbarawa”, alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia swala hilo,
Meneja wa Tanroads mkoani Kilimanjaro Mhandisi Kyando alisema swala hilo ni la
kiofisi na kushangazwa na kuhojiwa na mwandishi wa habari alipopata
taarifa hiyo.
“Umeona hiyo ndiyo stori, au
wamekutuma uwasemee? Zipo taratibu za kiserikali za kuwasiliana na si kupitia
kwa mwandishi wa habari”, alisema Kyando pale alipotakiwa na mwandishi wa
habari hizi kuzungumzia swala hilo.
Kwa upande wao baadhi ya Madiwani
wa halmashauri hiyo wameelezea kusikitishwa kwao na swala hilo ambalo walisema hata
kama kuna kasoro zilizojitokeza, linaweza kushughulikiwa bila mikwaruzo haswa
ikitiliwa maanani ya kuwa Tanroads, Tarura na halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
zote ni taasisi za serikali.
Akizungumzia sakata hilo, Diwani wa
Kata ya Kigonigoni Jeremiah Shayo alisema kuendelea kushikiliwa kwa lori hilo
kunaweza kuisababishia halmashauri hiyo hasara kubwa.
“Lori hili linatumia mfumo wa
umeme, likiendelea kukaa muda mrefu tena likiwa na mzigo mfumo wa uendeshaji
wake utaharibika na kuisababishia serikali kupitia halmashauri ya Mwanga kupata
hasara kubwa”, alisema Shayo.
0 Comments:
Post a Comment